26.7 C
Dar es Salaam
Saturday, February 24, 2024

Contact us: [email protected]

ENGLAND WAZIKOSA BILIONI 54/-


SAINT-PETERSBURG, URUSI        |

HATIMAYE timu ya taifa ya Ubelgiji, imefanikiwa kushika nafasi ya tatu kwenye michuano ya Kombe la Dunia nchini Urusi, baada ya jana kuwachapa wapinzani wao England mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Saint Petersburg.

Timu hizo zilishuka dimbani kuwania nafasi ya mshindi wa tatu huku leo akitarajiwa bingwa na mshindi wa pili kupatikana.

Bingwa wa michuano hiyo kati ya Ufaransa na Croatia atachukuwa kombe pamoja na kitita cha Dola za Kimarekani milioni 38, ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 86 za Kitanzania, wakati huo mshindi wa pili atachukuwa dola milioni 28, zaidi ya Sh bilioni 63.

Ubelgiji na England walikuwa wanawania nafasi ya tatu jana, hivyo ushindi wa Ubelgiji umewafanya wachukue kitita cha dola milioni 24 ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 54, huku England ambao wamemaliza nafasi ya nne wakichukuwa dola milioni 22 zaidi ya Sh bilioni 49.

Katika mchezo huo wa jana Ubelgiji ilifanikiwa kupata bao la mapema katika dakika ya nne lililofungwa na beki wao, Thomas Meunier, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Romelu Lukaku. Bao hilo lilidumu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza.

Baada ya kipindi cha pili kuanza England walionekana kupambana kutafuta bao la kusawazisha huku wakifika langoni mwa Ubelgiji mara kwa mara, lakini kocha wa Ubelgiji, Roberto Martinez, alifanya mabadiliko katika safu ya kiungo, akaingia Moussa Dembele kuchukuwa nafasi ya Youri Tielemans kwa ajili ya kwenda kupunguza kasi ya wapinzani hao.

Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kubwa kwa Ubelgiji kwa kuwa waliongeza kasi na kumpa nafasi kiungo Kevin De Bruyne kufanya anachotaka. Dakika ya 82, kiungo huyo alipiga pasi ya mwisho kwa mshambuliaji wao, Eden Hazard na kisha mchezaji huyo kuukwamisha wavuni.

Bao hilo liliwafanya England kupoteza nguvu za kupambana ili wapate bao la kufutia machozi, hivyo hadi dakika 90 zinamalizika Ubelgiji walionekana kuumiliki mchezo huo huku wakipiga pasi 674, wakati huo England wakipiga pasi 482.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles