28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Familia kubwa kuliko zote Uingereza, inaishi bila kutegemea misaada

KUWA na familia kubwa ni kitu kilichozoeleka katika nchi za dunia ya tatu, ambazo uzazi wa mpango kwa baadhi ya jamii haupewi kipaumbele ukilinganisha na mataifa yaliyoendelea.

Katika mataifa yaliyoendelea, kwa kawaida familia nyingi huwa na watoto wasiozidi watatu, lengo ni kuwa na familia unayoweza kuikuza na kuisomesha vyema katika dunia hii ambayo kila kitu ni gharama.

Lakini kwa baadhi ya familia katika mataifa hayo, ikitokea kuna familia kubwa ambayo inashindwa kujiendesha, nyingi hujikuta zikitegemea ruzuku kutoka serikalini, kitu ambacho hakiko kwa familia hii na ndiyo kusudio la makala haya.

Tunaizungumzia familia kubwa kuliko zote nchini Uingereza, yenye mume, mke na watoto 20.

Wazazi wa familia hii na watoto wao waliwaacha watazamaji nchini humo vichwa wazi baada ya kujitokeza hadharani.

Sue Radford(42), na mumewe Noel Radford (46), wakazi wa Morecambe, Lancashire, walimtambulisha mtoto wao kitinda mimba ambaye ni mvulana Archie (11), Septemba mwaka jana na wameapa kwamba mtoto huyo ni wa mwisho kwao.

Familia ilionekana katika kipindi cha ‘This Morning’ cha Kituo cha Televisheni ya ITV nchini humo wakiwa wameijaza na kuitawala studio nzima.

Watoto walikuwa na umri kati ya miaka 28 na miezi mitatu wote walikaa na au kucheza kwa staha huku wazazi wao wakizungumza na watangazaji Eamonn Holmes na mkewe Ruth Langsford, kitu kilichosifiwa na watazamaji waliokifuatilia kipindi hicho.

Watazamaji wengi walitoa maoni yao, wakisifu makuzi ya watoto hao na namna walivyoonesha tabia njema, pongezi nyingi wakizielekeza kwa wazazi wao kwa namna walivyoweza kuilea familia hiyo kubwa.

Kina Radfords walionekana katika kipindi hicho wakijiandaa kutengeneza kipindi chao kinachoitwa ‘20 Kids and Counting.’

Wengi hasa wanawake walishangaa pia namna Sue alivyoweza kuudhibiti mwili wake wa siku zote licha ya kuzaa idadi yote hiyo, lakini pia wakishangaa kutotegemea chochote kutoka serikalini ili kuishi.

Akizungumza na This Morning, Sue anakiri kuwa ana bahati kuwa mwili wake umekuwa ukirudia hali ya kawaida kila baada ya ujauzito.

Eamonn anauliza: “Sehemu kubwa ya kina mama watasema wana mtoto mmoja, wawili au watatu ama vinginevyo na ‘imenichakaza vibaya. Lakini kwako kwa namna ulivyo tena ukiwa na watoto 20 ni maajabu makubwa! Nini siri yako?”

Sue anacheka na kujibu: “Nadhani inatokea tu kufanikiwa, mwili wangu unaonekana kurudia katika hali ya kawaida kwa sababu ya mazoezi ya kukimbia.”

Wenzi hao wanasema wana furaha kuhitimisha idadi ya watoto kwa namba nzuri ya shufwa, baada ya kumkaribisha duniani mtoto wao wa mwisho mwaka jana.

Kitinda mimba huyo, Archie mwenye umri wa miezi kumi aliungana na Chris,  Sophie, Chloe, Jack, Daniel, Luke na  Millie, Katie, James, Ellie, Aimee, Josh, Max, Tillie, Oscar, Casper, Hallie na Phoebe.

Ruth anahoji namna wenzi hao wanavyoishi ukizingatia hawapokei ruzuku yoyote kutoka serikali kuendesha familia kubwa kiasi hicho. Sue na Noel wanasema wanasaidiana na watoto wao wakubwa kuishi.

Amy mwenye miaka 11 anasema amekuwa akisaidia familia yake na kwamba hilo ni jambo linalompa presha.

Wenzi hao walikutana mara ya kwanza wakati Sue alipokuwa na miaka saba tu na walipata mtoto wao wa kwanza Chris miaka 28 iliyopita wakati Sue akiwa na miaka 14 tu.

Wenzi hao wakaamua kumlea mtoto kwa vile wote wawili walilelewa kwa njia ya kuasili.

Walihamia katika nyumba yao ya kwanza pamoja na kuoana na muda mfupi baadaye wakakaribisha mtoto wao wa pili, Sophie wakati Sue akiwa na miaka 17.

Wakaendelea kupata watoto wengine 18, ambapo wamesisitiza kwamba Archie ndio wa mwisho.

Wamepata wajukuu baada ya binti yao Sophie kujifungua mtoto na sasa ana watoto watatu.

Familia inaishi katika nyumba kubwa, Victoria House yenye thamani ya Pauni 240,000 sawa na Sh milioni 700, ambayo zamani ilikuwa ya kutunzia wazee ambayo waliinunua miaka 11 iliyopita.

Wanajivunia kutokuwa na madeni yoyote na hufurahia likizo kila mwaka.

Hutumia Pauni 300 sawa na Sh 900,000 kwa wiki kwa ununuzi wa chakula ikiwamo lita nane za maziwa, lita tatu za juisi na maboksi matatu ya nafaka yakitumika kila siku.

Wanaposherehekea siku za kuzaliwa za watoto wao, hutenga bajeti ya Pauni 100 kwa zawadi na wakati wa sikukuu ya Krismasi hutenga Pauni 100 hadi 250.

Mumewe aliwahi kufunga uzazi wakati mkewe akiwa na mimba ya tisa, lakini baadaye wakaamua kufungua wakati walipoamua kupata watoto zaidi.

Mwaka 2013, wenzi hao walionekana katika kipindi cha televisheni wakiwa na watoto 16 katika makazi yao yenye vyumba 10.

Mwaka uliofuata Radford, alipoteza mvulana aliitwaye Alfie, wakati akiwa na mimba ya wiki 23.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles