Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameipa Uingereza muda Zaidi wa kujiondoa katika umoja huo kwa njia salama, kwa kuchelewesha mchakato wa Brexit kwa wiki kadhaa lakini bila kuondoa kitisho cha Uingereza kujiondoa bila makubaliano.
Umoja wa Ulaya umesema Uingereza inaweza kuahirisha tarehe ya kujiondoa, ambayo ilikuwa imepangwa kuwa Machi 29, hadi Mei 22 kama bunge la Uingereza litaidhinisha wiki ijayo mpango wa May wa kutalikiana na umoja huo.
Kama mpango huo uliokataliwa mara mbili utatupwa nje tena, Umoja wa Ulaya unasema Uingereza ina hadi Aprili 12 “kuja na pendekezo jingine mwafaka”. Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk amesema May ameukubali mpango huo.
Akizungumza baada ya kuhudhuria mkutano huo wa kilele wa Baraza la Ulaya mjini Brussels, May alisema bunge wa Uingereza sasa lina chaguo la kufanya kuhusu kitakachofuata.