28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

EU, Urusi, China wakiuka vikwazo vya Marekani kwa Iran

BRUSSELS, UBELGIJI

UMOJA wa Ulaya, Urusi na China zimejiweka katika nafasi ya kuvutana na Rais wa Marekani, Donald Trump baada ya kutangaza mipango ya kuiunga mkono Iran.

Mpango huo unahusisha kuanzisha njia maalumu za kurahisisha shughuli za kibiashara na Iran, hatua ambayo inakiuka vikwazo vya Marekani.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Federica Mogherini baada ya kukutana na wajumbe kutoka  Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Urusi, China na Iran juzi.

Mogherini alitangaza kwamba nchi hizo ambazo zote zimesaini makubaliano ya nyuklia na Iran zimefikia uamuzi wa kuendelea na shughuli za kibiashara na jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Alifafanua zaidi kwa kusema; “Washiriki wamesisitiza haja ya kulinda uhuru wa uendeshaji wa kiuchumi ili kuwa na fursa ya kufanya biashara kwa njia halali na Iran kwa kuzingatia kwa ukamilifu azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2231.”

Maamuzi yaliyofikiwa na nchi hiyo yanamaanisha Umoja wa Ulaya utaunda taasisi huru ya kisheria, ambayo itaratibu shughuli za kutoa na kupokea malipo ya fedha katika shughuli za kibiashara na Iran.

Mogherini aliendelea kusema kwamba kundi hilo la nchi za Ulaya, China na Urusi  limeidhinisha kwa kauli moja mapendekezo ya kiutendaji ya kuendelea kuzibakisha na kuziimarisha njia za kurahisisha mchakato wa malipo yanayohusu biashara na Iran ikiwemo ya mafuta.

Nchi zote zilizoshiriki katika mkutano uliofikia maamuzi hayo juzi ziliafiki kwamba Iran inatekeleza majukumu yake kama sehemu ya mkataba wa nyuklia uliosainiwa 2015.

Zilisema hilo limethibitishwa katika ripoti 12 mfululizo zilizowahi kutolewa na Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Atomiki (IAEA).

Lakini hatua iliyochukuliwa na nchi hizo ni dhahiri inaweka mazingira ya kuzuka mvutano mkubwa na Marekani.

Agosti mwaka huu, Marekani iliiwekea vikwazo Iran, ambavyo pia vinataja kwamba nchi yoyote au kampuni zitakazoshirikiana nayo kibiashara zitaadhibiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles