Na GLORY MLAY- DAR ES SALAM
MSHAMBULIAJI wa timu ya JKT Queens, Fatuma Mustapha, amesema kusimama kwa Ligi Kuu ya Wanawake, ni changamoto kubwa kwao, kwani wachezaji wengi watashindwa kulinda viwango kutokana na majukumu ya familia.
Serikali imepiga marufuku kwa siku 30, shughuli zinazosababisha mikusanyiko ya watu ikiwemo michezo, ikiwa ni tahadhari ya kuzuia kusambaa kwa virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona.
Ugonjwa wa corona umesababisha vifo vya maelfu ya watu duniani, tangu uliporipuka kwa mara ya kwanza nchini China na kasha kusambaa mataifa mengine.
Kwa hapa nchini, Serikali imethibitisha watu 20 kuambukizwa, huku mmoja kati yao akipoteza maisha.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Fatuma alisema wakati huu wanakutana na changamoto nyingi ikiwemo kazi za nyumbani kwani baadhi yao wameolewa hivyo kusimama kama mama.
“Kuna wale ambao wameolewa na wanafamilia, huu ni muda wa kukaa karibu na familia zao kwa hiyo kufanya mazoezi itakuwa ni kwa muda mchache sana, kuna wengine watakuwa wanafanya kazi nyingine hasa kuwasaidia wazazi wao katika ujasiriamali.
“Lakini naamini kama mchezaji anatambua kazi yake hawezi ataiheshimu lazima apambane kuhakikisha anafikia malengo yake, watenge muda wa kazi za nyumbani pamoja na mazoezi ili kulinda viwango vyao,” alisema.