24.9 C
Dar es Salaam
Sunday, April 21, 2024

Contact us: [email protected]

GESI YENYE SUMU YAZIDI KUONGEZEKA DUNIANI

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM


KIWANGO cha gesi ya Carbon inayotolewa duniani kinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia mbili mwaka huu hiyo ikiwa ni rekodi mpya, ripoti imeonya.

Kiwango hicho cha kutisha kilitangazwa na wanasayansi wakati wa mkutano wa kimataifa wa mazingira uliofanyika hivi karibuni mjini Bonn, Ujerumani.

Ilitarajiwa kwamba kutokana na kampeni zinazopigwa, ripoti ingeonesha kupungua kwa kiwango cha hewa yenye sumu, lakini kinyume na matarajio kimeongezeka.

Awali kiwango cha gesi ya Carbon kilikuwa hakijabadilika tangu mwaka 2014 hadi mwaka jana, lakini mwaka huu kimeongezeka, ikiashiria uwapo wa kazi kubwa zaidi kuikabili.

Ripoti inaonya kuwa iwapo kiwango hicho cha gesi chafu ya Carbon kitazidi kuongezeka kufikia mwaka 2020 au kubakia katika viwango vya sasa, basi malengo yaliyowekwa katika makubaliano ya Paris hayataweza kufikiwa.

Jopo la wataalamu wa mazingira lilitoa mwongozo wa ni kasi gani na kiwango gani cha gesi ya Carbon kinahitaji kupunguzwa ili kufikia malengo ya makubaliano ya Paris, pia lilieleza njia tofauti zitakazosaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Zaidi ya wanasayansi 15,000 wanaonya kuwa kuongezeka kwa gesi ya carbon, ukuaji mkubwa wa idadi ya watu duniani na mfumo wa maisha unaotumia kiasi kikubwa cha mali asili kunaathiri kwa kiasi kikubwa dunia na kuharibu raslimali zake.

Wanasayansi hao wakiongozwa na Corine Le Quere aliyeongoza utafiti huo, wameendelea kuonya kuwa watu wanavuruga maisha yao ya baadaye.

Ni mwenendo unaotia wasiwasi kuwa walimwengu wanaendelea kusababisha majanga makubwa yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi, mkondo unaosemekana kuwa mbaya zaidi kutishia kuangamia kwa viumbe hai katika kipindi cha miaka milioni 540.

Kundi jingine la wanasayansi nalo limetahadharisha kuwa viwango vya joto, ambavyo vimefikia nyuzi 1.1 vitasababisha barafu kuyeyuka katika ncha ya Antaktiki na hivyo kuongeza kina cha maji ya bahari hadi mita sita au saba zaidi na huenda ikachukua miaka mingine 1,000 kurekebisha mambo, iwapo hatua za dharura hazitachukuliwa sasa hivi kuyaokoa mazingira.

Kukabiliana na hali hiyo, mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na mageuzi makubwa ya teknolojia mpya katika sekta ya viwanda.

Mageuzi hayo yanaaminika yatachangia kwa kiasi kikubwa kusukuma mbele mchakato wa kuyalinda mazingira.

Hata hivyo, hilo linaweza tu kufikiwa iwapo sekta ya biashara na serikali zitaunga mkono mageuzi hayo kupitia sera madhubuti na mikakati kabambe.

Asasi za kiraia pia zimetaka sekta binafsi kushirikishwa zaidi katika kampeni ya dunia ya kuyaokoa mazingira kwa kupunguza viwango vya joto kupitia kupunguza utegemezi wa nishati kama vile mafuta na makaa ya mawe.

Sekta hiyo ya binafsi imetakiwa kuwekeza zaidi, kuimarisha matumizi ya teknolojia mpya na kuwa mstari wa mbele katika azma ya kupatikana suluhisho.

Ukiachana na hilo, takwimu zilizotolewa na wanasayansi 76 wa kutoka nchi 15 kuhusu ongezeko la joto ni pigo kwa makubaliano ya kuyaokoa mazingira yaliyofikiwa mwaka 2015 mjini Paris, Ufaransa.

Makubaliano hayo yalilenga kupunguza kiwango cha gesi chafu hasa kutoka viwandani inayochafua mazingira na hivyo kusababisha majanga kama vimbunga, mafuriko, ukame na kina cha maji ya baharini kuongezeka.

Ongezeko la viwango vya joto vilivyovunja rekodi pia vimesababisha ukame hasa katika mataifa ya Afrika na kusababisha baa kubwa la njaa, watu kupoteza maisha, mifugo kufa, ardhi kutolimika na watu kulazimika kuyahama makazi yao na kwenda kwingine kutafuta chakula, maji, lishe kwa mifugo na vyanzo vingine vya kujitafutia riziki.

Pia mabadiliko hayo ya tabianchi yamesababisha joto kali katika nchi kama vile India, Pakistan na nchi za Kiarabu huku nchi nyingine kama Marekani, Puerto Rico, za Pacifik na visiwani zikikumbwa na vimbunga vikali na mafuriko makubwa ya mara kwa mara yanayoharibu miundombinu na kusababisha maafa mengine makubwa.

Fiji ambayo ndiyo inashikilia urais wa kuandaa mkutano wa kimataifa wa mazingira imeonya kuwa inakabiliwa na gharama kubwa inayozidi kuongezeka ya kujilinda dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa sababu hiyo, imeutaka ulimwengu kuchukua hatua zaidi kupunguza gesi ya Carbon ili kuweza kuzilinda nchi masikini na visiwani zinazokumbwa na kitisho cha mafuriko zaidi na vimbunga.

Fiji inatumia asilimia 10 ya pato lake jumla la taifa kupambana na majanga.

China ambayo ni nchi ya kwanza duniani katika kuchafua mazingira, imechangia asilimia 3.5 zaidi ya gesi ya Carbon mwaka huu kutokana na uzalishaji zaidi wa nishati ya makaa ya mawe wakati ambao ukuaji wa uchumi wa taifa hilo ukiimarika. Nchi hiyo inachafua mazingira kwa asilimia 30.

Marekani ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikiongoza duniani kabla ya kushuka hadi nafasi ya pili kwa uchafuzi wa mazingira inatarajiwa kushuhudia kupungua kwa asilimia 0.4 tu ya utoaji wa gesi chafu mwaka huu.

Hayo yanakuja huku mameya wa miji 25 ya nchi mbalimbali duniani, wakiwakilisha watu milioni 150 wakiahidi kupunguza viwango vya gesi chafu ya Carbon hadi nyuzi sufuri ifikapo mwaka 2050 huku wakiimarisha juhudi za kuweza kuhimili zaidi athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mameya hao waliahidi kuweka mikakati kabambe ifikapo 2020 ya mpango mpya wa kuchukua hatua za kuyalinda mazingira na wakati huo huo kuwahamasisha wakazi wa miji yao kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua zaidi kuyalinda mazingira ili kunufaika kijamii, kimazingira na kiuchumi.

Waziri wa Mazingira wa Ujerumani Barbara Hendrick amesema wanahitaji ushirikiano wa kila kiongozi kufikia malengo ya kuyaokoa mazingira.

Miji tisa mikubwa ya Afrika ikiwamo Cape Town, Addis Ababa, Lagos na Nairobi itasaidiwa kufikia mipango ya muda mrefu ya kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kuambatana na malengo ya makubaliano ya Paris ya kupunguza viwango vya joto hadi chini ya nyuzi mbili kwa kusaidiwa na serikali ya Ujerumani.

 

Makubaliano ya Paris ni nini?

NI mwendelezo wa makubaliano kama hayo yaliyofanyika Kyoto, Japan kuhusu udhibiti wa athari za mazingira duniani.

Mkataba wa Paris unatokana na uamuzi wa nchi wanachama 195 duniani uliolenga kutekelezwa kwa asilimia zote mwaka 2020.

Maeneo makuu matatu yanayobeba maudhui ya malengo ya makubaliano hayo ni pamoja na kupunguza ongezeko la joto duniani kwa kiwango cha chini ya nyuzi joto mbili kutoka kiwango kilichokuwepo na kufanya juhudi za kuweka ukomo wa ongezeko la joto lisizidi nyuzi joto 1.5.

Aidha kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani katika namna isiyo na athari katika uzalishaji wa chakula duniani. Pia unasisitiza kuwapo kiwango cha kutosha cha fedha kusaidia kudhibiti hewa chafu duniani.

Jambo lingine ni nchi moja moja kutakiwa kuwa na mchango unaofaa kulinda mazingira na suala la maendeleo hayo, yawe yanaripotiwa kwa mamlaka husika kila baada ya miaka mitano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles