LICHA ya figisu zinazoendelea kwa klabu ya Geita kushushwa Daraja la Pili (SDL), ikihusishwa na kashfa ya upangaji matokeo ya kundi C Ligi Daraja la Kwanza, Mkurugenzi wa Kampuni ya Madini ya Geita Gold Mine (GGM) Ashanti, Terry Mulpeter, ameeleza kuwa wataendelea kuidhamini klabu hiyo mpaka watakapojiridhisha kuwa ilihusika na tukio hilo.
Kauli ya Mkurugenzi huyo imekuja baada ya uongozi wa klabu ya timu ya Geita kukataa kuhusika na jambo lolote linalohusu upangaji matokeo.
Akizungumza na MTANZANIA jana Geita, Mulpeter alisema tayari uongozi wa klabu hiyo ulipeleka barua katika kampuni hiyo kukana kuhusika na upangaji matokeo.
“Tunaweza kukoma udhamini wetu au kujiondoa endapo tu tutagundua timu ilihusika kupanga matokeo hayo.
“Hatutakubali kudhamini klabu yenye tabia ya ajabu, kwa sasa tutaendelea kufadhili lakini tukigundua kuwa kweli walihusika tunajiondoa ufadhili wetu,” alisema.
Mwaka jana kampuni hiyo kama mfadhili iliipa Geita jumla ya Sh milioni 300, ili kuweza kufanya vizuri ligi daraja la kwanza.
“Lengo langu ni kuisaidia timu hii ili kuifanya kuwa klabu kubwa Tanzania, lakini si kuharibu jina la kampuni kwa mambo yasiyofaa,” alisema Mulpeter.