25.7 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Gavana anayetuhumiwa kuua mwanafunzi kuendelea kusota rumande Kenya

NAIROBI, KENYA

GAVANA wa Migori, Okoth Obado na wasaidizi wake wawili wataendelea kubakia rumande baada ya Mahakama Kuu jana kusema itaamua maombi yao ya dhamana Ijumaa wiki hii.

Mahakama imeuruhusu upande wa mashtaka kuongeza shtaka katika kesi inayowakabili ya mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno.

Upande wa mashtaka uliwasilisha ombi hilo dhidi ya Obado, msaidizi wake binafsi Michael Juma Oyamo na karani wa Bunge la Kaunti ya Migori, Casper Obiero kufuatia kifo cha mtoto aliyekuwa tumboni mwa Otieno.

Kwa sababu hiyo, washukiwa hao watatu wanakabiliwa na mashtaka mawili ya mauaji ya Otieno na kichanga kilichokuwa tumboni, kinachoelezwa kuwa cha Obado.

Mahakama jana ilikuwa ikisikiliza mpango wa waendesha mashtaka kuongeza shtaka na maombi ya washukiwa kutaka kuwa nje kwa dhamana.

Kutokana na uamuzi huo, washukiwa watabakia polisi hadi Ijumaa hii, wakati mahakama itakapoamua iwapo waachiwe kwa dhamana au la.

Hata hivyo, Shirikisho la Wanasheria Wanawake na mama wa Otieno waliwasilisha maombi kutaka washukiwa wabakie rumande hadi kesi hiyo itakapokamilka.

Mwezi uliopita, Obado aliyekaa rumande kwa wiki mbili sasa, alishtakiwa kwa tuhuma za mauaji ya Otieno, shtaka ambalo alilikana.

Kwa muda wa siku kadhaa sasa, gavana huyo amekuwa akiendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Kenyatta (KNH), baada ya kuugua akiwa rumande katika Gereza la Viwandani jijini Nairobi.

Wakili wake, Evans Ondieki aliwaambia wanahabari kwamba mteja wake huyo anaendelea kupata nafuu.

Inasemekana Sharon (26) alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na gavana Obado.

Mwanafunzi huyo alikuwa na ujauzito wa miezi saba na alitekwa nyara Septemba 3 mwaka huu, kisha akapatikana akiwa ameuawa Septemba 5 katika msitu wa Homa Bay.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Jinali, DCI George Kinoti alisema ana ushahidi wa kutosha kuwashtaki waliotajwa kuhusika na mauaji ya Sharon.

Mauaji hayo yamezua mjadala mkali nchini hapa, huku baadhi ya viongozi kutoka Nyanza wakishinikiza madiwani (MCA) wa Migori kumtimua Obado.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles