29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Fidel Castro: Nyota ya Amerika Kusini iliyoanguka

Fidel Alejandro Castro Ruz
Fidel Alejandro Castro Ruz

NA FREDERICK FUSSI,

Fidel Alejandro Castro Ruz msomi wa shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Havana anayejulikana Amerika ya Kusini (Latin America) na ulimwenguni kama Mwanamapinduzi nchini Cuba aliyeingia madarakani mwaka 1959 baada ya kumpindua aliyekuwa Rais wa Taifa hilo Fulgencio Batista, amefariki dunia akiwa na miaka 90  Novembe 25, 2016.

Castro ndio kiongozi pekee duniani mwanamme baada ya Malkia Elizabeth wa Uingereza kuwa mtawala wa Taifa kwa miaka mingi zaidi takribani miaka 47, karibuni mara mbili zaidi ya miaka ambayo Mwalimu Nyerere aliyekaa madarakani hapa nchini kwa miaka takribani 24. Wakati Afrika kiongozi anayeongoza kwa kukaa madarakani muda mrefu ni Rais Robert Mugabe miaka  takribani 36, wakati mwenzao Nelson Mandela mpigania Uhuru na Mwanamapinduzi wa Afrika kusini akikaa madarakani miaka mitano tu kwa kipindi kimoja na kujijengea heshima duniani na kuweka rekodi ambayo pengine Castro na wenzake waliokaa madarakani miaka mingi hawana!

Fidel Castro ameishi miaka 90 duniani na kutumia zaidi ya nusu ya maisha yake duniani kama kiongozi pekee (maximum leader) wa Taifa la Cuba tangu mwaka 1959. Sera zake kuhusu ukomunisti, uhusiano wake kati ya Umoja wa Kisovieti enzi zile (Soviet Union) na kusuasua kwa uhusiano baina yake na Taifa la Marekani na kuweza kulitunishia misuli taifa hilo, kusaidia harakati za kimapinduzi katika nchi za Afrika ikiwamo Angola na Msumbiji, uwezo wake wa kuidhibiti Cuba kama kiongozi ni moja ya mambo mengi yanayomfanya Fidel Castro afahamike zaidi duniani.

Castro alipoingia madarakani mwaka 1959 akiwa anaungwa mkono na wananchi wengine wengi ambao hawakupendezwa na uongozi wa kidikteta wa Batista aliahidi mambo mengi ikiwamo kuleta uongozi wa kidemokrasia ambao hata hivyo haukuwahi kuwapo katika kipindi chote cha uhai wake! Castro hakuwahi kuwa na nia ya kung’atuka madarakani mpaka ugonjwa upomlazimisha kufanya hivyo mwaka 2006 alipoanguka jukwaani wakati anatoa hotuba kwa wafuasi wake! Castro pamoja na kufanya Mapinduzi nchini Cuba aliamua kuondoa haki za kisiasa, kiuchumi na kuamua kubana uhuru wa kujielezea (freedom of expression).

Castro aliweza kuwa mtawala wa muda mrefu kutokana na kipaji chake cha kuwa na akili sana na uwezo wake wa kujenga hoja, kuzitetea na kuwashawishi wengi kati ya watu wa Cuba, pengine wenye akili za kawaida! Taifa la Cuba liliendelea katika sera za elimu na afya hasa kutokana na kipaji cha Castro kuingiza sera za ukomunisti na baadaye ujamaa katika elimu na hivyo kuwafanya watu wengi wa Cuba kuwa watiifu kwa utawala wake kutokana na masomo waliyosoma kuwalazimisha kufanya hivyo hasa katika ubunifu wa mitaala. Mbali na kuboresha mazingira ya kujifunzia ikiwa pamoja na maslahi mazuri kwa walimu, Castro alitumia mitaala na mfumo wa elimu ya Cuba kama njia ya kuhalalisha utawala wake wa kidikteta uliodumu kwa miaka 47 ambapo baada ya afya yake kuzorota uongozi wa nchi alimuachia mdogo wake Raul Castro, ambaye hivi sasa ana miaka 85.

Elimu nchini Cuba hutolewa bure mpaka chuo kikuu ambapo uchaguzi wa nani aende chuo kikuu hudhibitiwa na Serikali kwa asilimia mia moja. Benki ya Dunia katika moja ya ripoti zake mwaka 2014 imeitaja Cuba kuwa na elimu bora zaidi katika nchi za Amerika ya Kusini. Pamoja na hayo Cuba inatajwa kuwa na maendeleo makubwa sana katika sekta ya huduma za afya ukilinganisha na mataifa mengine katika Bara la Amerika ya Kusini.
Mbali na kukosekana kwa demokrasia chini Cuba haibishaniwi kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Benki ya dunia kuwa Cuba imepiga hatua kubwa sana katika elimu hususani kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali na uwezo wa kuwatumia wataalamu hao kuleta maendeleo ikiwa ni pamoja na malipo na maslahi mazuri sio tu kwa walimu lakini pia kwa wataalamu. Juhudi hizi zinatambuliwa kama moja ya uwezo aliokuwa nao Fidel Castro kubadilisha hatima ya Taifa hilo kufikia mafanikio hayo! Castro alifanikiwa kuifanya elimu ya Cuba kuwa ya vitendo zaidi ya kuwa ya nadharia, kwa mfano inakadiriwa kuwa wanafunzi wanaojifunza ualimu hutumia asilimia 72 ya muda wao wa masomo kufundisha kwa vitendo katika shule mbalimbali.

Walimu nchini Cuba wanawajibika kwa matokeo ya wanafunzi, wanaweza kufukuzwa kazi kutokana na matokeo mabaya ya wanafunzi katika shule za umma, suala hili huwafanya walimu kuongeza juhudi katika ufundishaji, hasa kutokana na motisha ambayo tayari Serikali ya Cuba imeiweka katika msisitizo wa elimu ndani ya Taifa hilo! Huwezi kufananisha kwa mfano Taifa la Cuba na Tanzania katika elimu ambapo Tanzania shule moja huweza kukaguliwa kila baada ya miaka mitano wakati Cuba ufuatiliaji wa ufundishaji wa walimu hufuatiliwa mara kwa mara kwa wakuu wa shule waliopewa madaraka ya kusimamia ubora wa elimu!

Chini ya Uongozi wa Fidel Castro, huduma za afya kwa wananchi wa Cuba hutolewa na Serikali kupitia hospitali za umma na hakuna hospitali binafsi zinazotoa huduma hiyo nchini humo.  Ilipofika mwaka 2005 Cuba ndio ilikuwa nchi pekee duniani inayoongoza kwa kuwa na huduma bora za afya kwa maana ya idadi ya madaktari kwa kila mtu. Wastani wa watu 10,000 Cuba hutibiwa na madaktari 67 wakati nchini Marekani mwaka 2005 madaktari 24 walitibu watu 10,000 na Urusi idadi ya madaktari 43 walihudumia watu 10,000, hivyo kuifanya Cuba kuwa na madaktari wengi zaidi kufikia watu duniani pamoja na kuwa Taifa hilo kuwa na watu milioni 11.

Hatua hii ya maendeleo katika taaluma ya afya inaifanya Cuba kuwa ndio nchi pekee duniani inayoongoza kwa kutoa wataalamu wengi wa afya katika nchi zinaendelea zaidi hata ya nchi nane zilizoendelea zaidi kiviwanda duniani maarufu kama G8. Rekodi hii ya Cuba inatokana na uongozi wa Kidikteta  wa Fidel Castro uliodumu Cuba kwa miaka 47. Unahitaji kuwa na akili sana kama Fidel Castro kuongoza Taifa kidikteta kwa miaka 47 na kuweza kuongoza kuwa na wataalamu wengi zaidi katika sekta ya afya, pengine rekodi hii hakuna dikteta mwingine duniani amewahi kuiweka ukimuacha Marehemu Castro!

Rekodi hizi kubwa katika elimu na Afya zinamfanya Fidel Castro kuwa ni nyota wa Bara la Amerika ya Kusini iliyoanguka ghafla baada ya miaka 90 ya uhai wake duniani!

Fidel Castro ndio kiongozi pekee duniani wa Taifa ambaye amenusurika kuuawa na mahasimu wake wa kisiasa  zaidi ya mara mia sita (600) huku Shirika la Kijasusi la Amerika CIA liktajwa na vyombo mbalimbali vya habari kuhusika katika majaribio hayo! Castro aliyezaliwa Agosti 13, 1926 akiwa na miaka 25 aligombea ubunge mwaka 1952 na kabla ya uchaguzi Serikali ilipinduliwa na Dikteta Batista akachukua hatamu ya uongozi Cuba. Akiwa na wenzake 150 Castro alijaribu kuipindua Serikali ya Batista jaribio lililofeli na Castro kufungwa jela miaka 15 jambo lilipompa umaarufu Cuba. Mwaka mmoja baadaye aliachiwa kwa msamaha wa Batista ambapo alikimbilia nchini Mexico, ambapo alianza harakati za ukombozi wa Cuba mpaka alipofanikiwa kumuangusha Batista mwaka 1959.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles