29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

HALI ILIVYOKUWA ENEO LA MKUTANO

Na Waandishi Wetu – Dar es Salaam


SAA saba mchana waandishi wa habari takribani 200 walikuwa tayari wamekusanyika katika Hoteli ya Protea wakimsubiri aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye kupitia mitandao ya kijamii alitoa taarifa ya kutaka kuzungumza nao.

Kwa mujibu wa waandishi wenyewe, idadi hiyo ni kubwa na hawajawahi kuishuhudia katika mkutano wowote katika siku za hivi karibuni.

Wakati waandishi wakimsubiri hotelini hapo, saa 7:33 mchana zilianza kusambaa taarifa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kwamba Nape alikuwa amekamatwa na kupelekwa kusikojulikana.

Wakati kukiwa na taarifa hizo, saa 7:52 alitokea Meneja wa hoteli hiyo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Suleiman na kuwataka waandishi watawanyike kwa kile alichodai kuwa ni agizo la Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Susan Kaganda.

Agizo hilo liliwashtua waandishi ambao walianza kuhoji kulikoni, kwani kabla ya kauli ya meneja huyo, tayari Nape mwenyewe aliandika kupitia ukurasa wake wa Twitter, akiwataka watu waache uongo na kwamba alikuwa njiani akielekea Protea.

“Wanasambaza nimekamatwa! Niko njiani nakwenda Protea, niko salama, nimetoka Arusha na ndege mchana huu, nashauri waache uongo watulie,” lilisomeka andiko hilo la Nape.

Ujumbe huo uliwafanya waandishi wa habari wamuhoji zaidi meneja wa hoteli hiyo, wakitaka kufahamu ukweli wa kauli hizo mbili.

 “Jamani mimi sielewi chochote, nimepigiwa simu na RPC ameniambia muondoke hakutakuwa na mkutano hapa,” alisema meneja huyo.

Hata hivyo jibu hilo bado halikuwaridhisha waandishi na mahojiano kati yao yalikuwa kama ifuatavyo:

Mwandishi: Nani aliomba nafasi ya kufanya mkutano hapa na je, umemtaarifu kuhusu kuzuiwa kwa mkutano wake?

Meneja: Huu ukumbi aliyeomba ni Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Radio, Ruge Mutahaba, ambaye nimewasiliana naye na kumpa taarifa hii.

Mwandishi mwingine: Sisi tunachofahamu anayekuja kuzungumza hapa ni Nape, sasa Ruge anaingiaje hapo?

Meneja: Mimi sifahamu hilo, aliyeomba ukumbi ni Ruge na si Nape.

Mwandishi: Ruge aliomba nafasi ya kufanya mkutano hapa lini na saa ngapi?

Meneja: Alinipigia simu leo asubuhi akisema anaomba kuja kufanya mkutano leo (jana) saa nane, tukafanya maandalizi kama alivyoagiza.

Mimi siwezi kufanya maandalizi ya mtu kuweka mkutano wake hapa halafu baadaye nimfukuze, nimeagizwa na nimefikisha ujumbe kama nilivyowaambia.

Mwandishi: Hebu tuonyeshe namba ya simu ya Ruge, tuthibitishe kama kweli uliongea naye.

Meneja: Unaijua namba ya Ruge? (alimuuliza mwandishi).

Waandishi: Ndiyo, tuonyeshe.

Meneja huyo akatoa simu yake mfukoni na kuonyesha namba ya Ruge ambayo kweli ilionyesha mawasiliano yao.

Baada ya mazungumzo hayo ambayo yalidumu takribani kwa robo saa, waandishi walianza kumtafuta Nape kujua alipo.

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile ambaye naye alikuwapo katika viunga vya hoteli hiyo, baada ya taarifa hizo za kukanganya alilazimika kumpigia simu Nape.

Nape alisikika akisisitiza kuwa yuko njiani anakuja na kuwataka waandishi wa habari kuendelea kumsubiri.

 “Niko njiani nakuja, nisubirini msiondoke, hata nje tutazungumza, ikishindikana tutakwenda nyumbani kwangu,” alisikika Nape katika mazungumzo yake na Balile.

Baada ya kukata simu, Balile aliwaambia waandishi kwamba Nape anakuja wasiondoke.

Waandishi waliendelea kusubiri katika eneo hilo, lakini kwa hofu kubwa, wengi mawazo yao yalikuwa juu ya kuvamiwa na polisi na kuanza kusambaratishwa.

Saa 14:20, Nape alifika hotelini hapo, lakini aliishia nje baada ya kuzuiliwa kuingia ndani.

Waandishi walianza kukimbia kuelekea upande wa geti la hoteli hiyo, huku wakiuliza kulikoni. Wengine walijibu “polisi hao” na wengine wakajibu “Nape amekuja”.

Wakati huo, waandishi walionekana kusukumana mithili ya watu walioona hatari mbele yao na katika msafara huo alikuwapo pia Suleiman (meneja wa hoteli), ambaye naye alikuwa akielekea nje.

Suleiman alipofika getini, aliwaamuru walinzi kuzuia gari lolote kuingia ndani ya hoteli hiyo.

 “Hakikisha hakuna gari litakaloingia hapa; magari yatoke lakini yasiingie,” alisikika meneja huyo wa hoteli akiwaagiza walinzi ambao walitii agizo hilo.

 

Habari hii imeandaliwa na waandishi ESTHER MBUSSI, HAMISA MAGANGA NA ASHA BANI

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=oEdovxg2Fn0[/embedyt]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles