27.5 C
Dar es Salaam
Friday, July 1, 2022

Wasaidizi kisheria wasaidia wananchi Bumbuli

Na MWANDISHI WETU -TANGA

WASAIDIZI wa Kisheria kutoka Shirika la Bumbuli Paralagel Organization (BPO), wamefanikiwa kusaidia kurudisha kisima cha maji kwenye mamlaka ya kijiji kinachotumiwa na kata nne za Halmashauri ya Bumbuli mkoani Tanga ambacho kilikuwa kwenye uongozi wa shirika binafsi kwa miaka saba.

Kisima hicho ambacho kipo Kijiji cha Dule B, kwa sasa kinatoa huduma ya majisafi na salama kwa kata za Wena, Kaivei, Kambini na Mavengero.

Akizungumza mwishoni mwa wiki mjini hapa, Msaidizi wa Kisheria kutoka Bumbuli Paralegal Organization (BOP), David Yohana, alisema walipata taarifa kuwa wananchi wa Kijiji cha Dule B na vijiji jirani vilikuwa vikipata shida ya maji safi na salama, licha ya kuwa na kisima cha maji maeneo yao.

Alisema kamati ya maji iliyokuwa na jukumu la kusimamia kisima hicho, pia ilikuwa imekaa madarakani kwa takribani miaka saba kitu ambacho ni kinyume na sheria ndogo za halmashauri.

“Sisi wasaidizi wa kisheria kutoka BOP tulichukua jukumu la kuanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu sheria ndogo za halmashauri na umuhimu wa kurudisha kisima katika mikono ya wanakijiji. 

“Juhudi zetu zilileta mabadiliko na matokeo chanya kwani wananchi waliweza kuelewa na hivyo kisima kikarudishwa kwenye mikono yao,” alisema Yohana.

Mwisho

CRDB yaja na‘Jiachie Utakavyo’

Na MWANDISHI WETU –Dar es Salaam 

BENKI ya CRDB imezindua kampeni maalumu ijulikanayo kama “Jiachie Utakavyo” ambayo wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi sasa watafurahia riba ya hadi asilimia 14. 

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkurugenzi  wa Wateja Wadogo na wa Kkati wa CRDB, Boma Raballa alisema benki hiyo imefanya maboresho katika mikopo ya wafanyakazi ili kuwapa unafuu na kuwawezesha kufikia malengo yao waliyojiwekea.

“Jiachie Utakavyo inamaanisha wafanyakazi sasa wana wigo mpana zaidi wa kukopa kwa gharama nafuu, kwa muda mrefu na uhuru wa kuchagua wanachotaka,” alisema Raballa.

Alisema benki  imempa uhuru mteja kuchagua muda wa kulipa mkopo anaoendana na matakwa yake na kiwango cha riba anachotaka kulipa. 

“Kwenye Jiachie Utakavyo mteja ana uhuru wa kuchagua muda wa kulipa iwe ni mwaka mmoja, miwili, mitatu mpaka saba, na vilevile mteja atakuwa na riba anayoitaka kuanzia asilimia 14 mpaka 16,” alisema Raballa huku akibainisha kuwa kampeni hiyo inawapa fursa wafanyakazi kukopa hadi Sh milioni 100.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi, Stephen Adili alisema benki inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi wa taasisi za umma na sekta binafsi. 

Meneja Mwandamizi Mikopo kwa Wafanyakazi, Farida Hamza alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyakazi wote nchini kuchangamkia fursa hiyo.

“Mikopo hii si kwa wateja wa Benki ya CRDB tu, ni kwa wafanyakazi wote nchini, kama mfanyakazi ana mkopo benki nyingine, Benki ya CRDB ina utaratibu wa kununua mikopo ili kuwafanya wafanyakazi wote waweze kujiachia watakavyo na benki yao pendwa ya CRDB,” alisema Farida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,419FollowersFollow
544,000SubscribersSubscribe

Latest Articles