25.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Familia ya Mo yaangukia umma

NORA DAMIAN na Justine Damian-DAR ES SALAAM

IKIWA ni siku ya tano tangu kutoweka kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji (43), familia yake imetangaza kutoa Sh bilioni moja kwa atakayetoa taarifa muhimu zitakazofanikisha kupatikana kwake.

Hadi sasa hakuna taarifa zozote zinazoeleza chanzo cha kutekwa kwa mfanyabiashara huyo maarufu kwa jina la Mo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemaji wa familia hiyo Azim Dewji, alisema wamefikia hatua hiyo ili kuongeza juhudi za kuhakikisha mtoto wao anapatikana mapema.

“Familia inaahidi kwamba mtoa taarifa pamoja na taarifa zitabaki kuwa za siri kubwa baina ya mtoa taarifa na familia,” alisema Dewji.

Alisema wanapitia katika kipindi kigumu na kuwaomba watu mbalimbali waendelee kuwaombea.

“Tunaishukuru Serikali na taasisi zake kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha mtoto wetu anapatikana.

“Tunavishukuru vyombo vya habari kwa kazi kubwa ya kuutaarifu umma jambo hili zito.

“Tunashukuru taasisi za dini na kila mmoja wenu kwa maombi na kutufariji katika kipindi hiki kigumu familia inachopitia. Tunaomba muendelee kutuombea,” alisema.

Alifafanua kuwa kwa mwenye taarifa awasiliane nao kupitia Murtaza Dewji kwa namba 0755030014, 0717208478, 0784783228 au kupitia barua pepe [email protected].

Katika mkutano huo Dewji aliambatana na wanafamilia wengine akiwamo baba mzazi wa mfanyabiashara huyo, Gulam Dewji, ambaye alionekana kuwa mwenye huzuni.

Hata hivyo familia hiyo haikuwa tayari kupokea maswali ya waandishi na kusema nguvu ielekezwe katika kumwombea Mo apatikane.

POLISI YABARIKI

Alipoulizwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa kuhusu uamuzi huo wa familia, alisema haoni kama kuna shida.

“Aliyepotea ni mtoto wao na kama familia wameona pengine wakitumia mbinu hiyo inaweza kusaidia, sioni kama kuna shida,” alisema Mambosasa.

Taarifa zaidi zinabainisha kuwa hivi sasa kamera za CCTV zilizoko kwenye majengo mbalimbali zinafuatiliwa kuangalia maeneo yalikopita magari yanayodaiwa kuhusika katika utekaji huo.

“Huo ni upelelezi unaendelea na huwa hatusemi kila kitu,” alisema Mambosasa.

MO NA UTAJIRI WAKE

Mo alizaliwa mkoani Singida Mei 8, 1975 akiwa mtoto wa pili kati ya watoto watano wa Gulamabbas Dewji na Zubeda Dewji.

Kwa mujibu wa Mo mwenyewe katika moja ya mahojiano  na Kituo cha televishen cha CNBC cha Afrika Kusini siku za nyuma, ilikuwa ni kwa neema za Mungu kuwa aliweza kuishi baada ya kuzaliwa nyumbani bila ya usaidizi wa daktari.

Mo alisema hospitali ilikuwa umbali wa mwendo wa saa tatu kutoka nyumbani kwao na kwa kuwa hali ya mama yake ilikuwa mbaya, alilazimika kujifungulia nyumbani chini ya uangalizi wa mkunga na si daktari.

Akiwa na umri wa miaka mitatu, Mo alikwenda mkoani Arusha ambako alisoma darasa la kwanza hadi la saba kabla ya kuja Dar es Salaam ambako alisoma katika Shule ya Kimataifa Tanganyika (International School of Tanganyika).

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alikwenda kusoma Marekani ambako alimaliza elimu ya Chuo Kikuu katika Chuo cha George Town, moja kati ya vyuo vikuu bora nchini humo kilichopo katika Jiji la Washington akichukua masomo ya usimamamizi wa fedha.

Baada ya kuhitimu elimu ya chuo kikuu, alipata kazi nchini Marekani ambapo alikuwa akilipwa Dola za Marekani 40,000 (sawa na zaidi ya shilingi milioni 80). Hata hivyo, alikuwa akilazimika kufanya kazi kwa zaidi ya saa 100 kwa wiki.

Kutokana na kutumia muda mwingi sana kufanya kazi huku akishindwa kuweka akiba kutokana na gharama za maisha katika Jiji la New York, alijikuta akimpigia simu mara kwa mara baba yake kuomba msaada wa fedha ili aweze kuishi.

Hata hivyo, baba yake alimshauri kurudi nyumbani Tanzania ambako alimweleza kuwa kuna fursa nyingi.

SAFARI YAKE YA MAFANIKIO

Alipofika Tanzania mwaka 1998, alianza kazi katika kampuni ya baba yake ya Mohamed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) kama mdhibiti wa fedha na baada ya miaka miwili alipanda cheo na kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO).

Wakati akianza kazi, mauzo ya kampuni yalikuwa Dola za Marekani milioni 30 na chini ya uongozi wake yalipanda kwa kiasi kikubwa hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 1.4 mwaka 2014.

Moja kati ya mageuzi makubwa yaliyoletwa na Mo ndani ya MeTL ni kupanua wigo wa utendaji wa kampuni kutoka inayosafirisha bidhaa kama vile mazao nje ya nchi na kuagiza bidhaa nyingine hadi kuwa na viwanda.

Mo alikuwa nyuma ya uanzishwaji wa viwanda ambavyo kwa sasa vinafika 24 vikizalisha bidhaa kama sabuni, mafuta ya kupikia, vinywaji baridi, nguo, vyakula na nyingine nyingi.

Kutokana na kukua na kuongezeka kwa shughuli za kampuni, idadi ya wafanyakazi pia iliongezeka kwa kiasi kikubwa kutoka 4,000 hadi kufikia wafanyakazi 24,000 kwa sasa.

ldadi ya wafanyakazi walioajiriwa na MeTL inakadiriwa kuwa sawa na asilimia 4 ya wafanyakazi waliopo katika sekta isiyo rasmi huku kampuni ikichangia asilimia 2 ya pato la ndani.

MeTL pia inafanya kazi katika nchi nyingine tisa ndani ya bara la Afrika ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Sudani ya Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Malawi, Zambia na Msumbiji.

Lengo la bilionea huyu kijana, ni kufikisha mapato ya kampuni Dola za Marekani bilioni 5 kufikia mwaka 2020 na kuajiri watu zaidi ya 100,000 katika nchi mbalimbali barani Afrika.

ALIVYOTEKWA

Mo alitekwa nyara na watu wasiojulikana Alhamisi iliyopita katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay, Dar es Salaam, mahali ambako amekuwa akienda kufanya mazoezi ya mwili (gym).

Hadi sasa bado haijajulikana ni nani hasa aliyemteka na wapi alikofichwa ingawa taarifa za awali zilisema tukio hilo liliongozwa na raia wawili wa kigeni.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Mambosasa, walikaririwa na vyombo vya habari wakisema kuwa walioongoza tukio hilo ni raia wawili wa kigeni.

Tayari watu 26 wanashikiliwa kutokana na tukio hilo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alikaririwa na vyombo vya habari akisema hawawezi kuruhusu vyombo vya kimataifa kufanya uchunguzi wa tukio hilo kwakuwa Jeshi la Polisi bado halijashindwa kumpata Mo.

“Tunamtafuta na atapatikana pamoja na waliomteka, tumejipanga vizuri,” alisema Lugola.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles