23.2 C
Dar es Salaam
Sunday, March 26, 2023

Contact us: [email protected]

Wenye ulemavu wa kuona waomba Serikali kutatua changamoto ya uhaba wa walimu

Na Clara Matimo, Mwanza

Watu wenye ulemavu wa kuona wamesema bado kuna changamoto kubwa ya uhaba wa walimu wenye taaluma ya watu weye mahitaji maalumu hususani wasioona hivyo wameiomba Serikali kuongeza walimu hao.

Ombi hilo limetolewa jijini Mwanza  leo Februari 23, 2023 na Mshauri wa Jumuiya ya Maendeleo ya  wasioona  Tanzania James Shing’wenye wakati akisoma risala kwa niaba ya wasioona kwenye maadhimisho ya kitaifa ya siku ya braille.

Amesema changamoto hiyo inachangiwa na uhaba wa vyuo vya ualimu vinavyotoa mafunzo ya elimu maalumu pamoja na kutokuwa na motisha kwa walimu wa elimu maalumu maana wanaofundisha watoto  wenye ulemavu wana kazi kubwa zaidi kulinganisha na wanaofundisha wasiokuwa na ulemavu.

“Katika kuboresha upatikanaji wa elimu kwa wasioona tunaiomba Serikali kuongeza vyuo vya ualimu vya elimu ya mahitaji maalumu ikiwezekana iwe ni somo la lazima katika vyuo vyote vya ualimu pia iongeze motisha kwa walimu wa elimu ya mahitaji maalumu ili wawe na moyo wa kufundisha watoto wenye ulemavu pamoja na wasioona hii itasaidia kuongeza idadi ya walimu watakaopenda kujifunza elimu ya mahitaji maalumu,”amesema Shing’wenye.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amewataka wadau wa watu wenye ulemavu kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali wanayoitekeleza inayowajumuisha watu wenye ulemavu na wasioona pia amesisitiza kushirikisha kundi hilo kwenye miradi wanayoiandaa.

“Serikali imeendelea kuyapa kipaumbele masuala ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na masuala ya elimu, uwezeshwaji wa kiuchumi, afya na ajira katika kuzingatia takwa la sheria kwa watu wenye ulemavu kupitia Tamisemi hivyo wazazi na walezi tafadhari sana msiwafiche wala kuwanyanyapaa watoto  wenye ulemavu.

 “Serikali ya awamu ya sita  chini ya Mheshimiwa Rais  Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa watu wenye ulemavu imezindua Mwongozo wa Taifa wa Utambuzi wa Mapema na Afua stahiki kwa watoto wenye ulemavu wa mwaka 2021 pia Mwongozo wa Utekelezaji, Ujumuishwaji na Uimarishaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu wa mwaka 2022,”amefafanua Malima.

Malima amesema  kwa mwaka 2022 serikali imeandikisha watoto 2,883 wenye ulemavu katika elimu ya awali ambapo wasichana 1,413, wavulana 1,470,  Shule ya Msingi 3,318 na MEMKWA 122.

“ Serikali imeajiri Kada ya walimu nafasi 9,800  za afya 7612 ambapo jumla ya watu wenye ulemavu 261 sawa na asilimia 2.7 walikidhi vigezo na kupata ajira ya ualimu  kati yao 61  ni wasioona,”ameeleza Malima.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu  Joy Maongezi amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na wadau imetoa Fimbo nyeupe 35, viti mwendo 35mafuta kinga 35 miwani kwa wanafunzi 174, Essilor  glasses 174,miwani yenye lenzi inayobadilika kulingana na mionzi ya jua 172, monocular 268, makasha ya miwani 183, mabegi 341 pamoja na viungo bandia kwa watu 179 vyenye thamani ya Sh milioni 118,552,000 kutoka Taasisi ya Lohana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa maafisa Elimu wa Elimu maalumu Issa Kambi, amesema wao ni kiini cha maandishi ya Braille  hivyo wataendelea kujitoa kwa hali na mali katika kusimamia elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mwenyekiti wa chama cha wasioona Tanzania, Omar Itambu  amesema elimu kwa wasioona hapa nchini ilianza mwaka 1950 jijini Dodoma chini ya kanisa la Anglikana, mtu wa kwanza kupata elimu hiyo alikuwa Paul Milangasii na imekuwa ni mkombazi kwa wasioona ambapo aliwaasa wazazi na walezi wenye watoto walio na ulemavu kuwapeleka shuleni ili wapate elimu.

Maadhimisho ya kitaifa ya maandishi ya Braille hufanyika Januari 4,  kila mwaka, mwaka huu 2023 yameongozwa na kauli mbiu isemayo  ‘Eneza Ufahamu Kuhusu Umuhimu wa Braille.’ ambapo  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima alikabidhi jumla ya fimbo nyeupe 150.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,184FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles