Na CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM
KUKITHIRI kwa vitendo viovu na udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya wafanyabiashara kwa kupenyeza bidhaa hafifu kulichangia kwa kiasi kikubwa kudidimia kwa maendeleo ya viwanda mbalimbali hapa nchini.
Pia baadhi ya bidhaa hizo zilikuwa zikichangia uwezekano wa wananchi kufanya madhara mbalimbali ya kiafya.
Serikali ili kulinda walaji, wazalishaji na wawekezaji iliamua kuunda mamlaka mbalimbali ili kudhibiti vitendo hivyo.
Tume ya Ushindani hapa nchini (FCC), ni chombo cha Serikali cha Usimamizi wa mfumo wa uchumi wa soko kilichoundwa kwa sheria ya ushidani namba 8 ya mwaka 2003 ili kulinda na kuimarisha ushindani na kumlinda mlaji dhidi ya mienendo potofu.
Lengo la sheria ya ushindani ni kuimarisha na kuboresha hali ya maisha ya Watanzania kwa kuimarisha na kulinda ushindani madhubuti katika soko na kuzuia mienendo isiyo ya haki na potofu sokoni.
Lengo la yote hayo ni kuongeza ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma, kukuza ubunifu, kuboresha matumizi ya rasilimali kwa kuzingatia ufanisi na kumlinda mlaji dhidi ya mienendo potofu katika soko.
Tume hii imejidhatiti katika kutetea na kusimamia haki za mlaji, lakini pamoja na jitihada zake za kumwelimisha mlaji, bado mwamko ni mdogo.
Jitihada zaidi zinahitajika kutoka kwa wadau wote kusambaza elimu kwa mlaji ili waone haja ya kuchukua hatua na kutetea haki zao.
Kumlinda mlaji ni dhamira kuu ya wazalishaji wa bidhaa na huduma. Licha ya kupata faida katika shughuli wanazozifanya pia wamejengwa katika misingi mikuu mitatu ambayo ni elimu, utatuzi wa migogoro na utekelezaji wa sheria.
Tume ya Ushindani ina kurugenzi inayoshughulikia na kuchukua hatua za awali za upatanishi na kutoa ushauri wa namna ya kutetea haki za mlaji kwa mujibu wa sheria.
Lakini uamuzi wa kesi na malalamiko ya mlaji kwa masuala hayo hayafaywi na Tume ya Ushindani wala Baraza la Ushindani bali hushughulikiwa na mahakama za kawaida jambo ambalo ni changamoto kubwa.
Changamoto hiyo inakuja kutokana na ukweli kwamba suala linapofika mahakamani, kwanza linachukua muda mrefu hadi kufikia hukumu kutolewa na kutokana na hali hiyo, walaji wengi wanashindwa kuendelea na kesi hivyo kujikuta wakiacha kudai haki zao.
Aidha, kesi inapochukua muda mrefu baadhi ya walaji wanashindwa kufuatilia kutokana na usumbufu wanaokutana nao ikiwamo kushindwa gharama nyingine zinazohitajika pale ambapo shauri linapoendelea.
Wakati mwingine walaji hukosa muda wa kufuatilia kutokana na kutingwa na shughuli ya kujitafutia kipato.
Akitoa mada kwenye mafunzo ya siku moja yaliyowashirikisha waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari, kuhusu utekelezaji wa sheria katika kumlinda mlaji, Mkuu wa Idara ya Elimu kwa Mlaji kutoka FCC, Magdalena Utouh, anasema katika kipindi cha mwaka huu wamepokea malalamiko zaidi ya 180 na kwamba malalamiko hayo yameongezeka tofauti na miaka ya nyuma.
Anasema elimu inayotolewa ya kuwajengea uwezo walaji, imesaidia kugundua haki zao zilizovunjwa hivyo kwenda mahakamani kutoa malalamiko kwa tume na kuchukuliwa hatua.
Anasema asilimia 95 ya malalamiko hayo yameshughulikiwa ikiwa ni pamoja na ama mlaji kurudishiwa fedha zake alizotoa kwa ajili ya kupata huduma ama kupewa bidhaa mbadala.
Utouh anasema zaidi ya mikataba 150 imepitiwa kutoka kwenye taasisi za fedha kama benki na zile zinazotoa mikopo ya kifedha kwa wananchi.
“Katika upitiaji wa mikataba hiyo, tumebaini kwamba taasisi zinazotoa mikopo zinalalamikiwa na wananchi na kwamba wananchi wanapochukua mikopo wanateseka katika urejeshaji wa mikopo hiyo,” anasema Magdalena.
Anasema mfano mtu ana shida ya mkopo, taasisi inayotoa mkopo huo kwa kuwa na yenyewe inataka faida haimpi taarifa za kutosha kuhusu mkopo jambo ambalo limekuwa likileta utata wakati wa urejeshaji deni.
Anasema mkopaji hujikuta akilipa riba kubwa lakini anajikuta kuwa hana pa kutokea kwa kuwa amekwisha saini mkataba, hapo ndipo malalamiko yanapokuja.
Magdalena anasema taasisi nyingine za mikopo kwenye fomu ya kuomba mkopo unakuta maandishi madogo ambayo mkopaji hata kuyasoma anaona shida na kwa kuwa hitaji lake ni mkopo hasomi isipokuwa yeye anakimbilia kusaini tu fomu hizo na kuchukua fedha bila kuwa na taarifa za kutosha.
Anasema sasa changamoto inakuja pale uamuzi wa kesi na malalamiko kama hayo yanaposhughulikiwa na Mahakama badala ya tume, na kwamba wakati umefika sasa kwa tume kupewa nguvu zaidi ya kisheria kushughulikia uamuzi wa kesi na malalamiko ya walaji.
Anataja changamoto nyingine kuwa ni ufinyu wa rasilimali watu na fedha, uelewa mdogo wa haki na wajibu wa mlaji japo tume inaendelea na jitihada za kutoa elimu katika maeneo mbalimbali nchini.
“Walaji wanapaswa kuwa makini na kuanzisha vyombo vyao vyenye nguvu ya kuangalia masuala ya sera ili waweze kujitetea pale haki zao zinapovunjwa,” anasema Magdalena.
Anasema japo kifungu cha 92-95 cha sheria hiyo ya ushindani kimeelekeza uanzishwaji wa Baraza la Ushauri kwa mlaji, kazi zake, uendeshaji wake na masuala ya kifedha, suala hilo bado linashindikana kutokana na ukosefu wa rasilimali fedha.
Anasema Baraza la ushauri kwa mlaji ni kitu muhimu lakini linashindwa kufikiwa kwa sababu ya uhaba wa fedha, hata hivyo lilikuwapo miaka ya nyuma lakini lilivunjika kutokana na ukosefu wa fedha.
Anasema walaji ndio wanaweza kuwashughulikia wafanyabiashara au watoa huduma ambao wanaenda kinyume cha sheria ya Ushindani na si mtu mwingine.