Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MJANE wa aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini, Graca Machel yuko nchini katika ziara fupi kusaidia kumaliza tatizo la ndoa za utotoni kupitia programu na miradi mbalimbali atakayoifadhili ili kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu hatimaye kujikomboa na umaskini.
Katika ziara yake mama Machel, amekutana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, ambapo alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa jitihada kubwa inayofanya wizara hiyo kupambana na tatizo hilo la mimba za utotoni.
“Mkoa wa Mara ndio utakaokuwa wa kwanza kuanzishwa kwa programu hii kwani bado mkoa huo una mila kandamizi ikiwemo mfumo dume,” alisema Machel.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, alisema tatizo la ndoa za utotoni lipo lakini Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi za kiraia na vyombo vya habari, wanapambana kikamilifu kukabiliana na tatizo hilo.
Waziri Simba alitumia fursa hiyo kumshukuru Graca kwa jitihada anazozifanya kuwawezesha watoto wa kike kuondokana na umaskini.