Na MWANDISHI WETU,
KUNA usemi usemao ‘Karibu mgeni mwenyeji apone”, huenda ndivyo walivyokuwa wakinena wakazi wa mikoa ya Geita na Shinyanga baada ya kushiriki ipasavyo katika zoezi la usajili wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwaajili ya kupata vyeti vya kuzaliwa.
Baadhi ya wananchi kutoka katika mikoa hiyo, kwa nyakati tofauti walidiriki kusema kuwa wamekuwa wakisubiri huduma muhimu za kijamii kama hizo, lakini hupatikana kwa nadra katika ubora na ukarimu kama ule.
Kwa wale ambao waliwahi kushiriki katika mchakato wa kutafuta hati ya kusafiria (Passport) na wakawa hawana vyeti vya kuzaliwa watakumbuka usumbufu walioupata. Lakini si hivyo tu kuna hata wakati mwingine huduma za kijamii zinakwama kutokana na kutokuwapo kwa takwimu sahihi.
Wataalamu wa masuala ya maendeleo ya jamii wanasema kuwa kutokuwa na cheti cha kuzaliwa kunaweza kukwamisha hupatikanaji wa huduma bora za kijamii.
Wakazi wa mikoa ya Geita na Shinyanga wamekuwa kati ya mikoa mitano nchini, iliyofaidika na mpango maalumu wa kusajili watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa njia ya kidigitali.
Mradi huo ambao hadi sasa umetekelezwa katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mwanza, Songwe na baadaye Geita na Shinyanga unaendeshwa na Mamlaka ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) pamoja na Tigo ambao ndio wabunifu wa mfumo wa kidigitali ili kufanikisha zoezi hilo.
Kwa hali ilivyo na kutokana na takwimu, bila shaka wapo Watanzania wengi ambao watoto wao hawajasajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa. Huenda zikatajwa sababu nyingi juu ya tatizo hilo, lakini pia mfumo wa awali haukuwa rafiki na hasa kwa watu wanaoishi vijijini, ikilinganishwa na sasa.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa watoto milioni 230 wanaozaliwa katika mazingira ambayo hayaonekani ikimaanisha kwamba uzazi wao hausajiliwi. Kila mwaka kuna nyongeza nyingine ya watoto wasiosajiliwa duniani.
Kwa mujibu wa takwimu zilizopo asilimia 80 ya uzazi wa watoto wasiosajiliwa hutokea Afrika, Tanzania ikiwamo. Katika nchi nyingi, watoto ambao familia zao ni maskini au wanaoishi maeneo ya vijijini, kwa kawaida wengi wao imekuwa ni vigumu kupata usajili wa uzazi na kuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Nchini Tanzania mchakato wa usajili wa uzazi ulioanzishwa kupitia Sheria ya Usajili na Vifo vya Mwaka 2002 inawataka wazazi kusajili watoto wao ndani ya siku 90 baada ya kuzaliwa.
Katika hatua ya kwanza ni lazima wapate Tangazo la Uzazi kutoka hospitali au kituo cha afya mtoto alipozaliwa na kama ikitokea alizaliwa akiwa nyumbani, kuwepo taarifa kutoka kwa ofisa mtendaji wa kijiji.
UNICEF inatambua usajili wa uzazi kama haki ya msingi ya kila mtoto kwa madai kwamba, kuwapo usajili wa uzazi unamaanisha mpangilio mzuri wa huduma kama vile elimu ya watoto na nyingine za kijamii.
Wakazi wa mikoa ya Geita na Shinyanga wameelezea jinsi walivyopokea hali hiyo, ambayo wanaitafsiri kama huduma ya pekee kutokea katika maisha yao ya kawaida.
“Kwanza niseme kwamba huduma hii kwetu ni muhimu mno. Mara kwa mara tunasikia serikali ikituhimiza kuhakikisha watoto wana vyeti vya kuzaliwa, siamini kwamba kama kuna aliyechukia uwapo wa RITA na wadau wengine kama Tigo kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa hapa kwetu,” anasema Mama Kayenza mkazi wa Geita.
Burhan Hassan ni mkazi wa Shinyanga, anasema kuwa si kwamba hakuwa na mpango wa kumtafutia cheti cha kuzaliwa mtoto wake ambaye sasa ana miaka mitatu, bali anawashukuru Tigo kwa kurahisisha huduma hiyo na kuifanya kupitia katika simu ya mkononi.
“Kama kila kampuni itakuwa na ubunifu wa namna hii, basi maendeleo yatafika huku vijijini kwetu. Haya tumezoea kuyasikia mjini, lakini kwa hili la kusajili na kupata vyeti vya watoto wetu vya kuzaliwa limenikuna mno,” anasena Hassan, huku akiwataka wananchi wengine wa Mkoa wa Shinyanga kutumia fursa hiyo.
“Mara nyingi tumekuwa wepesi wa kukumbuka shuka kumekucha. Ningependa kuwashauri wana-Shinyanga wenzangu kutumia fursa kama hizi zinapojitokeza na kuachana na imani za ajabu ajabu,” anaelezea.
Kwa upande wake Meneja wa Tigo Kanda ya Ziwa, Ally Maswanya, anasema kuwa kampuni hiyo itaendelea kujiweka karibu na jamii na hasa kusaidia katika jitihada mbambali za serikali kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya kiuchumi.
Tigo ni moja ya wadau wa mawasiliano ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika sekta mbalimbali ikiwamo ya ustawi wa jamii na kuonesha umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya simu za mkononi kama nyenzo muhimu katika kufikia malengo endelevu.
Kwa mujibu wa utafiti wa idadi ya watu Tanzania (DHS) wa mwaka 2010, ni asilimia 16 tu ya watoto walio na umri chini ya miaka mitano walikuwa wamesajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa na mamlaka husika. Na kwa mujibu wa Takwimu za Sensa ya mwaka 2012 ni asilimia 13.4 ya Wananchi ndiyo waliyosajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa.
Kutokana na takwimu hizi, Tigo ikishirikiana na RITA na UNICEF tangu 2012 ilifanikiwa kutengeneza mfumo maalumu kupitia simu ya mkononi unaorahisisha utumaji wa taarifa za usajili wa watoto katika mfumo maalumu ya kuhifadhi kumbukumbu wa Mamlaka wa RITA.