Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Wahitimu wa kozi ya usimamizi wa viwanja na uandishi wa habari za michezo, wametaja changamoto inayosababisha miundombinu mibovu viwanjani kuwa gharama kubwa ya vifaa.
Wameyasema hayo kupitia risala yao waliyosoma mbele ya mgeni rasmi wakati wa kufunga mafunzo ya usimamizi wa viwanja na uandishi wa habari za michezo yaliyoandaliwa na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya leo Desemba 1, 2023 kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Wameeleza kuwa ustawi wa michezo unahitaji miundombinu bora ya viwanja lakini bado kuna changamoto nyingi ikiwamo gharama za vifaa na kukosa viwanja kuanzia ngazi ya kata.
Mmoja wa wanafunzi hao, Kocha Haji Fuko amesema wamepata vitu vingi katima mafunzo hayo kwani walikuwa wanafanya kazi huku baadhi ya mambo hawayafahamu.
Kwa upande wake Ofisa Michezo wa Baraza la Michezo la Taifa(BMT), Nicolaus Mihayo ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi, amekiri uwepo wa changamoto hizo lakini amewataka wahitimu hao wakawe chachu ya mabadiliko na wakatumie kile walichosomea kuendeleza michezo na kuhakikisha wanatunza miundombinu na kutoa taarifa zilizo sahihi.
“Tunapozungumzia miundombinu ya michezo nyie ndiyo mnatakiwa kwenda kufanya hiyo kazi ya kuibadilisha jamii na kujali viwanja vya michezo,” amesema Mihayo.