Mwandishi Wetu-Dar es salaam
ALIYEWAHI kuwa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Benfica ya nchini Ureno, Carraca Antonio Domingoz Pinto amewasili nchini, akiwa mgeni wa klabu ya Yanga.
Kwa mujibu wa taarifa
iliyotolewa na Klabu ya Yanga jana kupitia mtandano wake, Pinto atafanya kazi
ya kushauri mabadiliko ya kiumfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.
Pinto aliwasili nchini jana mchana Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JK Nyerere
na kupokelewa na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela pamoja na
Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambayo ni mdhamini wa klabu hiyo, Mhandisi,
Hersi Said.
Akizungumzia ujio wa Pinto, Mwakalebela alisema wanaamini atawezesha kufanikisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo.
“Ukiangalia wasifu wake utaona kabisa ni mtu wa namna gani, alipita Benfica ambayo imewatoa nyota wengi waliokuja kutamba duniani, pia amekuwa bora katika kuwauza wachezaji wao kama Contrao,”alisema.
Pinto aliwahi kufanya kazi Benfica kati ya mwaka 2008 hadi 2013 kabla ya kuondoka na kwenda kufanya na WSPORTS7.
Katika hatua nyingine,Yanga itashuka dimbani leo kuumana na Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga itaivaa Mtibwa ikiwa na kumbukumbu ya kuichapa Singida United, mabao 3-1Uwanja wa Liti mjini Singida, huku Mtibwa ikitoka kulazimishwa sare ya bao 1-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.