Na CHRISTOPHER MSEKENA,
NYOTA wa muziki wa Injili nchini, Goodluck Gozbert amesema aliwahi kupewa kichapo na mzazi wake mara baada ya kudanganya, badala ya kwenda shuleni yeye alikwenda kwenye tamasha la kampuni moja ya vinywaji baridi ili kuonyesha kipaji chake cha uimbaji.
Akizungumza na Juma3tata, Goodluck Gozbert alisema, baada ya kunyoosha mkono juu na kuchaguliwa kupanda jukwaani kwenda kuonyesha kipaji chake, alifanikiwa kuwa mshindi kati ya watoto kumi waliokuwa wanashindana na kutakiwa kupewa zawadi ya fulana na kreti moja la soda.
“Basi ile nashuka tu jukwaani kumbe mzazi alikuwa anatoka kwenye mizunguko yake wakati anapita akaniona, akasogea mpaka chini ya jukwaa, yaani ile nashuka tu, akanidaka na kofi, hapo nina T-shirt ya ushindi.
“Nashuka chini ili nikapewe na kreti langu la soda, lile kofi tu lilifanya nisahau kila kitu tukaanza kukimbizana humo uwanjani mpaka akanikamata,” anasema Goodluck.
Aliongeza kuwa baada ya kukamatwa alipelekwa msobemsobe mpaka nyumbani na kucharazwa fimbo za kutosha, kesi hiyo haikuishia hapo, mzazi wake alimpeleka mpaka shuleni ambapo iligundulika alikuwa hafiki shuleni mara kwa mara, akaongezewa fimbo na walimu wake zilizofanya aache utoro.
“Nikawa mwema pasipo kutoroka tena,
muziki ulinipa soda ambazo sikuzipata ila ilikuwa mi motisha iliyonipa imani na kipaji changu mpaka leo hii,” alisema mwimbaji huyo anayefanya vizuri kupitia wimbo alioshirikishwa na mwimbaji toka Kongo, Neema Mudosa uitwao Washangaze.