Na Mwandishi Wetu, Geita
WIKI iliyopita Mgodi wa Dhababu wa Geita (GGM), uliandika histori mpya ya kusaidia vijana 131 kuhitimu mafunzo ya Polisi Jamii katika Kijiji cha Nyakabale-Manga mkoani Geita.
Lengo la mafunzo hayo, ni kutoa ajira na kukabiliana na wimbi la uhalifu ambalo limekuwa likitishia usalama wa mgodi na majirani wanaozunguka eneo hilo.
Mafunzo hayo ambayo yaliendeshwa kwa miezi mitatu, yalikuwa ya aina yake kutokana na wahitimu kushirikishwa katika masomo muhimu kutoka kwenye taasisi za Serikali.
Miongoni mwa taasisi hizo ambazo zilisaidia kutoa elimu zaidi katika mafunzo hayo ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, Naibu wa Polisi anayeshughulikia Kitengo cha Polisi Jamii, Ahmada Abdallah alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kutokana na kuwapo mahitaji makubwa ya ulinzi katika mkoa huo.
“Natambua mmepata mafunzo ya vitendo,silaha na maadili kutoka kwenye taasisi zetu nilizotaja hapo juu… huu ni mfumo mpya wa kuwajengea uelewa wa sheria za nchi kwa sababu mnakwenda kufanya kazi kwenye jamii inayowazunguka.
“Lazima mtambue mkoa huu una watu mchanganyiko kutoka nchi za jirani, kwa hiyo katika somo la Uhamiaji mmefundishwa namna ya kutambua wageni, pia suala kupokea rushwa naamini Takukuru imewanoa vizuri…ndugu zetu wa JWTZ wamewapa mafunzo mazuri ya ukakamavu,tusaidie kulinda nchi yetu,”alisema.
Alisema siku zote maeneo ambayo yana uwekezaji mkubwa kama wa mgodi wa GGM, kunahitaji ulinzi wa kutosha ili kuimarisha maendeleo.
“Hakuna maendeleo sehemu yoyote duniani bila amani na utulivu,tunategemea mtakuwa mabalozi wa jambo hili,”alisema Abdallah.
Alisema kutokana na kazi nzuri inayofanywa na mgodi huo, kwa kujenga miradi ya maendeleo katika sekta za afya,elimu na mingine, itakuwa salama zaidi kama wahitimu hao watajitoa kweli kweli kuisimamia.
“Haiwezekani mjengewe miradi ya mamilioni ya fedha alafu ihujumiwe na watu wachache.Tena kibaya eneo hili linaongoza kwa wizi wa mifugo,dawa za kulevya aina ya bangi,nawaahidi sisi polisi tutashirikiana nanyi kwa nguvu zote,”alisema.
Alisema kama kila mhitimu anapaswa kuwa mzalendo kwa kulinda wenzake,kuheshimu sheria bila shuruti litakuwa jambo la busara.
“Nawaomba mno mkaishi maisha ya uhusiano na GGM kwa sababu wameonesha kuwajali kwa kugharamia mafunzo haya ambayo yamedumu kwa miezi minne,”alisema.
Aliwaasa wahitimu hao kutumia uwezo wao wote wa kukomesha mauaji ya watu ambayo yameshamiri katika mkoa huo.
“Hili ni tishio kubwa kwa Mkoa wa Geita kuna mauaji ya kukata watu mapanga.Jambo hili linawaongeza hofu kubwa wawekezaji,lisaidieni jeshi la polisi kuzuia hali hii,”alisema Kamishina Abdallah.
RPC Mponjori
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjori Mwabulambo anasema mafunzo hayo yatakuwa hazina kubwa katika suala la ulinzi kutokana na mkoa huo kuwa na matukio mengi ya uhalifu.
“Mafunzo haya yalijikita zaidi kuwajengea uwezo wahitimu 131 kwa kushirikisha taasisi nyeti za serikali,yatakuwa na msaada mkubwa wa kusaidia polisi kukabiliana na uhalifu.
“Tuliamua kuingizia baadhi ya masomo yetu kwa wahitumu kwa makusudi ili wajue namna ya kufanya kazi zao kwa weledi zaidi. Napenda kuwaambia ukweli kwamba kuanzia sasa naweza kulala bila hofu tofauti na maeneo niliyotoka,”alisema.
Anasema ushirikiano kati ya GGM, Polisi Jamii na polisi utajenga misingi imara ambayo itakuwa kivutio kwa wawekezaji.
Anasema mafanikio yote hayo yametokana na menejimenti nzuri ya GGM ambayo imedhamiria kuona kumaliza kero imekuwa chachu ya maendeleo hivi sasa.
“Najivunia menejimenti nzuri ya GGM ambayo kila kukicha tunashirikiana kwa kila jambo ili kuona tunasonga mbele,mafunzo haya hayakuja kwa bahati mbaya,”alisema.
Mkurugenzi GGM
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mkuu wa GGM, Terry Mulpeter anasema lengo la mafunzo hayo ni kutaka kuona jamii inayozunguka eneo la mgodi inaiishi kwa amani na utulivu.
“Tunataka kuona vijana kama hawa wanapata ajira kutokana na mafunzo haya,tumegharamia kila kitu ili mwisho wa siku wanaweza kuajiriwa popote.
“Naishukuru Serikali ambayo tumeshirikiana nayo kwa kutoa wataalamu wake kuwafundisha hawa vijana ambao wanaonekana kuiva vizuri kimafunzo,nategemea kuona mabadiliko makubwa siku zijazo.
“Nimevutiwa na maonesho yaliyooneshwa na wahitimu hawa namna ya kukabiliana na adui na ule wimbo wao ambao unaonesha kweli tumefika mahala pazuri. Nawahakikishia tutaendelea kuwaunga mkono,”alisema Mulpeter.
Kijiji
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Manga,Elias Lukanga alisema mafunzo yatakuwa mkombozi mkubwa kwao kutokana na kushamiri wimbi la ujambazi katika eneo hilo.
“Tumepata mkombozi wa usalama, vijana wetu hawa wakitumia uwezo wao waliopata kwenye mafunzo haya, wimbi la ujambazi litapungua,”alisema Lukanya.