Na EVANS MAGEGE,
WABUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wanatarajia kupitisha sheria ya kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) ili kupambana na mauaji ya watu hao katika eneo hili la Afrika.
Hatua hiyo imetokana na wabunge wa EALA kupitisha juzi azimio la kuzitaka nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuungana katika mapambano ya kuwadhibiti wahalifu wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya watu hao.
Azimio hilo ambalo lilipitishwa katika kikao chao kilichofanyika mjini Zanzibar, litawasilishwa kwa mara ya kwanza kama muswada binafsi (EAC Private Members Bill) katika vikao vya Bunge hilo vya mwezi ujao.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, Mbunge wa EALA kutoka Tanzania, Shy-Rose Bhanji, alisema lengo la kutungwa sheria ya kuwalinda watu wenye ulemavu ni kuwahakikishia haki na usalama wao ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati (EAC).
“Nina furaha ya kuwajulisha kuwa Bunge la Afrika Mashariki limepitisha azimio la kuzitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuungana kwa pamoja katika kupambana na kuwadhibiti vikali wahalifu wote wanaojihusisha kuwanyanyasa na kuwashambulia walemavu wa ngozi katika nchi zote wanachama.
“Azimio hilo limefuatia hoja niliyowasilisha jana(juzi) katika kikao cha Bunge huko Zanzibar na kuungwa mkono na Mbunge Aboubakar Zein wa Kenya na Nusura Tiperu kutoka Uganda,” alisema Shy-Rose.
Alisema azimio hilo linalitaka Baraza la Mawaziri wa EAC kutoka nchi wanachama kufanya kila linalowezekana kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kuwa na usalama wa kutosha na kuharakisha uchunguzi wa kesi za mauaji na vitendo vingine viovu.
Aliongeza kuwa azimio hilo pia limezitaka Serikali za nchi wanachama kutoa vifaa vya kinga ya jua na huduma nyingine za muhimu za kiafya kwa walemavu wa ngozi. Vile vile wapatiwe nafasi za upendeleo katika ajira, elimu na nafasi za ngazi ya maamuzi.