NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM
HALI ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, imezidi kuimarika ambapo kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.
Rage alipata ajali juzi mkoani Dodoma, akiwa pamoja na majeruhi wenzake wanne walilazwa katika hospitali ya mkoa huo kabla ya kuhamishiwa Aga Khan.
Akizungumza Dar es Salaam jana akiwa hospitalini hapo, Rage alisema anaendelea vizuri ambapo kwa mujibu wa daktari alisema itamchukua wiki tatu kupona kabisa bega lake.
“Nashukuru naendelea vizuri na naendelea kupata huduma, daktari ameniambia baada ya wiki tatu nitakuwa nimepona kabisa hivyo naendelea na matibabu,” alisema.
Akizungumzia ajali hiyo, Rage alisema dereva wa gari lao alikuwa anataka kulipita lori lakini ghafla dereva wa lori hilo akaingia katikati ya barabara.
“Hata hivyo, tunamshukuru sana dereva wetu kwa kuwa alipoona hivyo, badala ya kuligonga lori aliamua kwenda pembeni ndipo gari letu liliporuka na kuingia kwenye korongo likapinduka,” alisema.
Rage aliteguka bega la kushoto huku Munde akipata majeraha kichwani, usoni na kuvunjika mkono, majeruhi wengine wanaendelea na vipimo.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kabla ya kuanza kwa vikao cha Bunge hilo alitoa taarifa kuhusiana na wabunge hao kupata ajali.
“Kutokana na wenzetu kupata ajali uongozi wa Bunge hili, umeamua kuwasafirisha wajumbe hao kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi,” alisema.
Rage na Munde walikuwa wamelazwa katika wodi namba 18 Grade one, chumba namba moja na mbili wakiwa na majeraha mbalimbali mwilini.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Ezekiel Mpuya alisema vipimo vilionyesha Munde pamoja na kupata majeraha usoni na kichwani pia alivunjika mkono wakati Rage ameteguka bega la kushoto. Alisema hadi jana hali zao zilikuwa zinaendelea vizuri na wangeruhusiwa.