27.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

ECOWAS INAWEZA KUFUNDISHA UJASIRI BARANI BARANI AFRIKA?

rais

NA RAS INNO,

SARAKASI za kisiasa zinazoendelea nchini Gambia huenda zikabadilishwa mwelekeo wa kubinuka (somersault), ikiwa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) itatuma jeshi lake la dharura (ESF) kuzima kiburi cha Rais kigeugeu Yahya Jammeh aliyeshindwa uchaguzi huru aliousifia mwenyewe, kuwa wa haki kuliko wowote uliowahi kufanyika uliosimamiwa na tume aliyoiteua mwenyewe.

Jammeh aliyetawala kwa miongo miwili na ushei aliyeingia madarakani kwa Mapinduzi ya kijeshi alibadilika na kupinga kauli aliyoitoa awali si tu kwa Adama Barrow aliyemshinda lakini pia hata kwa hotuba kwenye luninga, kukubali kushindwa uchaguzi na sasa anataka kulitumbukiza taifa hilo dogo masikini katika mgogoro kwa tamaa yake ya madaraka. Jammeh (51) aliyeshindana na mpinzani wanayelingana kiumri alipata asilimia 36.7 ya kura zote zilizopigwa, Barrow alijizolea asilimia 45.5 na Mama Kandeh aliambulia asilimia 17.

Katika kilichoashiria wimbi jipya katika ukanda wa Afrika Magharibi, kwa viongozi walioko madarakani kukubali matokeo ya uchaguzi wanaposhindwa lililoanzishwa na Goodluck Jonathan aliyeshindwa dhidi ya Mahammudu Buhari.

 Lakini sasa Jammeh ambaye ni Mhafidhina wa Kiislamu aliyetamka kuwa kudumu kwake madarakani ni kwa mapenzi ya ‘Allah’ amegeuka akipingana na matakwa ya Allah, aliyekiri kuwa ametimiza mapenzi yake kwa kuwezesha muungano wa vyama saba vya upinzani kushinda anatia doa wimbi jipya la demokrasia katika ukanda huo kutokana na kugeuka ghafla na kupinga matokeo ya uchaguzi aliyoyakubali hapo awali.

Lakini ikiwa ECOWAS itafanikiwa kuingilia kijeshi sarakasi zinazoendelea nchini Gambia baada ya juhudi za kidiplomasia kushindikana, itaandika historia inayoweza kubadili sura ya namna migogoro ya kisiasa inavyoshughulikiwa barani Afrika na pengine kuzishawishi jumuiya nyingine zikiwamo SADC na IGAD kuwa na misimamo thabiti dhidi ya viongozi wenye ukaidi wa kukubali kushindwa kwenye chaguzi zenye mchakato halali wa upigaji kura.

Azimio la ECOWAS lililotolewa mwishoni mwa mwaka jana linahimiza uingiliaji kati wa kijeshi kama Jammeh atakataa kukabidhi madaraka, kwamba jeshi la jumuiya hilo limepewa mamlaka kamili kuhakikisha usalama wa Rais Mteule Barrow, kuapishwa kwake kwa mujibu wa Katiba ya Gambia na kuwalinda viongozi wengine wa kisiasa na wananchi wa taifa hilo kwa ujumla.

Mwenyekiti wa sasa wa jumuiya hiyo Rais Ellen Johson-Sirleaf alisaini uidhinishwaji wa azimio hilo lililofikiwa katika kikao cha 50 cha dharura cha viongozi wa nchi zinazounda umoja huo kilichofanyika Abuja nchini Nigeria, linalobainisha wazi kuwa jeshi la ESF likiingilia kati litatakiwa kuendelea na doria hadi wakati itakapothibitika kuwa hakuna figisu zozote zinazomzuia Rais Mteule Barrow kutimiza majukumu yake baada ya kuapishwa.

Lakini inavyoelekea azimio hilo linasababisha kufuruma kwa sintofahamu kwa kuwa Jammeh ambaye tangu alipoingia madarakani kijeshi ameshinda chaguzi nne kabla ya kushindwa huu wa sasa, ametishia kuwa jaribio lolote la kumng’oa kwa nguvu litachukuliwa kuwa uvamizi lakini akijinasibisha na mfa maji anayetapatapa kwa kuwa jumuiya nyingine zenye wigo mpana zaidi ikiwamo Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN) zinaunga mkono mikakati ya ECOWAS.

Katika kudhirisha hilo jeshi hilo la ECOWAS litakalotumwa kuingilia kati litagharamiwa kwa michango ya jumuiya hiyo, lakini pia msaada wa kifedha kutoka Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Uchumi ya Ulaya na wafadhili wengine. Licha ya hatima ya kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo iliyosikilizwa jana na Mahakama Kuu ya Gambia kwa dhamira ya kuzuia uapishwaji wa Rais Mteule Barrow mnamo Januari 19, siku moja baada ya muda wa utawala wa Jammeh kumalizika rasmi lakini hata matokeo yaliyokaguliwa na kusahihishwa makosa madogo yaliyotokea bado yanampa ushindi wa asilimia 43 dhidi ya asilimia 39 za Jammeh, huku mkuu wa tume hiyo huru ya uchaguzi Aliue Momar Njai amebainisha wazi kuwa madai ya Jammeh hayana mashiko.

Kuna mambo kadhaa yanayoweza kujiri katika kutanzua mkanganyiko huu wa Gambia ambao baadhi ya viongozi wa Mataifa ya Afrika Magharibi wameuvalia njuga kuutatua wakiwamo marais wa Nigeria, Liberia, Ghana na Sierra Leone waliomshawishi Jammeh kuachia madaraka kwa amani lakini amewakaidi.

Hata baadhi ya mabalozi wa Gambia katika nchi mbalimbali duniani  wakiwamo wa China, Uturuki, Marekani, Urusi, Uhispania, Ethiopia, Senegal, Guinea Bissau, Cuba na Ubelgiji wote wamemsihi Rais wao kuthamini mustakabali wa taifa hilo kuliko matakwa yake binafsi.

Bado kuna sintofahamu kuhusu mustakabali wa taifa hilo dogo lililogubikiwa lindi kubwa la umasikini likiwa katika nafasi ya 168 kati ya mataifa 187 kwenye orodha ya mataifa yanayojipapatua kukua kiuchumi huku robo tatu ya wananchi wake wakiishi katika umasikini mkubwa. Kuna mgawanyiko unaoyumbisha jeshi ambalo awali lilisemekana kumuunga mkono Rais Mteule Barrow, lakini katika siku za hivi karibuni nalo limegeuka na kutangaza utii kwa Jammeh ambapo Mkuu wa Majeshi Jenerali Ousman Badjie ametamka kusimama bega kwa bega na Jammeh baada ya tishio la ECOWAS kupeleka majeshi, akidhihirisha tamko lake kwa majeshi kudhibiti ofisi za tume ya uchaguzi jijini Banjul wakati mkuu wa tume hiyo akitokomea kusikojulikana kwa kuhofia usalama wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles