FILAMU inayozungumzia masuala ya rushwa ya ‘Homecoming’, baada ya kukamilika itaanza kuonyeshwa katika kumbi mbalimbali za sinema kuanzia mwezi ujao.
Muongozaji na mwandishi wa filamu hiyo, Seko Shamte, alisema filamu hiyo iliyoandaliwa na kampuni ya Alkemist Media inaonyesha namna vijana walivyo katika hatari kubwa ya kushiriki rushwa kutokana na ushawishi wa mazingira yanayowazunguka na namna wanavyoshindwa kukwepa vishawishi hivyo.
“Wazo la filamu hiyo lilianzia mwaka 2009, lakini mwaka 2013 ndipo wazo hilo lilipofanyiwa kazi ambapo mchanganuo ukapelekwa Mfumo wa Habari Tanzania, (TMF) kwa udhamini kabla ya kuanza kazi rasmi 2014,” alieleza Seko.
Seko alimtaja mwigizaji mkuu wa filamu hiyo kuwa ni Daniel Kijo, anayecheza kama mhitimu anayerejea nchini kutokea Marekani alikoishi zaidi ya miaka 10 na pia ndipo alipohitimu masomo yake, lakini baada ya kupata kazi ya benki anaingia katika matatizo makubwa ya rushwa.
Waigizaji wengine walioshiriki katika filamu hiyo ya dakika 120 ni Ahmed Olotu ‘Mzee Chilo’, Susan Lewis, Hashim Kambi na Abby Plaatjes, ambaye aliwahi kuwa mshiriki wa Big Brother Africa na wengine wengi.