KINSHASA, DRC
NAIBU Gavana wa Jimbo la Ikweta, Kusini Magharibu mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tathy Bikamba anakabiliwa na mashitaka ya kumbaka binti wa miaka 20.
Bikamba, ambaye amekana tuhuma hizo anadaiwa kufanya unyama huo baada ya kumpa dawa za kulevya.
Taarifa kutoka duru za karibu za uchunguzi wa kesi hiyo zinasema kuwa gavana huyo alimbaka binti huyo siku ya Jumamosi.
Bikamba kwa sasa yuko gerezani akisubiri kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka mawili ya kumwekea dawa za kulevya na kumfanyia tendo la ngono binti huyo bila ridhaa yake.
Lakimni
Wakili wa gavana huyo, Imbambo Engulu ametupilia mbali tuhuma hizo na kuishutumu mahakama ya jimbo hilo kwa kumtia korokoroni mteja wake bila kujali na cheo chake.
“Kushikwa kwake ni kama uonevu, tuliomba wamweke kwanza katika kizuizi cha nyumbani badala ya moja kwa moja gerezani, lakini majaji hawakukubali ombi letu, Nawambia kweli kuwa gavana hakufanya kitendo hicho, ni uongo,” alisema Engulu
Waziri wa Sheria, Faida Mwangiliwa ambaye pia ni miongoni mwa wanaharati wa haki za wanawake, ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa gavana huyo iwapo itathibitisha tuhuma hizo.
Kesi za ubakaji zimeripotiwa kwa wingi DRC. Matukio mengi zaidi yakifanywa na waasi na askari wa Serikali hasa mashariki mwa DRC.
Hivi karibuni, Serikali ya DRC imekuwa ikitoa adhabu kali kwa askari na maofisa wake wa jeshi wanaothibitika kufanya vitendo hivyo, ikiwamo kifungo cha maisha .