Waandishi Wetu, Bujumbura na Dar
JARIBIO la mapinduzi lilifanyika jana nchini Burundi kumpindua Rais Pierre Nkurunzinza kupinga mpango wake wa kugombea urais kwa muhula wa tatu.
Maelfu ya watu walimiminika katika mitaa ya mji mkuu wa taifa hilo, Bujumbura, kushangilia tangazo la mapinduzi lililotolewa na Meja Jenerali Godefroid Niyombare.
Hata hivyo, matokeo ya mapinduzi hayo yalikuwa mbali na uhalisia.
Uamuzi wa Jenerali Niyombareh ambaye alitimuliwa na Nkurunzinza kama mkuu wa usalama Februari mwaka huu, unatokana na kile alichokiita mpango haramu wa rais wa kuinajisi katiba kwa kutaka kuongoza kwa muhula wa tatu.
Niyombareh, ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Usalama wa Burundi alikuwa balozi wa Burundi nchini Kenya, alisema kamati ya taifa ya ukombozi ya watu watano imeundwa kuliongoza taifa hilo kwa muda.
Na wakati hayo yanatokea Rais Nkurunziza alikuwa Dar es Salaam akikutana na viongozi wenzake wa Afrika Mashariki kujadili mgogoro unaolikabili taifa hilo.
Taarifa zilisema baadaye Rais Nkurunzinza alikuwa akijaribu kurudi nchini mwake
Ofisi ya Rais yakanusha
Vilevile, Ofisi ya Rais nchini Burundi ilituma ujumbe katika mtandao wa jamii pamoja na taarifa rasmi ikikana kuwapo mapinduzi kabla ya kusema kuwa mapinduzi yameshindwa.
Katika mfululizo wa taarifa zake kwenye mtandao wa Twitter, Ofisi ya Rais awali ilisema hali imedhibitiwa na kuwa hakuna mapinduzi na kisha ikasema jaribio la mapinduzi limeshindwa.
Msemaji wa Rais, Willy Nyamitwe aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa wanajeshi watiifu kwa Rais Nkurunziza wanaidhibiti nchi na kuwa Jenerali Niyombareh na washirika wake wanasakwa.
Msemaji wa Rais alisema Nkurunziza atalihutubia taifa atakaporudi nyumbani na kwamba hahofii chochote.
Taarifa nyingine ya Ofisi ya Rais ilisema; “Kwa masikitiko makubwa tumebaini uwapo wa kundi la askari walioasi asubuhi (jana) hii na kutoa kauli ya mapinduzi.”
“Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Burundi inautangazia umma wa taifa na kimataifa kuwa jaribio hili la mapinduzi lilidhibitiwa na watu hawa waliotangaza mapinduzi kupitia vituo binafsi vya redio wanatafutwa na majeshi ya ulinzi na usalama wafikishwe katika vyombo vya sheria.
“Ofisi ya Rais inaomba umma wa Warundi na wageni wanaoishi Burundi kukaa kwa amani na utulivu. Kila kitu kinatekelezwa na hivyo usalama katika mipaka yote ya nchi inadhibitiwa,” taarifa ilisema.
Hata hivyo, maelfu ya waandamanaji wanaopinga mpango wa Rais Nkurunzinza kugombea urais kwa muhula wa tatu walimiminika katika mitaa ya mji mkuu wa Burundi, kushangilia taarifa hizo walizoziita ushindi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon alizitaka pande zote zinazopingana kuwa katika hali ya uvumilivu na kutumia busara kutatua mzozo huo.
Wakati upinzani ukipinga muhula wa tatu kuwa ni kinyume na katiba na makubaliano ya amani ya mjini Arusha, chama tawala cha Nkurunzinza cha CNDD-FDD kimekuwa kikisisitiza kuwa rais ana haki hiyo kwa vile muhula wa kwanza aliteuliwa na bunge hivyo kutohesabika kikatiba.
Mwandishi wa BBC, Maud Jullien aliyeko mjini Bujumbura alisema maelfu ya waandamanaji walionekana wakielekea katikati ya jiji wakiongozana na wanajeshi na vifaru baada ya mapinduzi hayo kutangazwa.
Lakini polisi waliwarushia risasi wanajeshi hao na umati na kusababisha vifo vya waandamanaji wawili.
Waandamanaji waliendelea kusonga mbele wakiliambia BBC kuwa huo ulikuwa ushindi baada ya wiki kadhaa za maandamano yao.
Walijaribu kuingia katika ofisi za shirika la utangazaji la taifa ambalo lilikuwa bado liko chini ya askari watiifu kwa rais.
Kulikuwa na ripoti kuwa askari wanaounga mkono mapinduzi waliokuwa wakijaribu kuingia katika jengo hilo walikabiliwa na upinzani mkali.
Ripoti nyingine zilikuwa zikisema kuwa askari watiifu kwa rais na wale wanaounga mkono mapinduzi walikuwa katika majadiliano.
Waandishi wa BBC waliripoti kuwa waandamanaji walivunja gereza kuu na kuachia waandamanaji waliokuwa wamekamatwa siku za nyuma kabla ya kuliteketeza jengo hilo kwa moto.
Mashuhuda walisema waandamanaji walikusanyika katika vizuizi vya barabara, ambako walizuiwa kuelekea katikati ya jiji na askari, lakini hali hiyo haikuzuia umati kushangilia.
Safari zote za ndege zafutwa
Jenerali Niyombareh, wakati akisoma taarifa yake kwa waandishi wa habari akiwa katika kambi ya jeshi, alisema hakuutambua uongozi wa Nkurunziza kwa sababu mpango wake wa kugombea kwa muhula wa tatu unakiuka katiba.
Akitangaza katika kituo binafsi cha redio, Jenerali Niyombareh alisema: “Umma umeamua kuingilia kati hatima ya taifa lao kuondoa mazingira haya yasiyo ya katiba ambayo Burundi inaonekana kuangukia
“Umma kwa kauli moja unakataa kabisa mpango wa muhula wa tatu wa Rais Nkurunziza…Rais Pierre Nkurunziza ameondolewa katika wadhifa wake. Serikali imepinduliwa,” alisema katika taarifa yake iliyoshangiliwa na waliomsikiliza.
Kamati ya Ukombozi wa Taifa ya Jenerali Niyombareh inahusisha majenerali wengine wa jeshi na polisi.
Alisema kwamba kazi ya chombo hicho itakuwa kurudisha umoja wa taifa na kuendesha mchakato wa uchaguzi katika mazingira ya haki na amani.
Nkurunziza aondoka Dar
Rais huyo wa Burundi ambaye alitua Dar es Salaam jana kushiriki mkutano wa viongozi wa wakuu wa nchi za EAC uliokuwa ukijadili ya siasa Burundi, alijikuta akiahirisha kushiriki kwenye mazungumzo baada ya kupata taarifa za mapinduzi nchini mwake.
Nkurunziza aliyetua saa 6.00 mchana na kufikia katika Hoteli ya Serena, aliondoka saa 11 jioni baada ya kuwapo taarifa kwamba waasi walizimwa na jeshi linalomtii.
Taarifa zilisema kuwa baada ya kuzima uasi huo Rais Nkurunziza alitakiwa kurejea nchini mwake haraka hali iliyofanya asihudhurie mkutano wa Dar es Salaam.
Aliondoka hotelini hapo akiwa katika msafara wa magari 12 yaliyokuwa ykiwahusisha wana usalama wa Burundi na wengine kutoka nchini.
Kabla ya kufika hotelini hapo MTANZANIA lilifika katika ubalozi wa Burundi saa 10.00 lakini hakuwapo kiongozi yeyote.
Wananchi Burundi
Wakati huohuo, raia wa Burundi wakizungumza kwa simu kutoka Bujumbura, walitoa kauli mbalimbali huku wengi wakifurahia kitendo cha jeshi hilo kumpindua Rais Nkurunziza na kudai kuwa maisha yao hivi sasa yako katika mikono salama.
Pamoja na mambo mengine wananchi hao wameeleza kuwa muda mfupi baada ya mapinduzi hayo kufanyika kituo binafsi cha Redio cha RPA kilichokuwa kimefungwa na Serikali kilifunguliwa.
Baadhi ya raia waliozungumza na MTANZANIA kwa sharti la kutotajwa majina kutoka nchini humo walisema kutokana na madhila makubwa waliyoyapata na baadhi ya ndugu zao kupoteza maisha ni vema kiongozi huyo asirejee nchini Burundi kwa ajili ya kulinda usalama wake.
Mmoja wa raia hao alisema; “Huku leo tunafuraha kubwa tunamshukuru Mungu sana huyo Rais (Pierre Nkurunziza), wamemtoa wamembakiza huko huko kwenu.
“Hali ya huku ni nzuri kabisa, nzuri sana ni furaha na makelele kila kona watu wamefurahi hakuna mfano”.
Alisema baada ya jeshi hilo kumpindua Rais Nkurunziza baadhi ya polisi walianza kurusha risasi, lakini jeshi hilo liliwadhibiti.
“Polisi wanarusha risasi lakini haziwezi kufanya kitu kwa sababu watu wote wameshatoka barabarani na jeshi limekamata nchi. Hata ile redio yetu ya raia ambayo ilikuwa inafikisha taarifa ambazo Serikali iliziona mbaya na kuifunga imeshafunguliwa sasa.
“Mumpe Rais Nkurunziza ndaro (sehemu ya kuishi), akija huku raia wanaweza kumuua kutokana na uchungu na hasira walizo nazo,”alisema raia huyo huku akiwa na furaha kubwa.
Butiku
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema suala hilo liko mikononi mwa marais wa nchi za EAC hivyo wanapaswa kuachwa kwanza wamalize mazungumzo ya kushughulikia suala hilo.
“Huwezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu tayari lipo mikononi mwa viongozi wakuu wa serikali, kufanya hivyo ni kwenda kinyume na itifaki, hivyo basi tunapaswa kuwaacha kwanza wamalize kazi yao,”alisema Butiku.
WASOMI
Baadhi ya wasomi na wanasiasa nchini wamesema jeshi hilo lilipaswa kuwa na subira hasa katika kipindi hiki ambacho viongozi wa Afrika Mashariki wanaendelea na mazungumzo ya kutafuta muafaka kuhusiana na mgogoro wa Burundi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, wasomi hao walisema kuwa viongozi wa nchi hizo wamekutana kujadiliana suala hilo, hivyo basi walipaswa kusubiri .
“Uamuzi wa jeshi la nchi hiyo kumpindua rais wao wakati mazungumzo bado yanaendelea siyo wa kuungwa mkono,”alisema Dk. Benson Bana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Mbwete
Rais wa Baraza la Chuo Kikuu cha Afrika, Profesa Tolly Mbwete alisema ikiwa jeshi limeamua kufanya hivyo linapaswa kusimamia suala la uchaguzi liweze kufanyika mapema na wananchi waendelee kutawaliwa na raia.
“Jeshi kutawala siyo vizuri ila wanapaswa kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika ndani ya siku mbili hizi waweze kurudisha utawala wa kiraia kwa wananchi,” alisema Profesa Mbwete.
Profesa Baregu
Naye Mhadhiri wa Chuo cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesigwa Baregu, alisema hali hiyo ilionekana ingeweza kutokea tangu awali kutokana na msimamo wa Rais Nkurunziza kuanza kuleta machafuko na uvunjifu wa amani.
Alisema viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) wanatakiwa kuendelea na jitihada zao za kumtaka Rais Nkurunziza kuachana na msimamo wake na kuhakikisha kuwa utawala wa Jeshi haujiandai kuota mizizi.
Kituo cha Sheria
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema kitendo cha jeshi la nchi hiyo kumpindua rais wao ni kukosa uvumilivu.
“Jeshi limekosa uvumilivu uliosababishwa na Rais Nkurunziza, kitendo hicho ni cha hatari zaidi hatuwezi kukiunga mkono kwa sababu kunaweza kuhatarisha maisha ya wananchi hasa pale watakapoamua kuiendesha nchi hiyo kijeshi,” alisema Dk. Bisimba.
WANASIASA
Katibu Mkuu wa cha NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, alitilia shaka mapinduzi hayo kwa kusema kuwa inawezekana Rais Nkurunziza amekula njama na jeshi hilo.
“Mimi nina mitizamo miwili tofauti, inawezekana Rais Nkurunziza amekula njama na jeshi lake aonekane kupindua nchi halafu baadaye waje wampe tena urais au pengine jeshi limeona liungane na raia na kukataa udhalimu unaofanywa na Nkurunziza,” alisema Nyambabe.
Mziray wa PPT
Mwenyekiti wa chama hicho, Peter Mziray, alilipongeza jeshi la Burundi na kutaka busara itumike zaidi kurejesha amani nchini humo.
Alisema ingawa mapinduzi si jambo jema lakini yako yaliyoleta neema kama yale ya ujamaa yaliyofanyika Urusi.
“Huwezi kupiga kura wakati mtu anataka kujiongezea muda na Burundi isiyotulia ni matatizo kwa Tanzania hivyo tunapenda kuona ikitulia,” alisema Mziray.
Askofu Niwemugizi
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Severine Niwemugizi, alisema jambo hilo lilitegemewa kwa vile ziko baadhi ya nchi zenye migogoro ya utawala ambazo ziliwahi kupinduliwa.
“Ukiwa legelege na kukiwa kuna kusuasua lazima atatokea mtu aweze kusimama katika ombwe lililojitokeza kama lilivyofanya jeshi la Burundi,” alisema Askofu Niwemugizi.
Sheikh Alhad
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema kilichotokea Burundi ni matukio ya viongozi kutojali makubaliano.
“Nkurunziza amevuna alichokipanda na hili ni tatizo la viongozi wengi wa Afrika wana ‘maradhi’ ya kutoheshimu katiba zao. Tujifunze kuheshimu makubaliano,” alisema Sheikh Alhad.
Viongozi EAC walaani
Akizungumza walichokubaliana kwenye mkutano wao, Mwenyekiti wa Wakuu wan chi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Kikwete alisema, viongozi wa jumuiya hiyo wamelaani vikali mapinduzi nchini Burundi.
Alisema njia hiyo haikubaliki na haiwezi kusaidia Burundi kutatua matatizo yanayoikabili kwa sasa.
Pia alisema pia viongozi hao wamekubaliana na kuishauri Tume ya Uchaguzi ya Burundi, isogeze mbele uchaguzi mkuu uliotarajiwa Juni mwaka huu mpaka hali ya usalama nchini humo itaporejea.
“Usalama ukisharejea, uchaguzi ufanyike ukizingatia Makubaliano ya Mkataba wa Arusha na Katiba,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete makubaliano mengine ni kuwa viongozi hao watakutana baada ya wiki mbili kutathimini hali itakavyokuwa katika taifa hilo.
Baada ya kuzungumza hayo, Rais Kikwete alisimama na wenzake kwa hali ya kutoruhusu maswali.
“Mlango ulio nyuma yenu mtapata chakula, karibu,” alisema Rais Kikwete huku akiwa amesimama akijiandaa kutoka nje ya ukumbi.
Hali ilivyokuwa awali
Ilipofika saa 6:56 mchana, Rais Jakaya Kikwete aliwasili kwenye ukumbi maalumu wa mikutano uliopo Ikulu kusubiri wageni wake.
Wa kwanza kuwasili kwenye eneo hilo alikuwa Makamu wa Rais wa Afrika Kusini, Cyri Ramoposa, aliyefuatiwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenya aliyefika saa 8:15 mchana ambako baada ya aliwasili Rais wa Rwanda, Paul Kagame aliyefika saa 8:29 huku Rais wa Uganda, Yoweri Museven akiwasili saa 8:36.
Baada ya viongozi hao kufika, waliingia kwenye chumba maalumu huku wageni wangine wakiwa nje kusubiri kuwasili kwa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza.
Baada ya muda hali kwenye eneo hilo ilibadilika kutokana na kuzagaa kwa taarifa za kupinduliwa kwa kiongozi huyo.
Maofisa wengine waliokuwa kwenye eneo hilo ambao ni wale wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walioandaa mkutano huo, maofisa wa nchi ambazo viongozi wao walikuwa kwenye eneo hilo na waandishi wa habari, kila mmoja alionekana akifuatilia taarifa kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kupitia simu za mikononi.
Wakati hali hiyo ya sintofahamu ikiendelea, Rais Kikwete alitoka nje ya ukumbi huo wa mkutano na kuwaacha wageni wake.
Kiongozi huyo alikaa nje kidogo ya ukumbi huo, akizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe pamoja na Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Othuman Rashid.
Baada ya mazungumzo hayo yalichukua takribani dakika tano, Rais Kikwete alirudi ndani ya ukumbi, hali hiyo iliongeza minong’ono nje ya ukumbi huo.
Marais hao waliendelea kukaa kwenye chumba cha mkutano mpaka saa 11:02 walipotoka na kupiga picha ya pamoja kisha Rais Museven akaondoka na wenzake wakarudi kwenye chumba cha mkutano.
Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Nkonzana Zuma, Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika nchi za Maziwa Makuu, Said Djinditi.
Meja Jenerali Niyombare ni nani?
Niyombare aliteuliwa kuwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Burundi mwaka 2014 akichukua nafasi ya Adolphe Nshimirimana, akiwa anatokea Kenya kama balozi wa Burundi.
Jenerali huyo anaelezwa kama ‘mwenye nidhamu’, akili, ‘mnyumbulifu’ na ‘muamini wa kweli,’
Alihesabiwa kama ‘mwenye maono’ kwa kazi zake kama ubalozi na wakati alipoajiriwa na CNDD-FDD na Jeshi la Ulinzi la Taifa la Burundi (FDN).
Lakini alitimuliwa na Nkurunziza kama mkuu wa usalama Februari 2015 bila kutolewa sababu za uamuzi huo.
Lakini ripoti zinasema alijiuzulu kutoka wadhifa wake wa mkuu wa polisi wa urais baada ya ripoti kuibuka kuwa Nkurunziza amejipanga kugombea muhula wa tatu.
Niyombare daima amekuwa akiita mpango huo wa rais kuwania muhula wa tatu ‘usio wa katiba.’
Katika makala iliyopo kwenye mtandao wa Gahuza.com, Niyombare amemwagiwa sifa kwa kuinua wasifu wa ubalozi wa Burundi nchini Kenya.
Makala hayo yalimweleza jenerali huyo kama kiongozi mwenye bashasha ambaye ushawishi wake haumzuii kupata mafanikio katika jukwaa la taifa la siasa na jamii.
Mwaka 2010 Niyombare alitangaza kuwa askari 12 na ofisa mmoja wa jeshi walikamatwa wakati wakiendesha mkutano karibu na Ziwa Tanganyika ambako walipanga kumpindua Rais Nkurunziza.
Nkurunzinza ni nani?
Nkurunziza alizaliwa Desemba 18, 1963 mjini Bujumbura katika familia ya Wahutu. Alisoma shule ya msingi kwenye mkoa wa Ngozi.
Babaye Eustache Ngabisha alikuwa mbunge wa Burundi mwaka 1965 akaendelea kuwa mkuu wa mkoa katika mikoa miwili.
Mzee Ngabisha aliuawa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1972 pamoja na Warundi wengine 400,000.
Nkurunziza alilelewa pamoja na ndugu saba, watano kati yao waliuawa wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya 1993 au wakipigania kama askari wa kundi la CNDD-FDD. Leo hii ana dada mmoja aliye hai.
Nkurunziza alikuwa mwalimu wa Chuo Kikuu cha Burundi wakati vita ya wenyewe kwa wenyewe, ambayo ilianza baada ya kuuawa kwa Rais wa kwanza aliyechaguliwa kutoka kabila la Wahutu, Melchior Ndadaye 1993.
Baada ya shambulio ya jeshi dhidi ya Wahutu kwenye chuo kikuu alijiunga na chama cha Baraza la Kitaifa kwa Kutetea Demokrasia, Burundi (CNDD-FDD) mwaka 1995.
Alijiunga na kundi hilo ambalo baadaye liligeuka chama cha siasa nay eye kama askari alipanda ngazi hadi katibu, baadaye makamu mwenyekiti wa CNDD-FDD mwaka 1998 na mwishowe mwenyekiti mwaka 2001.
Mwaka 2004 katika mahojiano na Shirika la Habari la IRIN, alikumbushia matukio ya kuogopesha aliyowahi kukutana nayo:
“Mwaka 1995, jeshi la Kitutsi lilishambulia kampasi za chuo kikuu na kuua wanafunzi 200. Walijaribu kuniua pia.”
“Washambuliaji walililenga gari langu lakini nilifanikiwa kuchomoka kutoka kwenye gari na kukimbia. Walililipua gari langu. kisha nikajiunga na CNDD-FDD kama askari. Vita hii ililazimishwa kwetu; hatukuianza.”
Baada ya mapatano ya amani ya mwaka 2003 alikuwa waziri wa utawala katika serikali ya mpito ya Rais Domitien Ndayizeye.
Baada ya ushindi wa CNDD-FDD katika uchaguzi wa mwaka 2005 alichaguliwa na bunge kuwa rais kabla ya kuchaguliwa katika uchaguzi mwaka 2010 ambao ulisusiwa na chama kikuu cha upinzani kwa madai ya kuwapo njama za kuuhujumu kwa maslahi ya chama tawala.
Mwaka 2015 alitangaza kwamba alitaka kugombea urais tena hatua ambayo imesababisha maandamano na uasi wa sasa kwa vile wapinzani walidai kufuatana na katiba ya nchi anastahili vipindi viwili tu.
Mwenyewe pamoja na chama chake anadai kwamba mara ya kwanza alichaguliwa na bunge na kikatiba anastahili kuchaguliwa mara mbili na wananchi wote.
Kwa upande wa maisha binafsi; Nkurunziza anajielezaa kama mlokole na shabiki wa michezo.
Hufurahia kucheza soka na kuendesha baiskeli. Alianza kucheza mpira wa miguu akiwa na umri wa miaka mitano na alichezea timu ya shule ya sekondari na chuo kikuu.
Kama mhadhiri wa chuo kikuu, Nkurunziza alitumia vipaji vyake vya mpira wa miguu kuwa kocha wa ‘Union Sporting’, timu ya daraja la kwanza.
Akiwa Rais aliwakusanya baadhi ya wachezaji wenzake wa zamani na kuunda timu mpya ya veterani ijulikanayo ‘Helleluia FC’ mwaka 2004. Na wakati akiwa Waziri, Nkurunziza aliwahi kuunda “Soccer Academy ” kituo cha soka ambacho watoto 300 kutoka kote Burundi walipata mafunzo mbalimbali.
Pierre Nkurunziza alimuoa mkewe mwaka 1994 na ana watoto watano.
Historia ya harakati za Amani Burundi
Mandhari ya siasa ya Burundi mbali ya demokrasia imetawaliwa na vita za wenyewe kwa wenyewe na mchakato mrefu wa kusaka Amani.
Mchakato huo mrefu wa amani unaanzia mwaka 1993 baada ya rais mhutu aliyechaguliwa kidemokrasia Melchior Ndadaye kuuawa na Watutsi wenye msimamo mkali.
Novemba 1995, marais wa Burundi, Rwanda, Uganda, na Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) walitangaza mpango wa majadiliano ya amani nchini Burundi chini ya Hayati Mwalimu Nyerere.
Julai 1996, Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya alirudi madarakani kwa njia ya mapinduzi yasiyo ya kijeshi.
Buyoya alijitangaza kuwa rais wa jamhuri ya mpito, huku akiliweka kando Bunge la Taifa na kuharamisha makundi ya upinzani na kutangaza hali ya hatari.
Mapinduzi hayo yalilaaniwa vikali na viongozi wa mataifa jirani na kumwekea vikwazo vya kiuchumi wakimtaka arudishe serikali ya kikatiba.
Buyoya alikubali mwaka 1996 kuhalalisha vyama vya siasa.
Hata hivyo, mapigano baina ya jeshi lililotawaliwa na Watutsi na makundi ya wanamgambo wa Kihutu ikiwamo CNDD-FND yaliendelea.
Kama sehemu ya shinikizo kutokana na mazungumzo ya amani Juni 1998, Buyoya aliunda katiba ya muda na kutangaza ushirika baina ya serikali na bunge lililodhibitiwa na wapinzani.
Baada ya kifo cha msuluhishi Nyerere Oktoba 1999, viongozi wa ukanda huo wakamteua Rais mstaafu wa Afrika Kusini marehemu Nelson Mandela kuwa mwezeshaji mpya wa mazungumzo ya amani ya Arusha.
Chini ya Mandela makubaliano yakafikiwa mwaka 2005.
Lakini Aprili 2015 ikiwa miaka 10 tangu kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe, mapambano yakaibuka kupinga uamuzi wa chama cha Nkurunziza kutangaza kuwa atawania muhula wa tatu.
Historia ya viongozi wa Burundi
Burundi ilipata uhuru kutoka Ubelgiji Julai Mosi, 1962 chini ya Waziri Mkuu Pierre Ndendandumwe, ambaye hata hivyo alikuja uawa na Mtutsi wa Rwanda Januari 15, 1965.
Taifa hilo likapata Rais wa kwanza Michele Micombero hapo Novemba 28, 1966.
Lakini Aprili 27, 1972 kukaibuka mauaji ya kimbari ya Burundi baada ya kuibuka uasi uliosababisha mauaji hayo dhidi ya Wahutu.
Novemba 2, 1976. Jean-Baptiste Bagaza akawa Rais wa Burundi kufuatia mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu, kabla hajaangushwa Septemba 3, 1987 wakati akiwa ziarani Canada.
Kufuatia mapinduzi hayo, Oktoba 2, 1987 Meja Pierre Buyoya akaapishwa kuwa Rais mpya wa Burundi na katiba mpya ikapitishwa Machi 1992.
Uchaguzi wa urais ukaitishwa Juni 2, 1993, ambako Melchior Ndadaye kutoka jamii ya Wahutu alishinda uchaguzi huo, kabla ya kuuawa Oktoba 21 mwaka huo huo na Watutsi wenye msimamo mkali.
Kifo chake kikaibua vita ya wenyewe kwa wenyewe na mauaji ya kimbarti dhidi ya Watutsi.
Februari 5, 1994 Cyprien Ntaryamira aliingia madarakani kama Rais wa Burundi kabla ya kufa akiwa pamoja na Rais wa Rwanda Juvernal Habyarimana.
Viongozi hao walikufa Aprili 6 mwaka huo baada ya ndege yao iliyokuwa ikikaribia kutua kwenue uwanja wa ndege wa Kigali, Rwanda kudunguliwa wakati wakitokea Dar es Salaam.
Tukio hilo pia lilisababisha mauaji mabaya zaidi ya kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani yaliyodumu kwa siku 100.
Aprili 8 mwaka huo, Sylvestre Ntibantunganya akatangazwa kuwa Rais wa muda wa Burundi lakini alinusurika kupinduliwa Aprili 25.
Akachaguliwa kuongoza serikali ya maridhiano Septemba 30 mwaka huo.
Machi 11, 1995, Waziri wa Nishati na Madini, Ernest Kabushemeye aliliwa na wala nyama za watu mjini Bunjumbura kabla ya miezi minne baadaye waasi wa Kihutu kushambulia kambi ya wakimbizi na kuua watu zaidi ya 300 Julai 21, 1996.
Taarifa hii imeandaliwa na Shaban Matutu, Mauli Muyenjwa, Patricia Kilemeta, Fred Azzah na Jonas Mushi