KARACHI, PAKISTAN
FAMILIA ya Waziri Mkuu wa Pakistan, Nawaz Sharif na wandani wake, wameipinga ripoti ya mahakama iliyokuwa inachunguza mali ya waziri huyo mkuu.
Familia hiyo imesema ripoti hiyo haina maana kwa kudai kuwa familia ya Sharif ina mali zisizolingana na kipato chake.
Wapinzani wa Waziri Mkuu huyo walimtaka ajiuzulu baada ya ripoti hiyo kutolewa.
Jopo la uchunguzi liliundwa na Mahakama ya Juu nchini humo kufanya uchunguzi wa madai yaliyoibuka kutokana na ufichuzi wa nyaraka za siri za Panama zilizoonesha matajiri wakubwa duniani wameficha fedha katika mataifa ya Ulaya.
Jopo hilo pamoja na mambo mengine, lilifanya uchunguzi dhidi ya familia ya Sharif kwa kipindi cha miezi miwili na kuwasilisha matokeo mbele ya mahakama juzi.
Jopo hilo lilimuhoji Sharif mwenyewe, watoto wake wawili wa kiume na mmoja wa kike na wanafamilia wengine.
Uchunguzi huo hatimaye ulifikia hitimisho kwamba kuna tofauti kubwa baina ya pato la waziri huyo na vyanzo vyake vingine vya mapato vinavyojulikana.
Wakati ripoti hiyo ikiwa bado haijawekwa wazi, kulikuwa na kurasa zilizopenyezwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii na kiongozi wa upinzani, Imran Khan akamtaka Sharif ajiuzulu kufuatia matokeo hayo, yaliyowatwisha lawama watoto wake.