Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
RAIS Jakaya Kikwete amekerwa na tatizo la foleni za Dar es Salaam na kusema chanzo chake ni askari wa usalama barabarani kushindwa kuvuta magari kwa utaratibu.
Akizungumza Dar es Salaam jana alipotembelea katika Viwanja vya Maonyesho ya Sabasaba katika Banda la Chuo Cha Ardhi, alisema pamoja na msafara wa magari yake kutokaa katika foleni barabarani lakini anajua hadha wanayoipata wananchi.
“Mimi napita kwa king’ora lakini natamani siku nipite kama watu wengine nione hadha wanayoipata, najua foleni ni tabu katika Jiji la Dar es Salaam ambayo inasababisha watu kutumia muda mrefu barabarani.
“Askari wa usalama barabarani wanavuta magari ya upande mmoja kwa muda mrefu na kuacha mengine yakisubiri,” alisema Rais Kikwete.
Alisema malori nayo ni chanzo kikubwa cha foleni barabarani na alishauri kama kuna uwezekano wahusika watafute njia za pembezoni zitakazoenda moja kwa moja bandarini tofauti na ilivyo sasa inatumika njia moja ambayo ni Barabara ya Mandela.
Alisema katika umbali wa kilomita 4.5 za barabara kunakuwa na malori zaidi ya 300 hadi 500 na mara nyingi yanaenda taratibu kutokana kubeba mizigo na hali hiyo inasababisha foleni kuwa ndefu zaidi.
Alisema kujenga barabara za juu ni njia mojawapo ya kuondoa tatizo lakini haitosaidia kama hakutakuwa kuwa na utaratibu mzuri wa malori.
Katika hatua nyingine, alisema kuna wawekezaji kutoka Hong Kong nchini China wanatarajia kuja kujenga jengo la ghorofa 50 kwa ajili ya biashara.
“Hawa watu nimeshawakubalia kwa sasa tupo tunahangaika na watu wa mipango miji kwa ajili ya kuwapatia kiwanja lengo lao wajenge katika eneo ambalo litakuwa linaonekana,” alisema Rais Kikwete.
Pia alisisitiza matumizi ya Mashine za Elektroniki za kutoa Risiti za Kodi (EFDs).
Msisitizo huo aliutoa alipotembelea Banda la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
“Lazima tukazanie matumizi ya EFDs, hatuwezi kuendelea na mambo ya kizamani,” alisema Rais Kikwete.