30.8 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

GGM YAKATAA KUGHARAMIA MAZIKO YA KIJANA ALIYEUAWA MGODINI

Na HARRIETH MANDARI-GEITA

SERIKALI imegharamia taratibu zote za maziko ya Shinje Charles (24) aliyefariki dunia akiwa ndani ya Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM), baada ya mgodi huo kukataa kugharamia.

Pia imetoa siku saba kwa Jeshi la Polisi  kuhakikisha uchunguzi na upelelezi wa tukio hilo unafanyika na kukamilika.

Serikali imefikia uamuzi huo baada ya kuibuka mvutano baina ya GGM, ndugu wa marehemu na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Geita, kutokana na ripoti ya daktari kueleza kuwa marehemu alikutwa na majeraha kichwani yaliyotokana na kupigwa kwa kitu chenye ncha kali huku  GGM wakisema alianguka katika moja ya mashimo ya mgodi huo.

Kifo cha Shinje kilitokea Agosti 21, mwaka huu saa 10 usiku akiwa na vijana wenzake watatu walioingia katika eneo la GGM upande wa Nyankanga kwa lengo la kuchukua mawe ya dhahabu na kukimbizwa na walinzi na yeye kukamatwa akiwa hai na ndugu wa marehehmu waligoma kuzika mwili huo hadi ripoti ya uchunguzi itakapotolewa.

Akizungumza juzi baada ya kamati hiyo kukutana na GGM, ndugu wa marehenu  kujadili hatima ya sakata hilo na kuzuru eneo linalodaiwa kijana huyo alianguka kwenye shimo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga, alisema kwa kuwa maiti ilikaa muda mrefu Serikali imekubaliana na ndugu kuzika mwili huo na kutoa siku saba kwa jeshi hilo kufanya uchunguzi na kutoa ripoti kamili.

“Kwa kuwa GGM imekataa kutoa huduma za mazishi, Serikali ya mkoa tutahakikisha tunagharamia taratibu zote za maziko wakati huo tukiwa tunasubiri uchuguzi zaidi utakaofanywa na polisi na baada ya siku saba tutapata mwafaka,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Geita, Joseph Kasheku (Msukuma), alisema kamati ya ulinzi na usalama iliitaka GGM kugharamia mazishi lakini walikataa hivyo kufanya hadi kikao hicho kinamalizika kutopatikana kwa suluhu.

“Hadi sasa GGM wametelekeza maiti hiyo nakuendeleza hali ya sintofahamu miongoni mwetu kwa sababu kwa mujibu wa ripoti ya daktari kijana huyo alikutwa na majeraha kichwani yaliyotokana na kupigwa kwa kitu chenye ncha kali na GGM wanasema marehemu alianguka katika moja ya mashimo ya mgodi wao, hapo ndipo unapoona jinsi gani maelezo yanakinzana,” alisema.

Kaka wa marehemu, James Charles,  alisema amekubaliana na ushauri wa Serikali wa kutaka kuzika kwanza mwili wa marehemu na akaomba uchunguzi kufanyika zaidi.

Siku ya tukio vijana watatu akiwamo Shinje, waliingia katika eneo la mgodi la Nyankanga, ambalo inaelezwa kuwa haliendeshi shughuli za uchimbaji kwa sasa  kwa ajili ya kutafuta dhahabu na walikimbizwa na walinzi wa mgodi na kufanikiwa kumkamata huku wengine wawili walifanikiwa kukimbia na kujificha.

Utata kuhusu kifo hicho ulikuja baada ya waliokimbia kukamatwa na walinzi kisha wakatoa taarifa kuwa mwenzao Shinje alikuwa hai wakati akikamatwa na mmoja wa vijana hao, Shija Masemu, alisema baada ya walinzi hao kuanza kuwakimbiza, walifanikiwa kumkamata mwenzao na wao kufanikiwa kukimbia na kujificha kwenye moja ya mashimo ya mgodi huo na walifanikiwa kutoka Agosti 23, mwaka huu.

“Ilikuwa Agosti 21, mwaka huu ambapo mimi pamoja na wenzangu tulienda kutafuta mawe ya dhahabu katika moja ya mashimo hayo ambayo kwa muda mrefu hakuna shughuli za uchimbaji zinafanyika, tuliwaona askari hao jumla wakiwa nane walifanikiwa kumkamata marehemu Shinje  na kumwingiza kwenye gari akiwa hai na kuendelea kutukimbiza, sasa tunashangaa kusikia eti amekutwa amekufa kwenye mashimo,” alisema Masemu aliyekuwa na kijana mwingine, Philipo Enock.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles