Na ANDREW MSECHU
-DAR ES SALAAM
RAIS wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS) anayemaliza muda wake, Fatma Karume, amesema hatawania tena nafasi hiyo kwa sasa kutokana na majukumu yanayomkabili.
Fatma ambaye alichukua nafasi hiyo Aprili mwaka jana akipokea kijiti kutoka kwa aliyekuwa mtangulizi wake, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amevunja ukimya baada ya taarifa za awali kuonyesha si miongoni mwa waiojitokeza kuchukua fomu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Fatma alisema amechukua uamuzi huo kwa kuwa anahitaji kuelekeza nguvu kusimamia biashara zao.
“Sitagombea mwaka huu. Washirika wangu wanapendelea nitumie muda wangu mwingi kwa sasa katika biashara zetu na kutokana na ushirikiano walionipa kwa mwaka mzima uliopita, sitawaangusha,” alisema.
Kauli hiyo inamaliza utata uliokuwa umejitokeza awali kuhusu kama atagombea nafasi hiyo kwa mara nyingine au la.
Ukimya mkubwa ulikuwa umetanda katika kipindi cha kuomba nafasi ya uongozi wa chama hicho ambacho kinafikia tamati Jumatano wiki ijayo.
Ukimya wa Fatma pia ulitajwa kuwaweka njia panda zaidi baadhi ya wanachama wa TLS hasa wale waliokuwa na matumaini ya kuona kiongozi huyo anatetea kiti chake.
Licha ya kamati ya uchaguzi ya chama hicho Februari 13 mwaka huu kutangaza imesogeza mbele hatua ya kupokea maombi ya wagombea hadi Jumatano wiki ijayo, Fatma alikuwa hajajitokeza kuonyesha nia ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Hata hivyo katika akaunti yake ya Twitter yenye utambulisho wa jina la Fatma Karume a.k.a Shangazi, juzi aliandika ujumbe uliosomeka, “Good morning everyone . Najua nilikuwa kimya kwa muda. Don’t worry hawajaniteka ili nikae kimya, niko busy kidogo.”
Katika uchaguzi wa mwaka jana, Fatma alijitokeza katika dakika za mwisho mwisho kuwania urais wa TLS na kufanikiwa kiti hicho kwa kuonekana na ni mtu sahihi wa kumrithi Tundu Lissu ambaye alikuwa anamaliza muda wake.
Fatma alichuana na kufanikiwa kuwabwaga Godwin Mwapongo, Godfrey Wasonga na Godwin Ngwilimi ambao tayari walikuwa wameonyesha kuwa na ushawishi mkubwa wa kuchaguliwa.