25.9 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Gwajima akamatwa uwanja wa ndege

Josephat Gwajima
Josephat Gwajima

ASIFIWE GEORGE NA ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limemkamata  Askofu wa Kanisa la Ufufuo na  Uzima, Josephat Gwajima, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), baada ya kushuka katika ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) akitokea  nchini Kenya.

Askofu Gwajima, alikamatwa jana asubuhi na makachero wa Jeshi la Polisi waliokuwa wamepiga kambi eneo hilo, baada ya kupata taarifa za kuwasili kwake.

Vyanzo vya habari kutoka kwa watu wa karibu na Askofu Gwajima, viliiambia MTANZANIA kuwa baada ya kiongozi huyo wa kiroho kushuka katika ndege, alitakiwa kupanda helikopta yake ili aelekee Hoteli ya Sea Cliff iliyopo Masaki, Dar es Salaam kwa ajili ya mapumziko.

Kabla ya kuanza safari ya kuelekea Sea Cliff, Askofu Gwajima, alijikuta akiishia mikononi mwa polisi na kupelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa.

Vyanzo hivyo vilidai kuwa baada ya kufikishwa kituoni, alipelekwa kwa Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na baadaye  ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo, Camillus Wambura.

“Askofu Gwajima alikamatwa uwanja wa ndege na polisi akitokea nje ya nchi na kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu na kuhojiwa, lakini ameachiwa kwa dhamana na simu zake za  kiganjani zinashikiliwa kwa ajili ya uchunguzi,” kilisema chanzo hicho.

MTANZANIA ilipomtafuta msemaji wa kiongozi huyo wa kiroho, Yekonia Behagaze, ili kuzungumzia suala hilo, alikiri kiongozi wao kukamatwa.

“Ni kweli Askofu Gwajima amekamatwa na polisi leo (jana) asubuhi akitokea nje ya nchi, alihojiwa kwa saa nne,” alisema.

Alisema baada ya kumaliza mahojiano hayo, aliachiwa kwa dhamana ili aendelee  na majukumu yake.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Sirro, alipoulizwa na MTANZANIA, alithibitisha kukamatwa kwa Askofu Gwajima.

“Ameletwa, amehojiwa, amepewa dhamana na uchunguzi unaendelea,” alisema.

Jeshi la Polisi lilianza kumtafuta Askofu Gwajima tangu Juni 16, mwaka huu, baada ya askari kuzingira nyumba yake iliyopo eneo la Salasala.

Sababu kubwa ya kutafutwa Askofu Gwajima ni kwa ajili ya kuhojiwa juu ya mahubiri yake aliyoyatoa kanisani kwake Ubungo Maji, Juni 11, mwaka huu.

Katika mahubiri hayo ambayo yalisambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, Askofu Gwajima alisikika akikosoa utendaji kazi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Pia alisikika akimshauri Rais Dk. John Magufuli, kuhama Chama Cha Mapinduzi (CCM) iwapo watakataa kumkabidhi uenyekiti wa chama hicho.

Alidai kama ikishindikana, basi Magufuli apeleke muswada bungeni kuondoa kinga ya rais ili  Kikwete ashtakiwe kwa makosa aliyoyafanya akiwa madarakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles