29.8 C
Dar es Salaam
Sunday, September 15, 2024

Contact us: [email protected]

Mkataba wa gesi wavuja

gesi mtwara
gesi mtwara

NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

MKATABA wa mgawanyo wa mapato yanayotokana na uzalishaji wa gesi asilia kati ya Shirika la Mafuta Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Mafuta ya StatOil ya Norway, umevujishwa.

Mkataba huo ambao unadaiwa utaipotezea Tanzania Sh trilioni 1.6 kwa mwaka, umevuja na kusambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kuzua mijadala kutokana na mgawanyo wake kutoeleweka wazi.

Kwa mujibu wa makala yaliyoandikwa na jarida la mtandaoni la African Arguments, Tanzania itapoteza zaidi ya Sh trilioni 1.6 kila mwaka kulingana na viwango vya uzalishaji wa gesi asilia katika kitalu namba mbili.

Kitalu hicho kinamilikiwa na Kampuni ya StatOil na Kampuni ya ExxonMobil ya Marekani.

Pamoja na mambo mengine, mgawanyo huo pia unadaiwa kuwa ni sehemu ya Norway kujilipa fedha zake za misaada mbalimbali waliyoitoa nchini kupitia mkataba huo.

“Tangu Tanzania ipate uhuru, Norway imetoa misaada ya thamani ya Dola za Marekani bilioni 2.5 wakati kwa mkataba huu na Kampuni ya StatOil ambayo inamilikiwa na Serikali ya Norway kwa miaka 15 watapata dola bilioni 5.6.

“Kwa hiyo kwa miaka saba tu Norway itakuwa imerudisha misaada yake yote mara mbili zaidi,” ilisema sehemu ya makala hayo katika mtandao wa African Arguments.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema) amesema katika taarifa yake kwamba, kuvuja kwa mkataba huo kumesaidia kuona ukweli wa matamko ya viongozi kuhusu ni namna gani Tanzania itafaidika na utajiri wake wa gesi.

Alisema kama mkataba huo mmoja taifa litapoteza matrilioni ya fedha, hali ikoje katika mikataba mingine 29.

Kwa mujibu wa Zitto, hivi sasa ugunduzi wa gesi asilia nchini ni lita za ujazo trilioni 51 ambazo ni sawa na mapipa bilioni 10 ya mafuta.

“Katika gesi asilia iliyopatikana nchini, StatOil peke yao wana jumla ya lita za ujazo trilioni 20, sawa na mapipa ya mafuta bilioni 4 ambazo ni zaidi ya mafuta yaliyogunduliwa nchini Uganda na Ghana kwa pamoja.

“Hata hivyo, utajiri wote huu utainufaisha zaidi Norway na Marekani kupitia kampuni zao kuliko watu wa Tanzania, Watanzania watabaki kupewa misaada ya vyandarua na mataifa haya ilhali wanafaidi gesi asilia yetu.

“Natoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini kutoa tamko kuhusu mkataba huu kati ya TPDC na StatOil, vile vile Kampuni hii ya StatOil kutoka nchi rafiki mkubwa wa Tanzania ina wajibu wa kutoa maelezo ya kina.

“Serikali ieleze ni hatua gani inachukua kurekebisha mkataba huu na StatOil nao waeleze watachukua hatua gani kuhakikisha wanaacha unyonyaji huu mkubwa na wa aibu kwa taifa la Norway,” alisema Zitto.

Alisema ni wakati muafaka kwa Watanzania kuona mikataba yote ya gesi na mafuta ambayo Serikali imeingia na wawekezaji.

Zitto alisema mkataba huu wa StatOil uliovujishwa uwe ni chachu ya kulazimisha Serikali na kampuni kuweka mikataba yao wazi kwa kuanza mashinikizo hayo sasa kwa faida ya vizazi vijavyo.

“Mwanzoni wengi wetu tulidhani kuwa tatizo la mkataba huu ni eneo la umiliki wa kampuni tu kulingana na namna ulivyowasilishwa, kumbe mgawanyo mzima wa mapato unakwenda kinyume na maelezo ya Serikali na TPDC kwa umma.

“Mkataba uliovuja unaonyesha kwamba, makubaliano ambayo Serikali imeingia na wawekezaji hawa wa Norway yanakwenda kinyume na mfano wa mkataba unaotakiwa kusainiwa (Model PSA).

“Uchambuzi nilioufanya kulingana na viwango vya mgawo wa mapato kati ya PSA na mkataba huu unaonyesha kwamba, Tanzania itapata mgawo kiduchu sana na kinyume na mgawo unavyopaswa kuwa,” alisema.

Kwa mujibu wa sheria mkataba wa mgawanyo wa mapato unaopaswa kutumiwa na TPDC katika mikataba na wawekezaji inatakiwa kilo 0-249.999 katika viwango vya uzalishaji kila siku, TPDC wapate asilimia 50 na mwekezaji asilimia 50.

Kilo 250 hadi 499, TPDC wapate asilimia 55 na mwekezaji asilimia 45 na kilo 1,500 na kuendelea TPDC wapate asilimia 80 na mwekezaji asilimia 20.

“Tofauti na mkataba huu, katika kilo 0- 299.999 za gesi ya viwango vya uzalishaji kila siku, TPDC inapata asilimia 30 na StatOil asilimia 70, kilo 300-599.999 TPDC asilimia 35 na mwekezaji asilimia 65 na kilo 1,500 na kuendelea ndiyo wote wanapata asilimia 50 kwa 50,” alisema.

Kwa mgawanyo huo wa mapato alisema utaifaidisha zaidi Kampuni ya StatOil ambayo ni kinyume na mkataba unavyopaswa kuwa.

“Wakati mgawo wa nusu kwa nusu upo katika uzalishaji wa chini kabisa kwenye ‘model PSA’, kwenye mkataba wa StatOil mgawo huo upo kwenye uzalishaji wa juu kabisa.

“Ukilinganisha mgawanyo huu wa mapato, iwapo kiwango cha ‘model PSA’ kingetumika Tanzania ingepata shilingi trilioni 1.6 zaidi ya kiwango itakachopata kwenye mkataba wa sasa uliovujishwa, hii ni kutokana na bei ambazo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limeweka katika uchambuzi wake kuhusu gesi asilia ya Tanzania,” alisema.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alikataa kuzungumzia kuhusu mkataba huo huku akielekeza watafutwe TPDC na Kampuni ya StatOil huku akihoji ni vipi kuvuja kwa mkataba ndiyo kunafanya Tanzania ipoteze fedha hizo.

Alisema kama mkataba una makosa au umevuja wa kuwaona ni hao waliotajwa.

“Huyo mtu aliyetuma sijui kuandika hayo ninyi wenyewe mmemfanyia uchunguzi ni mtu wa namna gani, maana siku hizi mtu yeyote nchi hii anaweza kuhongwa Dola 200 akaandika au kuzungumza chochote hata bungeni.

“Mimi nina vitu vingi vya kufanya zaidi ya kupitia hayo mambo ya kwenye mitandao, ukiacha kazi niliyopewa nina kazi ya taaluma yangu ya jiolojia ambayo naifanya kila siku,” alisema Profesa Muhongo.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Enyi watanzania mko wapiii??? nchi hii inakoendea siko, kwan tunaendekeza kusaidiwa ndio maana tunaingia hasara kama hii ya kuinufaisha nchi ya norway ukizingatia norway ni nchi tajiri kati ya nchi tajiri duniani na bado utajiri wetu tunawapa wao, kwa nini nchi inaingia mikataba bila kushirikisha wananchi na kujikuta tumeingia mikataba feki na inayotuumiza ukizingatia ajira kwa vijana bado ni duni hakuna huduma muhimu hakuna elimu nzuri kwa nin nchi yetu tumekuwa na giza nene lisilotoka??? tunaiomba serikali iingilie kati na kupunguza muda wa mikataba hii feki kwan tunaishia kuomba mpaka mwisho wa dunia hili ni janga kwa kizazi kijacho na maisha yanazid kuwa magumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles