25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 29, 2021

TFS yatumia Sh milioni 600 kuelemisha jamii kanda ya ziwa

NA GAUDENCE MSUYA, Mwanza

WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS), Kanda ya Ziwa umetumia zaidi ya Sh milioni 600 kuwezesha jamii katika masuala ya elimu ya uhifadhi wa misitu, ufugaji nyuki na matumizi bora ya ardhi.

Meneja wa wakala huo Kanda ya Ziwa, Ebrantino Mgiye, jana alisema kuwa  wakala huo uliwezesha wananchi na jamii kupanda miti  ili kuboresha ardhi iliyoharibiwa, kulinda ikolojia na kusaidia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi katika mikoa ya Geita, Mwanza, Kagera, Mara na Simiyu.

“TFS ina wajibu wa kuratibu na kusimamia shughuli za uhifadhi wa misitu kwa niaba ya Serikali, inalenga kupanda miti ya kutoa mazao ya misitu, kulinda vyanzo vya maji na viumbe hai walio kwenye hatari ya kutoweka ambapo mwaka 2019/20 ilitenga fedha zilizotumika kuiwezesha jamii kupanda miche milioni mbili baada ya wakala kuotesha miche hiyo na kuigawa kwa jamii bure,”alisema Mgiye.

Alisema ili kurejesha miti iliyopotea kutokana na changamoto mbalimbali na shughuli za kibinadamu mwaka wa fedha 2020/21, TFS  imetenga Sh. milioni 200 zitazowezesha shule kuotesha na kupanda miche milioni 3.7, pia Wataanzisha bustani za mikoa ambazo zitagharimu Sh milioni 182  ili kufikia lengo la kupanda miti milioni sita kwa kanda yote.

Kuhusu uwezeshaji wa kiuchumi kwa vikundi vya kijamii vya ufugaji nyuki, alisema wametumia Sh milioni 40  kutoa elimu  kwa vikundi 124 na mizinga 200  kwa vikundi 20 kikiwemo cha Umoja wa Kusaidiana wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (UKWAMA).

Pia alisema mwaka 2019/2020 TFS ilitoa mafunzo ya ufungaji nyuki na kupanda miti kwa walemavu wasio sikia 60 ili kuwawezesha kuona namna bora ya kufuga nyuki na kuanzisha mashamba ya miti.

 “Tumefanya hivyo ili kuongeza uelewa na watambue ushiriki wao katika ufugaji na uanzishaji wa mashamba ya miti. Tumetoa madawati zaidi ya 200 kwa shule mbalimbali kusaidia kutatua changamoto hiyo, tunajenga mabweni ya wanafunzi huko Buhindi huko Buchosa tukishirikiana na halmashauri,”alisema Mgiye.

Meneja huyo wa TFS Kanda ya Ziwa alieleza  kama taasisi katika kupunguza migogoro ya ardhi kwa jamii, zaidi ya Sh milioni 200 zimetumika kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa  vijiji 13 katika wilaya za Geita na Biharamulo.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,301FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles