ROME, ITALIAÂ
Habari njema kutoka Italia zinaarifu kuwa nchi hiyo kwa mara ya kwanza imerekodi idadi kubwa ya watu waliopona virusi vya corona katika kipindi cha masaa ishirini na nne.
Kulingana na mkuu wa idara ya kukabiliana na majanga, Angelo Borelli, watu 2,563 wamethibitishwa kupona virusi vya corona katika kipindi cha siku moja.
Idadi ya walioambukizwa virusi hivyo pia imepungua kwa kiasi kikubwa.
Kati ya Alhamis na Ijumaa ni visa 3,786 vya maambukizi vilivyoripotiwa.
Kulingana na Taasisi ya Kitaifa ya Afya mjini Roma, karibu wahudumu wa afya 17,000 wameambukizwa virusi hivyo sasa huku idadi kubwa wakiambukizwa wanapokuwa kazini.
Huko Marekani, ikiwa inaongoza kwa visa vya maambukizi na vifo kote duniani kwa sasa gavana wa mji wa New York ambako ndio kitovu cha virusi hivyo Marekani, Andrew Cuomo, ameendelea kushambuliana na Rais Donald Trump huku akisema kuwa Trump anaelekeza lawama kwa majimbo tofauti sasa na kwamba lengo lake kuu ni biashara kuliko jamii zilizoathirika zaidi.
Kauli hiyo ya kiongozi huyo imekuja baada ya Trump kusema kuwa hivi karibuni, atalegeza vikwazo vilivyoko sasa hivi ili kuunusuru uchumi wa Marekani.
Nchini Uingereza, Profesa mmoja mkuu wa afya ya umma amewaambia wabunge kuwa huenda karibu watu 40,000 wakafariki dunia nchini humo kwa kuwa Uingereza ilichukua muda mrefu kuchukua hatua za kukabiliana na mripuko wa virusi vya corona.
Mashariki ya Kati nako uongozi mkuu wa dini ya Kiislamu Saudi Arabia umesema iwapo mlipuko corona utaendelea basi Waislamu watalazimika kuswalia nyumbani wakati wa mfungo wa Ramadhani na hata sikukuu ya Iddi.
Wakati huo huo Dubai, imeongeza kwa wiki moja marufuku yake ya kutotoka nje kwa siku nzima ili kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.