Na MWANDISHI WETU – KASULU
WATENDAJI wa Halmashauri ya Mji wa Kasulu mkoani Kigoma, wametakiwa kupanga bajeti na mikakati yenye mrengo wa jinsia bajeti zao ziweze kuwanufaisha wananchi wote.
Ofisa Programu Ushawishi na Utetezi wa TGNP , Deogratius Temba alikuwa akizungumza kwenye warsha ya siku moja ya wakuu wa idara za halmashauri ya mji iliyoandaliwa na TGNP kwa kushirikiana na Shirika la Idadi ya watu Duniani (UNFPA) mjini Kasulu.
Alisema bajeti za halmashauri ni bajeti za wananchi kwa hiyo zinatakiwa kubeba sauti zao kwa ukamilifu.
“Halmashauri ndipo walipo watu, ni muhimu kusikia bajeti yao ikigusa mahitaji makuu ya wanawake na wanaume hasa katika eneo la maji, elimu, afya na kilimo.
“Suala la ukatili wa jinsia ni lazima tulipe kipuambele kwenye mipango yetu kwa sababu tunatekeleza mpango kazi wa taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Jinsia kwa wanawake na watoto,”alisema Temba.
Alisema ukatili wa jinsia ni eneo ambalo lisipopewa kipaumbele kuhakikisha unakoma hasa kwa wanawake na watoto, ni vigumu kwao kushiriki kwa ukamilifu katika shughuli za uchumi, na itakwamisha jitahada za serikali ya awamu ya tano ya kufikia uchumi wa kati na maendeleo ya watu.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mji, Simon Mahela, alisema halmashauri hiyo imekuwa ikijitahidi kutenga fedha kuwezesha wasichana wa sekondari kupata elimu bora.
Alisema kutokana na ushirikiano na elimu inayotolewa na TGNP na UNFPA wataweka nguvu zaidi kuhakikisha bajeti zao zinazingatia usawa wa jinsia.