NA TUNU NASSORO -DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura), itawachukulia hatua kali wamiliki wa majengo ya makazi na biashara watakaotoza fedha za umeme zaidi ya bei elekezi inayoitoa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Mhandisi Godfrey Chibulunje, wamiliki hao wanatakiwa kutumia bei elekezi inayoelekezwa na Serikali.
Alisema kuwa wamiliki hao wanatakiwa kufuatilia bei elekezi zinazofanyiwa marekebisho mara kwa mara na kutangazwa kupitia gazeti la Serikali.
“Ni amri inatolewa kwa wamiliki wa majengo ya makazi na biashara, kwamba bei za umeme kwa ajili ya wapangaji wao isizidi bei zilizoidhinishwa na Ewura,” alisema Chibulunje.
Alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mmiliki yeyote atakayekiuka amri hiyo.
Chibulunje alisema kwa sasa bei elekezi kwa wateja wanaotumia chini ya uniti 75 kwa mwezi ni Sh 100 kwa kila uniti moja.
“Matumizi yatakayozidi uniti 75 yatatozwa Sh 350 kwa kila uniti moja itakayozidi ambapo umeme unatolewa katika msongo mdogo kwenye njia moja ya 230V,” alisema Chibulunje.
Aliongeza kuwa wateja wenye matumizi ya kawaida, hususani wa majumbani kwenye biashara ndogo, viwanda vidogo, taa za barabarani, mabango na mengineyo, bei elekezi ni Sh 292 kwa kila uniti moja.
“Umeme utatolewa kwa njia moja 230 V na njia tatu kwa 400V,” alisema Chibulunje.
Alisema kwa wenye matumizi ya kawaida ya umeme 400V na wenye matumizi zaidi ya uniti 7,500 kwa mwezi, tozo ya huduma ni Sh 14,233, bei ya nishati Sh 195 kwa kila uniti na bei ya mahitaji ya juu ni sh 15,004 kwa kila KVA kwa mwezi.
“Kwa wateja waliounganishwa katika msongo wa kati wa umeme, watatakiwa kulipia tozo ya huduma ya Sh 16,769 kwa mwezi, bei ya nishati 157 kwa kila uniti na bei ya mahitaji ya juu ni Sh 13,200 kwa KVA kwa mwezi,” alisema Chibulunje.
Aliongeza kuwa wateja waliounganishwa katika msongo mkubwa wa umeme ikijumlisha Zeco, Bulyanhulu na Twiga Cement, watalipia bei ya nishati kwa Sh 152 na bei ya mahitaji ya juu ni Sh 16,550 kwa KVA kwa mwezi.