25.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

FAMILIA YA WEMA, DIAMOND WAPIGA KAMBI POLISI DAR

BEATRICE KAIZA NA KYALAA SEHEYE

SAKATA la baadhi ya wasanii wakubwa nchini kuhusishwa na biashara ya dawa za kulevya limezidi kuchukua sura mpya, huku wazazi wa Wema Sepetu na Nassib Abdul ‘Diamond’ wakikutana polisi kujua hatima ya watoto wao.

Wazazi hao wa wasanii hao tangu juzi wamekuwa wakishinda Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaaam baada ya Jeshi la Polisi kuwaita wasanii hao kwa mahojiano na kisha kuwaweka ndani.

Wakizungumza na MTANZANIA jana kituoni hapo wanafamilia hao walisema kwa sasa imekuwa ngumu kukaa kwenye nyumba zao bila kujua hatima ya watoto hao ambao hadi sasa wanashikiliwa na polisi.

Akizungumza huku akiwa kama mtu aliyepatwa na hamaki mama mzazi wa Wema Sepetu, alisema kwa sasa anasubiri kauli ya Polisi ili aweze kujua kama mtoto wake atafikishwa mahakamani au laa.

Alisema kitendo cha kukamatwa mtoto wake na kuwekwa ndani kimemuumiza kama mzazi ingawa kwa sasa hana la kufanya zaidi ya kusubiri uamuzi wa vyombo vya dola.

“Kama mzazi nimeumia sana ila kwa sasa ninawaomba mniache maana siwezi kuongea kitu chochote kuhusu hili, hadi hapo polisi itakapotoa maamuzi yao ya uchunguzi wanaoufanya, ndiyo nitajua nini niseme,” alisema mama Wema

Baada ya kutoa kauli hiyo mama huyo alionekana ni mtu mwenye msongo ambapo muda wote alikuwa amekaa kimya tofauti na ilivyo kawaida yake ambapo huwa ni mtu mwenye ucheshi.

MAMA DIAMOND

Wakati timu ya MTANZANIA inawasili kituoni hapo, mama Diamond, baada ya kuona waandishi wa gazeti hili walikimbilia ndani ya gari na hata alipofuatwa ili kuzungumza naye aligoma kufanya hivyo.

“Jamani kwa sasa sipo tayari kuongea chochote kile,” alisema mama huyo huku akipandisha kioo cha gari.

Baada ya mama Diamond kugoma kuzungumza alijitokeza dada wa mwanamuziki huyo, Esma Kandili ambaye ni mke wa msanii Ahmed Ngahemela maarufu kwa jina la ‘Petit Man’

“Mume wangu amekutwa na balaa hili tangu Februari 2, mwaaka huu ambapo ilikuwa siku ya kumbukumbu yangu ya kuzaliwa ni kitu ambacho sitakisahau katika maisha yangu kimeniumiza sana kuliko ambavyo watu wanadhani.

“Naumia na ninazidi kuumia kuona taarifa za uongo zinasambazwa kwenye mitandao ya kijamii zikimuhusisha na mdogo wangu Nassib, jamani watu wawe na huruma kwani sisi ni binadamu kama wao kila siku sisi wanatuombea mabaya yatukute kwenye familia yetu,” alisema.

Wazazi wa TID

Nao  wazazi wa Khaleed Mohamed ‘TID’,  walikuwepo kituoni hapo ambapo walikuwa wameandamana na familia ya Wema na Petit man, wakiwemo kaka zake wawili na mama yake mzazi ambao walionekana wako kwenye huzuni hawakutaka kuongea chochote kile na kusubiri hatima ya ndugu yao.

BABU TALE

Kutokana na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii taarifa za kuitwa polisi mwanamuziki Diamond, MTANZANIA ilimtafuta meneja wa mwanamuziki huyo, Hamis  Taletale maarufu kama Babu Tale, ili kupata ufafanuzi wa kwa nini anatajwa na hata kuzushiwa Diamond na dawa za kulevya.

“Taarifa hizo si za kweli hazijakamilika kwa kifupi Kampuni ya Wasafi imeshazoea kuzushiwa habari za uongo. Nawaomba mashabiki wa WCB wawe na amani na sisi, hatuhusiki na biashara hiyo (dawa za kulevya) ila wasiotutakia mema ndiyo kila kukicha wanazusha ili kutupoteza kwenye ramani lakini watashindwa,” alisema Babu Tale.

VANESSA, TUNDA POLISI LEO

Mbali na wasanii hao mwishoni mwa wiki iliyopita Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwataka wasanii Vaness Mdee pamoja na Tunda wajisalimishe polisi leo (Jumatatu) kwa mahojiano kuhusu tuhuma dhidi yao kushiriki biashara ya dawa za kulevya.

MTANZANIA ilimtafuta msaa Vanessa Mdee, ili kuweza kujua kama atakwenda polisi leo au laa simu yake ya kiganjani iliita bila kupokewa.

Hata hivyo taarifa zinaeleza kuwa Vanessa kwa sasa yupo nchini Afrika Kusini akirekodi tamthilia ya Sugar.

NAPE ATAKA BUSARA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema busara inatakiwa kutumika wakati wa kuwachukulia hatua wasanii waliotajwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwamba wanajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo alisema pamoja na kwamba ni rahisi kuwatambua wasanii maarufu wanaojihusisha na dawa hizo, wasanii hao wasichukuliwe hatua kwa kutumia hisia.

“Kwanza nikiri tu kwamba, tatizo la matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa na waathirika wakubwa wanaonekana kuwa ni wenye majina makubwa ingawa inawezekana kuna watumiaji wengi.

“Sisi kama wizara, suala hili tumekuwa tukilijadili na hata Serikali kwa upande wake imekuwa ikilijadili pia kwani hata wasanii kama Ray C tumewahi kuwapa fursa ya kupata matibabu ya kuacha dawa hizo.

“Sisi tunaunga mkono juhudi zozote zinazofanywa na Serikali za kupambana na jambo hilo kwa sababu lengo ni kuokoa wadau wetu. Pamoja na hayo, mjadala uliopo sasa ni namna tunavyoshughulika na waathirika, yaani tutawashitaki kwa sheria ipi wale waliowahi kuathirika na dawa hizo.

“La msingi hapa ni kutumia busara ya kushughulika na suala hili kwa sababu ni rahisi sana kutengeneza brand (alama) yako, lakini brand hiyo inaposhushwa kwa namna yoyote, inakuwa vigumu kuipandisha tena.

“Tusiwahukumu watu kwa hisia, lazima suala hili lishughulikiwe kwa kulinda haki za watuhumiwa ili ikithibitika hawahusiki na matumizi ya dawa hizo, iwe ni rahisi kwao kurejesha heshima yao,” alisema Nape.

NZOWA AMPONGEZA MAKONDA

Kamishna Mstaafu wa Jeshi la Polisi kitengo cha Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa amesifu jitihada zinazofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda za kupambana na biashara ya dawa za kulevya huku akisisitiza kuwa yupo tayari kutoa ushauri pale utakapohitajika.

Akizungumza na MTANZANIA kwa njia ya simu jana akiwa wilayani Mbozi mkoani Songwe anakoendelea na shughuli za kilimo baada ya kustaafu, alisema jitihada hizo zinapaswa kuungwa mkono na watu wote wanaowatakia mema vijana wa nchi hii.

Kuhojiwa kwa wasanii hao kunatokana na orodha ya watu 50 iliyotangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Katika orodha hiyo alitaja watu wanaouza, kutumia pamoja na kuhusika na biashara ya mihadarati, wakiwamo vigogo wa Jeshi la polisi, wamiliki wa kumbi maarufu za starehe  jijini Dar es Salaam na wafanyabishara wa dawa za kulevya.

Kwa upande wa jeshi la polisi, Makonda aliagiza aliyekuwa Kamanda Polisi Mkoa wa Kinondoni, Christopher Fuime, kukamatwa mara moja ili kuhojiwa kwa tuhuma hizo pamoja na askari 12 ambao tayari Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, amewasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi dhidi yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles