24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Hakuna namna lazima wakae

YANGA

NA ZAINAB IDDY,

HAKUNA namna lazima wakae tu, ndivyo tunavyoweza kusema pale wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Yanga leo watakaposhuka dimbani dhidi ya Medeama kutoka Ghana mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Huu ni mchezo wa tatu kwa Yanga katika harakati za kuwania Kombe la shirikisho hatua ya makundi. Michezo miwili ya awali ilikuwa ni dhidi ya Mo Bejaia ya Algeria ambako ilipoteza kwa bao 1-0 kabla ya kupoteza nyumbani kwa idadi kama hiyo dhidi ya TP Mazembe.

Medeama itawakabili Yanga huku ikiwa imepoteza mchezo mmoja mbele ya Mazembe kwa kufungwa mabao 3-1 mjini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), kisha kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Mo Bejaia.

Katika mchezo huo, Yanga inahitaji matokeo ya ushindi mbele ya Medeama ili kurejesha imani yake kwa Watanzania, lakini pia kujiweka mazingira mazuri ya kuingia katika hatua ya nusu fainali kwenye michuano hiyo.

Kutokana na umuhimu wa mchezo huo, Kocha wa Yanga, Hans van de Plujim na benchi la ufundi wameweka mikakati thabiti ya kuhakikisha wapinzani wao hao hawatoki salama kwa kuwanoa vilivyo mastraika wao tegemeo.

Kwa mujibu wa kocha Hans, moja ya mipango yake ni kuona mastraika wake hawafanyi makosa katika harakati za kufunga kwa kila nafasi zitakazopatikana.

“Tumekuwa tukipoteza nafasi nyingi katika sehemu ya ufungaji jambo ambalo mara kwa mara limekuwa likitugharimu, kwa kipindi chote tangu kumalizika mchezo wetu na TP Mazembe, tumekuwa tukisisitiza suala la ufungaji.

“Kwa asilimia kubwa naamini tumeweza kulimaliza hasa baada ya kuwanoa vilivyo washambuliaji wetu pamoja na kuijenga vizuri safu ya ulinzi kuhakikisha hakuna anayeweza kufika langoni mwetu, hivyo matumaini yangu mechi ya kesho itakuwa na matokeo mazuri kwetu,” alisema Pluijm raia wa Uholanzi.

Mchezo wa Yanga na Medeama utachezeshwa na waamuzi kutoka Misri ambao ni Ibrahim Nour El Din atakayekuwa mwamuzi wa kati akisaidiwa na Ayman Degaish na Samir Gamal Saad, wakati mwamuzi wa akiba akiwa ni Mohamed Maarouf Eid Mansour.

Aidha, Kamishna wa mchezo huo atakuwa Pasipononga Liwewe kutoka Zambia na maofisa wasimamizi ni Mfubusa Bernard ambaye atasimamia utendaji wa waamuzi wakati Mratibu Mkuu wa mchezo huo kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) atakuwa Ian Peter Keith Mc Leod.

Hadi sasa Yanga iliyopo Kundi A  inaburuza mkia  ikiwa haina pointi huku Medeama ikiwa nafasi ya tatu wakiwa na pointi moja, namba mbili ikienda kwa Mo Bejaia wenye pointi nne wakati TP Mazembe  inayoongoza kileleni ikiwa na pointi sita.

Kama Yanga watashinda mchezo wa leo watakuwa na pointi tatu na kukamata nafasi ya tatu nyuma ya TP Mazembe na Mo Bejaia ambazo nazo zitakutana kesho ambapo hata Wanajangwani hao wakishinda hawawezi kukuta pointi za wawili hao.

Mo Bejaia ambao wapo nafasi ya pili wanazo pointi nne hivyo hata Yanga wakishinda watakuwa na pointi tatu, huku TP Mazembe ambao wapo kileleni wakiwa na pointi sita wakijizatiti kuhakikisha hawapotezi ili kuendelea kukalia usukani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles