ABU DHABI, UAE
KIONGOZI wa Umoja wa Falme za Kiarabu – UAE ametoa amri ambayo inafikisha mwisho rasmi mgomo wa nchi hiyo dhidi ya Israel, kufuatia makubaliano yaliyosimamiwa na Marekani ya kurejesha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.
Amri hiyo inafuta kabisa sheria namba 15 ya mwaka 1972 pamoja na adhabu inayotokana na ukiukaji wa marufuku hayo, kwa mujibu wa shirika la habari la WAM.
Muafaka huo unaoyarejesha mahusino kati ya Israel na UAE uliotangazwa Agosti 13. Uliihitaji Israel kusitisha mpango wake tata wa kuinyakua ardhi inayoikalia ya Ukingo wa Magharibi ambayo Wapalestina wanaihitaji.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo akiwa pamoja na Mfalme wa Bahrain Hamad bin Issa Al Khalifa alipotembelea Manama
Shirika la habari la serikali WAM limesema hatua hiyo ya kuondoa mgomo dhidi ya Israel imefanywa kwa amri ya Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan, mtawala wa Abu Dhabi na kiongozi wa Falme za Kiarabu.
Amri hiyo mpya inawaruhusu Waisrael na makampuni ya Israel kufanya biashara na UAE, ambalo ni shirikisho la falme saba katika Rasi ya Uarabuni.
Hatua hiyo pia inaruhusu ununuzi na kufanya biashara kutumia bidhaa za Israel.
Kufikishwa mwisho kwa ususiaji huo kunaruhusu watu binafsi na makampuni kufanya makubaliano na vikundi na watu binafsi ambao wanaishi nchini Israel, kuwa na uraia wa Israel ama kufanyakazi kwa niaba ya Israel popote pale. Pia inaruhusu kuingia, kubadilishana, kumiliki na kufanya biashara kwa kutumia bidhaa za Israel ndani ya UAE.
Israel na UAE zilitangaza makubaliano ya kurejesha mahusiano ili kupata kutoka Israel hatua ya kusitisha mpango wake tata wa kunyakua sehemu ya eneo linalokaliwa na Israel la Ukingo wa Magharibi.
Makubaliano hayo yanaifanya UAE kuwa nchi ya tatu ya Kiarabu baada ya Misri na Jordan na nchi ya kwanza ya Ghuba ya Uarabuni, kuwa na mahusiano ya kidiplomasia na Israel.
Kumekuwa na uvumi mkubwa juu ya iwapo mataifa mengine ya Kiarabu yatafuata mfano huo.
Siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Mike Pompeo alifanya mazungumzo na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, kama sehemu ya ziara yake ya mashariki ya kati, ambayo ilijumuisha Israel, Bahrain na Oman.