Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Kampuni ya Fastjet Tanzania imekanusha kujitoa katika biashara ya usafiri wa anga nchini na kufafanua kuwa Kampuni mama (Fastjet PLC) ndiyo iliyojitoa kwa kuuza hisa zake kwenye soko la hisa nchini Uingereza.
Ofisa Habari wa Fastjet, Lucy Mbogoro, ameiambia Mtanzania Digital hayo leo Jumatano Novemba 20, baada ya kuwapo kwa mkanganyiko kwa kampuni hiyo mama kuuza hisa zake jambo lililotafsiriwa litaiweka pabaya kibiashara kampuni hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho Kampuni ya Ndege nchini (ATCL), imefufuliwa na inafanya vizuri sokoni.
“Kampuni ya Fastjet PLC, ndiyo iliyojitoa kama mwekezaji lakini kuna wawekezaji wengine na kwa sasa Lau Masha (Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi), akiwa ni mwekezaji mkubwa, kwa kifupi shirika limekuwa la Watanzania,” amesema Lucy.
Novemba 5, mwaka huu, Masha aliteuliwa kuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Fastjet Tanzania, ambapo moja ya majukumu yake yalikuwa ni kusimamia mpango wa Fastjet Tanzania kujiondoa na kujitegemea kutoka kampuni hiyo mama (Fastjet PLC) ambayo makao makuu yake yako nchini Uingereza.