Na LUSUNGU HELELA-MUSOMA
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, amesema kutokana na kukua kwa teknolojia, maofisa wa idara ya wanyamapori watakuwa na uwezo wa kuwaona faru popote walipo wakati wakiwa ofisini.
Amesema hali hiyo itasaidia kuwalinda wanyamapori hao ambao wapo hatarini kutoweka.
Hasunga amesema maofisa hao watakuwa na uwezo wa kufuatilia mienendo ya wanyama hao popote walipo kujua kama wanaumwa au wana tatizo lolote linalohitaji msaada.
Hasunga aliyasema hayo hivi karibuni alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, baada ya kushuhudia uwekaji wa vifaa vya utambuzi kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa faru wa hifadhi hiyo.
“Hatua hiyo ni muhimu kwenye uhifadhi wa wanyamapori na itasababisha majangili kukamatwa hata kabla ya hawajamuua mnyama,” alisema Hasunga.
Mratibu wa Mradi wa Faru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Phillibert Ngoti, alimweleza naibu waziri kuwa hatua hiyo ya kuweka alama za vifaa vya kisasa, unafanywa katika hifadhi hiyo kwa kushirikina na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (Ncaa), Taasisi za Frunkfurt Zoological Society (FZS) na Friedkin Conservation Fund.
“Hatua ya kuweka vitambuzi hivyo kwenye faru, unafanyika kwa namna mbili, yaani kuna vitambuzi vinavyowekwa ndani ya pembe za faru na kuna vitambuzi vinavyowekwa kwenye mguu mmoja wa mbele wa faru ili kusaidia kujua popote pale walipo,” alisema.
Kiongozi wa Mradi wa Uhifadhi kutoka FZS, Rian Habuschagne, alisema mradi huo umefadhiliwa na Frunkfurt Zoological Society kwa kushirikiana na Friedkin Conservation Society.