27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Escrow yamtega tena JK

Jakaya-KikweteNA EVANS MAGEGE

SASA kuna kila dalili kuwa mwangwi wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyotikisa mkutano wa 16 na 17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utaendelea kusikika kwa namna ya kuihanikiza Serikali kuwajibika zaidi.
Dalili hizi zimeonyeshwa waziwazi na baadhi ya wabunge hususani waliokuwa vinara wa kupambana na kashfa hiyo ambao hawajaridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete dhidi ya watendaji wa Serikali na viongozi wa kisiasa walioguswa na ripoti ya uchunguzi wa kashfa hiyo.
Mmoja wa wabunge walio katika mkakati huo ambao kimsingi unalenga kumng’oa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni David Kafulila wa Kigoma Kusini.

Kafulila katika mahojiano yake na MTANZANIA Jumamosi alisema hatua zilizochukuliwa na Rais Kikwete kushughulikia maazimio nane ya Bunge haziridhishi na kuongeza kuwa kabla ya kuketi kwa mkutano wa 18 wa Bunge anapaswa kuwa amemfukuza kazi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Alisema Waziri Muhongo ni muhusika muhimu katika kashfa hiyo, kwa sababu alidiriki kusimama bungeni na kulidanganya taifa kuwa fedha zilizokuwa zimehifadhiwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow hazikuwa za umma hadi uchunguzi wa vyombo vya dola ulipothibitisha pasipo shaka kuwa ni za umma.
“Hatufanyi haya kwa lengo la kumkomoa mtu, hapana kabisa. Sisi tuna dhamira ya dhati ya kutetea maslahi ya taifa kwa hiyo hatuko tayari kumuona Rais akiendelea kumuacha kiporo Waziri Muhongo.
“Rais anaonekana kusuasua kuchukua uamuzi dhidi ya Waziri Muhongo, sasa kama itatokea akashindwa kutengua uteuzi wake hadi Bunge lijalo tutawasilisha hoja binafsi ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu tukiwa na kusudio la kumng’oa kwenye wadhifa wake, hiyo ndiyo njia pekee ya kumwondoa Waziri Muhongo,” alisema Kafulila.
Alipoulizwa iwapo mkakati huo wa kumng’oa Waziri Mkuu Pinda unaungwa mkono pia na wabunge wa CCM, alisema hawezi kuzungumzia msimamo wa wanasiasa wengine hata hivyo, ujasiri waliouonyesha baadhi ya wabunge wa chama hicho wakati wa mjadala uliopitisha maazimio ya Bunge unaondoa shaka ya kupata uungwaji mkono wa kutosha.
Mbali na Kafulila, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge wa Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, alipoulizwa msimamo wake kuhusu jambo hilo, akiandika kwa maandishi kupitia barua pepe alisema anaamini Serikali itatekeleza maazimio yote ya Bunge.
Ingawa tayari Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue amekwishamsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kupisha uchunguzi dhidi yake kwa kashfa ya Escrow, bado yapo mashinikizo yanayotaka hatua zaidi zichukuliwa kwa mujibu wa maazimio nane ya Bunge.
Mbali na Katibu Mkuu Sefue, Jaji Mkuu Othaman Chande bado yuko kimya kuhusu majaji wa Mahakama Kuu walioguswa katika kashfa hiyo.
Awali viongozi wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kwa nyakati tofauti walikaririwa na vyombo vya habari wakitoa matamshi yenye mwelekeo wa kulishinikiza Bunge kuiwajibisha Serikali iwapo Rais Kikwete hatatekeleza maazimio yote nane ya Bunge.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, ndiye aliyekaririwa kwanza akieleza kuwa endapo Rais Kikwete atashindwa kumwajibisha Prof. Muhongo, wabunge walio ndani ya Ukawa watawasilisha hoja na kushawishi wengine kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu sambamba na kuitisha maandamano nchi nzima.
Wakati shinikizo hili likizidi kushika kasi, Rais Kikwete katika hotuba yake ya kufunga mwaka aliendelea kusisitiza msimamo wake wa kumuweka kiporo Prof. Muhongo kwa maelezo kuwa uchunguzi dhidi yake haujakamilika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles