23.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Farijala aenda jela tena kwa EPA

Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam

MFANYABIASHARA Farijala Hussein aliyemaliza kifungo kwa kuiba fedha za akaunti ya EPA, amehukumiwa tena kwenda jela baada ya kupatikana na hatia katika kesi nyingine ya wizi wa zaidi ya Sh milioni 400 katika akaunti hiyo.

Vilio vilitawala katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam baada ya Farijala kuhukumiwa kwenda jela miaka mitatu kwa kila kosa na kurudisha zaidi ya Sh milioni 400. Mahakama ilimpa adhabu Farijala ya kwenda jela jumla ya miaka 15 kwa makosa matano aliyotiwa hatiani.
Farijala na mwenzake aliyeachiwa huru, Ajay Somani walisomewa hukumu jana na jopo la mahakimu linaloongozwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Projestus Kahyoza.

Farijala aliwahi kuhukumiwa katika mahakama hiyo na kutiwa hatiani katika kesi namba 1161 ya mwaka 2008 na kesi namba 1164 ya mwaka huo kwa mashtaka kama hayo ya kughushi na kujipatia fedha kwa udanganyifu katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Jopo lilisema kwamba washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na mashtaka sita yakiwamo ya kula njama, kughushi nyaraka mbalimbali na kujipatia Sh 455,874,624.51 kwa kutumia nyaraka za uongo kutoka BoT, fedha ambazo zilikuwa katika akaunti ya madeni ya nje (EPA).

Hakimu Francis Kabwe alisema Ajay anashtakiwa kwa makosa mawili; kula njama na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wakati Farijala anashtakiwa kwa mashtaka sita yakiwamo kula njama, kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya ufanganyifu.

“Katika shtaka la kwanza upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kwamba washtakiwa walikula njama kutenda kosa la kujipatia fedha, hivyo mahakama inawaachia huru washtakiwa wote,” alisema.
Katika shtaka la pili la kughushi, hakimu alisema hati ya usajili wa Kampuni ya Ruaha Investment upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha kwamba mshtakiwa Farijala alighushi, hivyo inamtia hatiani.
Pia mahakama hiyo ilimtia hatiani Farijala baada ya kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba aliwasilisha nyaraka hiyo ya kughushi benki, alighushi hati ya makubaliano wakionyesha kwamba wanapaswa kuhamishiwa zaidi ya Sh milioni 400 na kuiwasilisha benki na mshtakiwa huyo ndiye aliyejipatia fedha hizo kwa njia ya udanganyifu.
“Mshtakiwa wa pili Ajay hakula njama kutenda kosa, mshtakiwa wa kwanza Farijala tu ndiye aliyeghushi na kuwasilisha nyaraka zilizoghushiwa kwa nia ya kujipatia fedha, hivyo mashtaka dhidi ya mshtakiwa wa pili hayajathibitishwa.
“Jamhuri pamoja na kuwasilisha mashahidi saba mahakamani, walishindwa kuthibitisha bila kuacha shaka shtaka la kula njama na shtaka la kujipatia fedha lililokuwa linamkabili mshtakiwa wa pili,” alisema hakimu Kabwe

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles