Na Nyemo Malecela,Kagera
Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera imefanikiwa kupunguza kiwango cha udumavu kwa watoto chini ya miaka miwili baada ya kuweka mkakati wa kuhakikisha maafisa maendeleo ya jamii na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanasimamia lishe ya mtoto tangu akiwa tumboni mwa mama hadi atakapozaliwa na kufikisha umri wa miaka miwili kwa kuwafuata kwenye jamii.
Mkurungenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Fatina Laay amebainisha hayo kwenye kikao cha lishe cha Halmashauri hiyo cha robo ya kwanza ya mwaka kwa kusema kuwa waliamua kuwapangia maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kusimamia lishe ya wajawazito na watoto chini ya miaka miwili kwa kuwafuata nyumbani.
“Lishe bora inaanza wakati mtoto akiwa tumboni, hivyo wahudumu hao wa afya wanatakiwa kuhakikisha wanajua mama mjamzito anakula chakula gani, baada ya kujifungua mtoto ananyonyeshwa maziwa pekee kwa muda wa miezi sita na baada ya miezi sita anakula mlo kamili wenye makundi matano ya vyakula.
“Mwanzoni tatizo la udumavu lilisababishwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kukabiliwa na changamoto ya ufuatiliaji ngazi ya jamii lakini kwa sasa tumegawa majukumu ya kusimamia jamii kwa kila kata jambo ambalo linasaidia jamii kupata uelewa wa kutosha kuhusu lishe bora mara kwa mara,” alisema Laay.
Laay alisema wamekubaliana na wakuu wa idara wa Halmashauri hiyo kuwa ajenda ya lishe iwe ya kudumu kwenye vikao vyote vitakavyofanyika kwenye kata.
“Jamii ikiwa na lishe bora magonjwa nyemelezi yatapungua kwa jamii na hali hiyo itaisaidia serikali kupunguza bajeti ya kununua madawa hospitalini.
Maana watoto wakiwa na udumavu watakuwa wakipatwa na magonjwa nyemelezi mengi ata watakapokuwa wakubwa jambo litakalowalazimu kwenda hospitali mara kwa mara,” amesema.
Ameongeza kuwa atawaandikia barua watendaji wa vijiji na kata wote ili kuanzia sasa wawe wanawahusisha wahudumu wa afya ngazi ya jamii kwenye vikao vyote ili waweze kupanga mikakati ya kudumisha lishe katika jamii.
Naye Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Desdery Karugaba alisema kwa kuangalia viashiria vinavyopelekea udumavu kwa watoto, idadi ya watoto wenye utapiamlo katika Halmashauri hiyo kwa kila robo ya mwaka inazidi kupungua.
“Mfano robo ya Aprili hadiJuni, tulikuwa na watoto 80 lakini sasa hivi tuna watoto 50, hii ni kutokana na afua zilizotekelezwa ambazo zimesaidia uelewa kuhusu lishe kuongezeka na watoto wenye utapiamlo mkali kupungua.
Pia kiwango cha wakina mama wajawazito wanaohudhuria kliniki kinaridhisha japokuwa bado wapo wakina mama ambao hawahudhurii kliniki lakini ni wachache,” alisema Desdery.
Mbali na changamoto hizo pia Desdery alisema imewekwa mikakati ya kuhakikisha kila mama anahudhuria kliniki pale anapojigundua ana ujauzito, ambapo wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuhakikisha wanatembelea kaya zote ili kutoa elimu na kuwashawishi wajawazito hao kujua umuhimu wa kuhudhuria kliniki.
Desdery alisema changomoto kubwa wanayokabiliana nayo kwa sasa ni uelewa mdogo wa matumizi ya vyakula na mabadiriko ya mfumo wa maisha, ambao umesababisha wakina mama kuwa watafutaji jambo linalosababisha kuwa na muda mfupi wa kumfuatilia mtoto.
“Mfano unakuta mama ama vikundi hisa vitano, kwa hiyo siku tano za wiki atakuwa anahudhuria vikundi hivyo, je una uhakika gani wakati mama anahudhuria shughuli za vikundi mtoto alikuwa anapatiwa lishe inavyostahili?
“Mama wamekuwa ni watafutaji wakubwa wa fedha za kutunza familia jambo ambalo linawalazimu wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutoa elimu kwa mwanaume ili waone umuhimu wa kushirikiana na mama katika malezi ya mtoto endapo mmojawapo atakuwa katika majukumu ya kutafuta fedha mwingine aweze kumwangalia mtoto kwa ukaribu,” amesema.