Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imetoa wito kwa vyama vya siasa kufanya siasa zinazozingatia Sheria na utaratibu ili kuendelea kulinda amani utulivu na umoja wa kitaifa.
Hayo ameyasemal jijini Dar es Salaam leo Jumanne Agosti mosi, wakati wa kikao maalum cha Baraza la Vyama vya Siasa lililowakutanisha viongozi wa dini na wa vyama vya siasa na Msajili wa Vyama hivyo, Jaji Francis Mutungi ambapo amesema lengo ni kuelimishana namna ya kufanya siasa safi zitakazolinda utu na kujenga nchi.
Amesema wanafuatilia mwenendo wa siasa zinazoendelea nchini, hivyo wameona ipo haja ya kuwakutanisha wanasiasa na viongozi wa dini ili kuelimishina jinsi ya kufanya siasa kwa kutenganisha kazi za siasa na dini.
“Tumekutana na leo na viongozi wa dini na viongozi wa siasa kwani tumekuwa tukifuatilia siasa zinazoendelea nchini tumeona siyo nzuri na viongozi wa dini kuhusishwa kwenye siasa hizo. Ofisi ya Msajili haiwezi kuwa kila sehemu hivyo nasisitiza kuwepo na amani na utulivu kwa ajili ya nchi,”amesema Jaji Mutungi.
Amesema amelazimika kusema hayo kwa sababu Watanzania ni wamoja hivyo wawe na utaratibu ambao hautasababisha taifakuingia katika mpasuko.
Amesema mazingira mazuri aliyoyaweka Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kufanya siasa yanapaswa yatumike vizuri ili kuboresha siasa nchini, utulivu, amani na umoja wa kitaifa.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Alexander Makulilo amesema uhusiano wa siasa na dini ni changamano hivyo Serikali inapaswa kuweka Sheria ili kuratibu muungano huo.
Amesema sheria zimekataza kutumia viongozi wa dini katika majukwaa ya siasa ili kunadi sera za vyama.
“Kuwa matumizi ya lugha za uchochezi,kuzalilisha nchi, lugha za kibaguzi, lugha za kuzalilisha jinsia na lugha za kuzalilisha nchi zimepigwa marufuku na kisheria zinatambulika badala yake vyama vya siasa vinapaswa kuuza sera zake ili waungwe mkono,” amesema Profesa Makulilo.