KINASHASA, DRC
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linalowahudumia watoto, Unicef likishirikiana na washirika wao limetangaza orodha ya watoto 155 ambao wamepoteza wazazi wao au waliachwa bila mlezi kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola uliotokea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Katika taarifa iliyotolewa na shirika hilo nchini humo, Unicef inasema idadi hii inawajumlisha watoto ambao wamepoteza mzazi mmoja, wawili au wanaowatunza ambao walifariki dunia kutokana na Ebola pamoja na wale ambao waliachwa bila mlezi baada ya wazazi wao kutengwa na kuwekwa katika vituo vya matibabu.
Taarifa inaendelea kusema kuwa watoto ambao hupoteza wazazi wao kutokana na Ebola wanapata machungu mengi moyoni kwani hunyanyapaliwa, hutengwa na pia hushuhudia mzazi wake au mlezi wake akifariki dunia na hilo ndilo jambo linalowasumbua.
Mwakilishi wa Unicef nchini DRC, Dk. Gianfranco Rotigliano, anasema kumpoteza mzazi au mtu wa karibu inaweza kuwa hali ngumu kwa mtoto na jukumu lao kama Unicef ni kuwalinda na vile vile kusaidia watoto wote ambao wameathirika na virusi vya Ebola.
Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani (WHO), limetoa idadi mpya ya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini DRC tokea mwezi Agosti.
Msemaji wa WHO, Fadela Chaib, akiwa mjini Geneva Uswisi Ijumaa, aliwaambia waandishi wa habari kuwa hadi Septemba 18, idadi kamili ya visa vya Ebola vilivyoripotiwa ilikuwa 143, huku 112 vikibainishwa kuwa Ebola ambapo watu 91 wamepoteza maisha.