|Kulwa Mzee, Dar es Salaam
Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Wilbard Mashauri anayesikiliza kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe amegoma kujitoa.
Hakimu Mashauri ametoa uamuzi huo leo Jumanne Julai 10, baada ya kuombwa na washtakiwa hao kujitoa wakidai hawana imani naye.
“Ilitolewa sababu kwamba kwa mwonekano wa hakimu hawezi kutenda haki, niko katika benchi hili kwa miaka 22 sasa sijawahi kuombwa kujitoa kwa sababu za ajabu ajabu kama hizi, sababu hiyo sikuitilia maanani.
“Nimepitia sababu zote za kutaka nijitoe lakini maombi hayo hayana mashiko ya kutosha kunikataa,” amesema Hakimu Mashauri.
Aidha, Hakimu Mashauri amesema aliziona sababu zote zaidi ya 10 hazina msingi ikiwamo kwamba anapendelea upande wa Jamhuri na kwamba ana nia ovu ya kutaka kuzika haki.
Washtakiwa katika kesi hiyo wanatuhumiwa kufanya mkusanyiko usio halali, kufanya uchochezi wakiwa katika mkutano wa kampeni za Jimbo la Kinondoni, Viwanja vya Buibui Februari mwaka huu.