23.3 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Polisi yatoa sharti zito kwa Chadema

Na ANDREW MSECHU

-DAR ES SALAAM

JESHI la Polisi limetoa masharti magumu kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),   likiwataka viongozi wa chama hicho kufuata sheria na maelekezo ya  mikutano katika majimbo na kata zao.

Masharti hayo yalitolewa jana ikiwa ni siku mbili baada ya viongozi wa Chadema waliomaliza kikao chao cha Kamati Kuu   wiki iliyopita kutoa   maazimio ya kufanya mikutano ya hadhara.

Walieleza kuwa kwa sasa wanaandaa ratiba ya kuanza mikutano  hiyo itakayofanyika mchana peupe huku wakijikita katika sera bila kupambana na mtu.

Wakati wakisema hayo, Jeshi la Polisi nchini limepokea taarifa hiyo kwa tahadhari likisema hakuna mtu anayekatazwa kufanya mkutano kwenye eneo lake, kinachotakiwa ni kutoa taarifa mapema.

Msemaji wa Polisi,   Ahmed Msangi alisema jana kuwa vyama vya upinzani havijazuiwa kufanya mikutano ya hadhara ila vinatakiwa kufuata taratibu za  sheria.

Alisema taratibu hizo ziko wazi na viongozi wote wa vyama vya siasa wakiwamo Chadema wanazijua, kwa hiyo hakuna anayezuiwa kufanya mikutano hiyo iwapo watazifuata.

Akizungumza na MTANZANIA,   Msangi, alisema utaratibu wa  sheria unawataka viongozi wa vyama vya siasa kuwasilisha barua ya kuomba kibali ndani ya saa 48 kabla ya kufanyika  mikutano hiyo.

“Sisi wakifuata taratibu zote zinazoelekezwa katika sheria hatuana wasiwasi, watume hizo barua saa 48 kabla ya kufanyika  mkutano na sisi tunatoa vibali. 

“Ila ikumbukwe kuwa ni kila mtu kenye jimbo lake. Ni kwamba hatujazuia mtu kufanya mkutano kwenye jimbo lake,” alisema. 

Alipoulizwa kuhusu nafasi ya viongozi wakuu wa vyama   ambao wanatakiwa kujenga vyama maeneo yote ya nchi hivyo kuhitajika kufanya mikutano ya hadhara kwenye maeneo yote, alijibu kwa ufupi; “Hao wote wanajua utaratibu na walishapekwa maelekezo.” 

Msimamo mpya Chadema 

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu agizo hilo la polisi, Mkurugenzi wa Itikadi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema watahakikisha viongozi wakuu wanatumia haki yao kupitia sheria namba tano ya Vyama vya Siasa na kulitaka Jeshi la Polisi kusimama kwenye sheria na lisitake kujificha kwenye matamko yasiyo ya  sheria.

Alisema msingi wa sheria unawataka viongozi wa siasa kutoa taarifa polisi   wapate ulinzi na si kuomba kibali na ndivyo watakavyofanya.

“Polisi wanaposema wanaoruhusiwa ni wabunge kwenye majimbo yao wanatumia sheria gani? Mbona Dk. Bashiru Ally anazunguka huko na huko akifanya kampeni.

“Yeye ni mbunge wa wapi? Au Polepole anapozunguka kuko na huko kufanya kampeni yeye ni mbunge wa wapi?” alihoji.

Alisema viongozi wa Chadema watafuata taratibu za  sheria na watatumia haki yao ya  katiba kufanya mikutano hiyo katika maeneo yote ya nchi hasa kipindi hiki ambacho taifa linaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Awali, akizungumzia msimamo wa chama baada ya kikao kilichofanyika Februari 9 hadi 10, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vicent Mashinji  alisema si kwamba Chadema imerudi nyuma kufanya mikutano ya hadhara, bali walikuwa wametingwa na majukumu mengine lakini wanaandaa utaratibu.

“Tumeona CCM huko Karatu wamefanya mikutano ya hadhara na kukashifu. Sisi tulishaamua tutafanya mikutano ya hadhara na mchana peupe kwa sababu  kufanya mikutano si jinai.

“Tunaandaa ratiba, niwatake wapenda demokrasia duniani kupinga kuingiliwa. Tuna sera zetu, hatutakuwa na muda mchafu wa kupambana na watu,” alisema Dk. Mashinji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles