Na Ramadhan Hassan,Dodoma
MAMLAKA ya Serikali Mtandao(eGA) imetaja vipaumbele vyake ikiwemo kupanua uwezo wa Mtandao wa Mawasiliano Serikalini na kuufikisha katika wilaya zote nchini ili kurahisisha utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao.
Hayo yameelezwa Februari 23,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Mhandisi Benedict Ndomba wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka hiyo kwa mwaka 2023.
Mkurugenzi huyo ametaja kipaumbele kingine kuwa ni kuendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa Taasisi zote za umma.
“Ikiwa ni pamoja na kupitia na kukagua miradi na Mifumo ya TEHAMA ya kimkakati, kisekta na kitaasisi,”amesema Mkurugenzi huyo.
Kipaumbele kingine ni kupitia na kutathmini hali ya usalama wa mifumo na miundombinu ya Serikali Mtandao na kuzishauri Taasisi za Umma katika maeneo ya kuboresha, pamoja na kufuatilia utekelezaji wake.
“Kuendelea kuunganisha Mifumo ya Taasisi za Umma kwenye Mfumo wa Serikali wa Kubadilishana Taarifa (Government Enterprise Service Bus – GovESB).
“Kuendeleza shughuli za tafiti na ubunifu katika matumizi ya teknolojia mpya za TEHAMA ili kuibua huduma mpya kwa umma na kuwezesha matumizi sahihi ya teknolojia mpya zinazoibuka,”amesema Mhandisi Ndomba.
Amekitaja kipaumbele kingine ni kujenga mifumo tumizi ya Kisekta kwa kushirikiana na Sekta husika na kuiwezesha kubadilishana taarifa na mifumo ya sekta nyingine pale inapohitajika.
“Kupitia mradi wa Tanzania ya kidijitali, wilaya zote zitaunganishwa na mtandao wa Serikali na zitakuwa na uwezo wa kufanya shughuli zao kupitia mtandao.
“Mradi huu upo katika hatua za manunuzi na tunatarajia ndani ya miezi 18 hadi 24 hali za halmashauri kimtandao zitaboreka,”amesema.
Amesema mpaka sasa Ofisi zote za Makatibu Tawala wa Mikoa wameshahamia katika matumizi ya Serikali mtandao.
Amesema Ili kuondokana na tatizo la mtandao kuwa chini hatua zilizochukuliwa ni kuweka mfumo utakaofuatilia halmashauri na vituo vinavyotoa huduma ili kuona kweli kama mtandao uko chini.
“Itakuwepo eGA, TAMISEMI na ofisi zingine zenye huduma hizo. “Vile vile tutahakikisha kwamba TAMISEMI inaanza kutumia mfumo ambao utaondoa mchakato wa kwenda kuomba Control Namba na badala yake atakuwa anajihudumia mwenyewe kupata namba hiyo,”amesema Mhandisi Ndomba.