Na ANDREW MSECHU
NIKIWA Dar es Saalaam, jiji linaloongoza kwa wingi wa magari nchini,
nashawishika kufanya utafiti wa tabia za watumiaji wa barabara na
namna wanavyotii sheria na kanuni za usalama barabarani.
Katika maeneo mengi, madereva na watumiaji wa magari wanaonekana kujua
vyema alama za barabarani na baadhi ya hatua wanazotakiwa kuchukua
kujikinga na athari zitokanazo na ajali pale zitokeapo.
Ajali haipigi hodi. Pamoja na juhudi zote zinazochukuliwa ili kuzuia
ajali, bado zinatokea na kusababisha majeruhi na vifo.
Zipo sababu mbalimbali zinatajwa kama vyanzo vikuu vya ajali, zikiwemo
tabia za watumiaji barabara, kama vile mwendokasi, ulevi, ubovu wa
magari na ubovu wa miundombinu ya barabara.
Lakini kuna tabia zinazohatarisha usalama wa mtumiaji wa chombo cha
moto na pengine kumsababishia kifo pindi ajali itokeapo kama vile
kutokufunga mkanda wa usalama, kutokuvaa kofia ngumu kwa wapanda
pikipiki na kutokutumia vizuizi vya watoto.
Miongoni wa tahadhari muhimu katika kujikinga na madhara yatokanayo na ajali, ni matumizi ya mikanda ya abiria kwenye magari, ambayo husaidia kupunguza madhara ya majeraha hata vifo wakati ajali inapotokea, hatua ambayo watumiaji wengi wanaizingatia.
Lakini kwa Tanzania, lipo kundi lililosahaulika, kundi la watoto wa umri mdogo chini ya miaka 12 ambalo mikanda ya usalama haiwezi kuwasaidia
kutokana na maumbo yao kuwa madogo.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Dunian (WHO) matumizi ya vizuizi maalumu vya watoto (child restraints) ni njia pekee inayoweza kuwaokoa watoto dhidi ya madhara yatokanayo na ajali.
WHO inaeleza kuwa nchi nyingi duniani, bado hazina sheria maalumu ya
kulazimisha matumizi ya vizuizi hivyo ambavyo vimekuwa muhimu katika kuokoa maisha ya watoto, pindi watumiapo huduma za usafiri wa magari.
Katika mwongozo wa usalama barabarani: Matumizi ya mikanda na vizuizi vya watoto uliotolewa na WHO, watoto wanapaswa kutumia vizuizi ambavyo vinafaa kwa saizi yao. Matumizi ya aina sahihi ya kizuizi kwa umri wa mtoto, urefu, uzito na mapungufu ya mwili hupunguza vifo vya watoto kwa kati ya asilimia 50 na 75 pale inapotokea ajali.
Pia, kwa mujibu wa taarifa ya WHO kuhusu hali ya usalama barabarani ya mwaka 2015 inaeleza kuwa ni nchi 53 pekee duniani zina sheria ya matumizi ya vizuizi vya watoto ambapo Tanzania haipo kwenye nchi hizo na kubainisha ni wazazi wachache wenye uelewa wa matumizi ya vizuizi kama njia sahihi ya kumlinda mtoto awapo kwenye gari.
WHO inaeleza kuwa watoto wachanga hadi wenye miaka 11 wanapaswa
kutengewa kiti maalum kinachoweza kumtosha kulingana na uzito na umbo lake akiwa kwenye gari.
Taarifa hiyo ya WHO kuhusu umuhimu wa matumizi ya vizuizi vya watoto,
inaeleza kuwa watoto kama watumiaji wa vyombo vya moto ni waathirika
wakuu wa ajali za barabarani, kwani hupata majeraha makubwa na hata
kupoteza maisha.
Kiwango cha madhara kinatofautiana katika nchi zilizoendelea, zenye
kipato cha kati na zenye kipato cha chini kutokana na namna watumiaji
wa magari wanavyoongezeka.
Kwa hivyo ni muhimu kwamba matumizi ya vizuizi vya ajali, ikiwemo
vizuizi vya watoto kuzingatiwa katika nchi hizi ili kupunguza madhara
yatokanayo na ajali ikiwamo majeraha na vifo miongoni mwa watumiaji wa magari.
“Watoto wanapaswa kutumia vizuizi ambavyo vinafaa kwa saizi yao.
Matumizi ya aina sahihi ya kizuizi kwa umri wa mtoto, urefu, uzito na
ukubwa wa mwili hupunguza vifo vya watoto kwa kati ya asilimia 50 na
asilimia 75,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ya WHO.
Sehemu ya taarifa hiyo inafafanua kuwa kumekuwa na programu ambazo
zinaweka na kutekeleza sheria za lazima za kuwa na mikanda ya abiria
kwenye siti za magari, pamoja na kampeni za elimu ya umma,
zinafanikiwa kuongeza viwango vya matumizi ya vizuizi hivyo, kwa hiyo
kusaidia kupunguza majeraha na vifo.
Sheria za kuhakikisha kunakuwa na mikanda kwa ajili ya abiria kwenye
magari ambazo zinatekelezwa kupitia utekelezaji wa msingi zinafaa
zaidi katika kuongeza viwango vya matumizi. Tayari mataifa mengi
yameingia katika mkakati wa kimataifa wa kuweka sheria za matumizi ya
vizuizi vya ajali…. Ulipaswa kuelezea vizuizi vya watoto na sio
mikanda.
Gharama
Kwa Tanzania, gharama za viti maalumu vya watoto ambavyo huuzwa
kutokana na ukubwa na ubora zinatofautiana katika maeneo tofauti.
Saidi Chuma, muuzaji wa siti za watoto katika eneo la Madonna jijini
Dar es Saalaam, anasema huuza viti hivyo vya mtumba kwa kati ya Sh
150,000 hadi Sh 200,000 kwa siti moja, lakini gharama inakuwa ya juu
zaidi kwa viti vipya, ambavyo hauzia Sh 200,000 na kuendelea.
“Siti hizi, kwa kuwa haziji na magari, watumiaji wa magari hulazimika
kuja kuzinunua kwa ajili ya ulinzi wa watoto wao. Zinatofautiana
kutokana na ukubwa, yaani umri wa watoto. Wanunuzi bado ni wachache,
inaonekana kwa kuwa watu wengi hawana magari.
“Siti hizi huchukua muda mrefu kununuliwa, inaweza kukaa hata miezi
mitano au sita. Wapo wanaonunua, ndiyo maana tunaendelea na biashara
hii, lakini bado hakuna muammko sana, labda hata hao wenye magari
wengi hawana watoto au hawaoni haja ya kununua,” anasema Chuma.
Vizuizi hivyo vya watoto hupatikana katika maduka kadhaa
yanayojihusisha na uuzaji wa vifaa vya magari, nguo na vifaa vya
watoto ambapo katika eneo la Siza madukani, huuzwa kati ya Sh 150,000
hadi Sh 450,000 kutegemea na ubora na ukubwa.
Jinathan Jackob, mkazi wa Sinza anasema ni baba wa familia ya watoto
wanne, mtoto wake wa mwisho akiw ana miaka mitatu kwa sasa. Anaona
umuhimu wa kununua vizuizi hivyo, lakini hajawahi kufanya hivyo,
japokuwa amekuwa akitumia gari kwa miaka 15 sasa.
Anasema suala la gharama kubwa ya vizuizi limekuwa likimkatisha tamaa
kwa sababu kutokana na hali ya uchumi, manunuzi ya vizuizi hivyo
ambayo ni ya gharama kubwa na kwamba ukifuata utaratibu unatakiwa
kununua hadi vitatu kwa hatua za mtoto kuanzia miaka 0 hadi miaka
minane.
“Sasa kwa hali ilivyo, ni kwamba matumizi ya kila kizuizi ni miaka
miwili hadi mitatu. Baada ya hapo hakina matumizi tena. Ndiyo maana
sijaona kama kuna ulazima wa kufanya hivyo,” anasema.
Anasema anatambua kwamba japokuw abado hakuna sheria ya moja kwa moja inayohimiza matumizi ya vifaa hivyo, huenda uwepo wa sheria rasmi
ukasaidia kuwahimiza watu kununua na kuwa na vizuizi hivyo kwa ajili
ya kuwakinga watoto wakati inapotokea ajali.
Madhara yatokanayo na kutokutumia vizuizi hivyo
Kuna madhara makubwa yatokanayo na kutokuzingatia matumizi ya vizuizi
vya watoto. Madhara hayo ni pamoja na magonjwa ya akili, ulemavu hata
kifo. Na kwa kuwa watoto wadogo hawawezi kujisimamia wenyewe,
wanahitaji msaada wa mzazi au mlezi kuhakikisha wakati wote wanakuwa
salama.
Kwa kuwa wakati wote awapo safarini, mtu mzima anatakiwa kufunga
mkanda, umuhimu huo wa kuwa na kizuizi ni zaidi kwa mtoto ambaye
hawezi kuhimili mitikisiko au jambo lolote baya linaloweza kutokea
kwenye gari.
Wakati watu wazima wakifunga mikanda, watoto wadogo wanatakiwa kutumia vifaa maalum ambavyo hujulikana zaidi kama vizuizi vya watoto hasa katika magari binafsi.
Vizuizi vya watoto ni viti maalum vyenye mikanda mahususi kumlinda
mtoto ambapo vimetengenezwa kulingana na uzito, urefu na umri wa
mtoto.
Licha ya umuhimu wa kuwa na viti maalum vya watoto kwenye magari,
Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973 haijaweka wazi kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa kumlinda mtoto dhidi ya hatari yoyote
inayoweza kutokea kwenye gari.
“Mimi mwaka jana (2017) nilipata ajali na ‘Airbag’ (Mfuko maalum wa
kumkinga mtu asiumie kwenye ajali) haukufanya kazi niliumia sana, sasa
fikiria kama mtoto umempakata kiti cha mbele alafu akapata ajali!
Wazazi ni wakati wa kutumia viti hivyo na kuhakikisha hawakai siti za
mbele,” anasema Neema Komba mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam.
Ili kuhakikisha zaidi usalama wa mtoto, viti hivyo maalum vinapaswa
kufungwa kwenye siti za nyuma na wadau wa usalama barabarani
hawashauri mtoto kukaa siti za mbele ili kuepuka kuchomoka kwa mtoto
pindi ajali inapotokea au gari linaposimama ghafla.
Mabadailiko ya sheria
Wadau mbalimbali wanaishauri Serikali kuongeza mkazo wa kuwalinda
watoto pamoja na kuifanyia mabadiliko sheria ya Usalama Barabarani ili
wazazi wawajibike kuwanunulia watoto wao viti maalum.
“Mzazi asisubiri hadi sheria imbane anunue kizuizi cha mtoto kwenye
gari, wanaopata madhara ni watoto wao wenyewe,” anasema Mkurugenzi
Mtendaji wa shirika la Tanzania Child Rights Forum (TCRF), Jones John.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mabalozi wa Usalama barabarani
Tanzania (Road Safety Ambassadors RSA), John Seka anasema kuwa
wanaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi ya vizuizi vya
watoto na mabadiliko ya sheria.
“Tunategemea kabla ya mwaka 2019 haujaisha basi muswada wa marekebisho ya Sheria ya Usalama Barabarani ya mwaka 1973, ufikishwe bungeni na vizuizi vya watoto kuwa lazima katika magari binafsi ili kuweza kumlinda mtoto kwani ni haki yake kulindwa na madhara yoyote,” anasema John.
Historia
Tangu gari ya kwanza ilipitengenezwa mwanzoni mwa miaka ya 1900,
marekebisho kadhaa yamekuwa yakifanyika kwa ajili ya kuimarisha
usalama wa abiria kwenye magari.
Awali, vifaa vingi vya kinga vilikuwa vikijali zaidi kuangalia usalama
wa watu wazima bila kujali usalama watoto, lakini kuanzia miaka ya
1930, vilianza kutengenezwa viti maalumu kw aajili ya kuwakinga watoto
wakati wa ajali.
Ilipofika mwaka 1962, mbunifu wa Uingereza, Jean Ames alibuni siti
yenye mikanda kwa ajili ya kuwalinda watoto.
Kwa sasa, aina ya vizuizi vya watoto kwenye magari vinahusisha viti
maalumu vinavyounganishwa kwenye virti vya magari, kwa ajili ya
kuwakinga watoto mara inapotokea ajali, vikiwa na uwezo wa kubeba
watoto kwaukubwa na uzito tofauti.
Baadhi ya viti (lakini sio vyote) vinaweza kutumiwa kwa kutumia
vishikizo maalumu, au kwa kufungwa peke yake. Viti vingine havina
vishikizo maalumu. Vibebezi hivi vya watoto wachanga huwekwa kwenye
viti vya nyuma vya magari binafsi ambapo husaidia kupunguza madhara
inapotokea mtikisiko wa ajali.
Viti vyenye upande wa nyuma vinaonekana kuwa salama zaidi, na kwa
watoto wenye umri wa mwaka mmoja hadi miwili, inashauriwa kuwaweka nyuma watakapokuwa wameongezeka urefu wa kiti cha gari kinachozingatia matumizi ya mikanda ya kawaida.